Pole za Soudy Brown, Fid Q kwa Diamond zawatoa ‘povu’ watu

Muktasari:

  • Meneja wa Diamond, Babu Tele, anasema msanii huyo licha ya tukio lililompata yuko salama na buheri wa afya huku akiendelea na shoo zake kama ilivyo-pangwa.

Kama ulidhani vile vijembe kati ya mtangazaji maarufu Soudy Brown na msanii wa Bongo Fleva, Farid Kibanda ‘Fid Q’ dhidi ya tamasha la Wasafi vingewatengenezea chuki utakuwa unajidanganya, kwani wameweza kutoa pole zao baada ya msanii Diamond Platinumz kudondoka akiwa jukwaani.

Tukio la kuanguka jukwaani kwa Diamond lilitokea juzi katika uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga, akiwa katika mwendelezo wa tamasha la Wasafi, ambalo mpaka sasa limeshafanyika katika mikoa ya Mtwara, Iringa, Morogoro na Rukwa (Sumbawanga). Akiwa jukwaani kuimba wimbo wa ‘Zilipendwa’ na wasanii Rayvanny na Mbosso, Diamond aliyekuwa kifua wazi huku amevalia suruali yenye ufito mweupe pembeni, ubao uliowekwa chini ya jukwaa ulisogea na kujikuta anaanguka kwa kutumbukia chini ya jukwaa, jambo lililozua gumzo mitandaoni.

Licha ya kudondoka, meneja wao, Babu Tale alisema vijana wake waliendelea kuimba wakiwa chini ya jukwaa. Miongoni mwa waliotoa pole kwa Diamond ni Soudy Brown na Fid Q.

Wawili hao kipindi ambacho kulikuwa na mchuano mkali wa kufanyika siku moja kwa tamasha la Wasafi mkoani Mtwara na lile la Fiesta jijini Dar es Salaam, kwa nyakati tofauti walionekana kurushiana vijembe.

Fid Q aliyekuwa mmoja wa wasanii waliopangwa kutumbuiza Fiesta ambayo baadaye iliahirishwa, aliingia katika majibizano na Babu Tale, baada ya kuonekana katika tangazo akiwa analisifia tamasha hilo.

Kitendo hicho kilitafsiriwa na Tale kama kejeli kwao na kumtuhumu Fid Q kuwa licha ya kuwa msanii wa siku nyingi, hamiliki hata gari, jambo ambalo msanii huyo alimjibu na kueleza kuwa mafanikio kwake si magari ingawa anayo mengi.

Katika ukurasa wake, Fid Q aliandika; “Poleni wana..siku zote hakuna kazi isiyokuwa na changamoto..Aluta Continua”.

Kwa upande wa Soudy Brown jana katika pole zake aliandika, “Tuweke ushilawadu pembeni, pole sana muuza karanga, pole na maumivu pole kwa ajali, I hope pole hiyo kupokewa kiroho safi na Diamond kwa kumjibu ‘Thank you brother.”

Baadhi ya walioona posti hizo za pole za Soudy na Fid Q, walikuwa na mtazamo tafauti ambapo wengine waliwapongeza na wengine kuwaponda na kuwaambia waache unafiki. Mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la His exellency Fande, alimsifu Fid Q na kusema ameonyesha ukomavu na ndio maana ya kuitwa mkongwe.

Kwa waliosoma zile za Soudy, wapo waliolisema ni unafiki kwa kuwa tangu tamasha hilo lianze hawajawahi kuandika chochote iweje baada ya kumuona Diamond kaanguka ndipo afanye hivyo. Mwananchi lilizungumza na Babu Tele ambaye alisema msanii wake pamoja na tukio hilo lililompata yuko salama akiwa buheri wa afya.

Awali tamasha la Wasafi mkoani Rukwa lililofanyika Sumbawanga lilipangwa kufanyika Jumamosi, lakini lilishindikana kutokana na mvua badala yake likafanyika Jumapili bila ya kiingilio.