NDANI YA BOKSI: Ray C, hata mtandao wa Instagram ni unga

Ray C

Mtungi wote ulikwisha kichwani na kupata hasara mara mbili. Ndiyo, hasara ya pesa niliyotumia kununua kinywaji kilichotoweka kichwani kwa wakati huo, na hasara ya kusikia maneno ya kuumiza.

Mshikaji anadondosha chozi kwa ajili ya kiumbe wa kike. Ni mzuri, ndiyo. Pengine mzuri sana kuliko wasichana kibao wanaozurura katika mabaa na barabara ya jiji hili la Dar es Salaam.

Ndiyo. Lakini, ukweli ni kwamba yeye ni mmoja wao. Na yeye alikuwa amemuokota kama alivyowahi kuokota wasichana wengine kadhaa waliotangulia kabla ya huyu aliyemuumiza.

Ni mida ya jioni Jumapili iliyopita niko Kinondoni kwenye baa moja maarufu yenye umri mdogo sana tangu kufunguliwa kwake. Watu kibao wakiumiza makoo kwa pombe na meno kwa mifupa ya nyama choma.

Watu wako ‘bize’ kiasi kwamba wamepoteza kumbukumbu na imani yote ya kama kuna kifo. Kila nimuonaye ana uso wenye nuru ya kipuuzi yenye kumpa mtu jeuri ya kuamini kuwa hakuna shida.

Niko na mshikaji anameremeta shavuni kibwege kwa umande wa machozi. Siyo machozi ya furaha kama Wafaransa na Kombe la Dunia, hapana. Huyu ni machozi ya kutendwa na mkewe. Kuumizwa.

Simulizi yake inakera kwa tabia anazofanyiwa na mkewe. Jamaa ana wakati mgumu sana, ni miongoni mwa watu wasio na furaha duniani. Uso umejenga urafiki na kifo cha kujitakia. Alipofikia, sumu na kitanzi kwake siyo tatizo, bali ni suluhisho.

Jamila (Jina siyo halisi) ana haki gani ya kumfanyia vile mshikaji (mumewe)? Nilijiuliza baada ya kushuhudia chozi jingine na kilio cha kwikwi kwa mshikaji. Jamila ni nani zaidi ya msichana mwingine?

Mwisho nilimpuuza na michozi yake nikahamia kaunta kuendelea kuuvuruga ubongo kwa mtungi. Ni baada ya kuniambia huyo Jamila alimpata kupitia mtandao wa Instagram na kumfanya mke rasmi. Nilifuta na namba yake kabla sijalewa zaidi.

Mtu mwenye akili zake timamu hawezi kuoa mke wa mtandaoni. Hawezi kuwa na demu muuza sura mitandaoni. Sikatai kuwa nao ni viumbe walioumbwa na Mungu, lakini wenye ukaribu zaidi na shetani.

Wanawake mnafanya dunia iwe hivi. Hebu fikiria dunia bila wanawake au mabinti ingekuwaje? Ingekuwa dunia ya kipuuzi sana aisee. Sitamani hilo litokee hata kwa nusu saa ya dunia bila totozi.

Pengine Mwana FA mpaka leo asingetoka kimuziki. Mabinti walimfanya awe miongoni mwa wanamuziki wa kizazi kipya. Ukitaka ufanikiwe haraka sana kimuziki, waimbie hawa viumbe kina “Hawa”.

Magereza yasingekuwepo. Wengi wao waliopo jela wamefungwa kwa sababu ya kuwaridhisha wanawake zao kifedha. Pale wanapoona bila pesa wataishia kuwaita shemeji, wanaamua kufanya lolote.

Kuna walioiba, kupora, kutapeli, kuua kwa ajili ya mapenzi, na wenye maovu mengine mengi ambao chanzo kilikuwa ni wanawake. Ndani ya muda mfupi siku za karibuni kuna askari wengi wamejiua kwa sababu ya viumbe hawa.

Asilimia kubwa wanaume hununua magari kwa sababu ya wanawake kurahisisha usafiri. Bila hivyo wallah wengi wasingenunua. Totozi zinakulazimisha pesa ya kununulia kiwanja na tofauti elfu tatu, uamue kununua ndinga kwanza.

Halafu sijui nao wamerogerezewa kwenye magari. Hata mwanaume akiwa na gari la kubebea maiti ilimradi kuna viti, basi kwao burudani. Totozi na ndinga ni kama siasa na rushwa.

Mitindo na nyumba za fasheni zisingekuwepo. Wabunifu kama Gucci na wengine wangekuwa wapasua mbao. Ubunifu upo kwa ajili yao hawa wanaume ni kama kulazimisha.

Pia vitu kama poda, wanja na vinginevyo vingi visingekuwepo. Changamoto nyingi na maendeleo ya dunia hii yanaletwa na wao, bila wanawake magari ya kifahari yangekuwa ya kazi gani?

Bila wao hakuna kidume wa kwenda kwenye majumba ya filamu. Msela gani wa kukaa sehemu zaidi ya saa mbili kuangalia igizo huku akitafuna bisi?

Kila kitu kizuri kipo kwa ajili ya mwanamke. Wao ndio wanunuaji wakubwa wa bidhaa zote. Wananunua chakula kwa wingi kuliko uwezo wao wa kula. Wananunua nguo na viatu kwa wingi kuliko muda wanaotumia kuzurura. Wanavaa vitu vingi mwilini kuliko ukubwa wa miili yao.

Nywele za kuvaa. Nyusi za kupaka. Kope za kubandika. Sikioni kuna hereni. Mkononi kuna bangili. Shingoni kuna mkufu na kiunoni cheni au shanga. Mguuni kuna vikuku. Pia kucha zote za kuvalishwa.

Hapo hujaongelea mavazi na mafuta pamoja na mapambo mengine yasiyo ya lazima. Mwanamke ni pambo la dunia. Wameumbwa hivyo na miili yao inaruhusu kupambwa kwa maneno na vikolombwezo.

Ukitaka utajirike haraka uza bidhaa kwa ajili ya wadada. Hawa ndio wameifikisha dunia hapa ilipo. Wao ndio chanzo cha uchungu na chanzo cha utamu pia. Wanafanya dunia iwe hivi ilivyo kama ni mbaya au nzuri.

Wanawake ni maua. Wanaleta furaha duniani na hufanya wanaume wafurahie maisha au wasifurahie. Nenda sehemu walipo wanaume tupu, eneo hilo lazima lijenge urafiki na uchafu kuanzia watu mpaka mazingira.

Wanawake ni jeshi kubwa sana. Na kwa wingi wao kama kila mmoja akisimama kwenye nafasi yake dunia itabarikiwa. Kwa maana hata Mwenyezi Mungu anamsikiliza zaidi mwanamke. Lakini ndivyo sivyo kwa sasa.

Hivi sasa imekuwa tofauti sana. Sidhani kama wanawake wote wanasikilizwa siyo tu na Mungu, bali hata shetani mwenyewe hataki kuwasikiliza. Wanafanya mambo ambayo shetani hata miaka 1,000 mbele hatakuja kuyafanya.

Kuna wanawake wa dunia ya sasa kama shetani angewafuata kama Hawa wa Adam, shetani angeshangaa anakutana nao njiani wakimfuata na kumrubuni yeye ili aje kuiteketeza dunia na viumbe wake.

Wanawake wa mjini hivi sasa shetani wao ni mitandao. Utandawazi umekuwa shetani kamili kwa wanawake wengi kuliko shetani mwenyewe wa kuzimu kama siyo ahera.

Yule aliyemrubuni Eva anatakiwa arudi shuleni kusomea upya elimu ya kurubuni wasichana ili awe sawa na mitandao ya kijamii. Akili ya wasichana wengi hivi sasa ipo mitandaoni.

Huko ndiko kunakofanya wanawake wafanye lolote ili waonekane. Kuanzia wake za watu na wengineo wengi tu huko mitaani wanashikiwa akili na maisha ya mitandao. Wamekuwa mateja mtandao.

Rehema Chalamila ‘Ray C’ baada ya kuishinda vita ya matumizi ya dawa za kulevya, sasa ameingia kwenye vita nyingine ambayo hii haina ‘sober house’ wala ‘methadone clinic’. Matumizi mabovu ya mitandao.

Ray C anataka jamii ya Instagram imheshimu. Anataka watoto wa Instagram ambao wengi wao akili mbovu na umri mdogo wa kuwazaa wamtambue yeye ni nani na kapata ustaa lini.

Akili za mitandaoni zimeshaua ndoa nyingi sana. Zimevuruga biashara na mapenzi kama siyo uchumba na siri kibao za watu. Mitandao imeua watu kwa sababu ya akili zilizopo huko.

Ray C hii leo hawezi kujibishana na watoto wa Instagram. Watu wazima wenzake huwezi kuwakuta wanachangia kwenye kurasa za wapuuzi wengi wa insta. Ray C anataka kushindana nao.

Watu wameathirika na mitandao hii. Sakata la Munalove na kifo cha mtoto wake, ukichunguza mwanzo mwisho ni mitandao iliyofanya haya yafikie hapa. Muna naye ni wale mitandao na umaarufu wake upo huko zaidi ya mitaani.

Shetani huyu wa mitandao anataka mtu ule chakula kama cha Kempiski kila siku. Kuanzia breakfast mpaka dinner. Hivyo ndivyo vyakula wanavyoposti wehu mitandao. Wewe utaanzaje kuposti ugali na dagaa? Akili za mtandao hufanya mtu hata msibani uache kumlilia aliyefariki, uanze kuwaza juu ya nyumba ya Mabibo kama itafaa kwa msiba au ukafanyie Mikocheni ulikopanga.

Maisha ya mtandao yanakufanya uogope mpaka kivuli chako.

Maisha ya mtandao hivi yanawafanya watu washinde ndani kutwa nzima kama hawana kitu. Kwa sababu akitembea mitaani ataonekana tofauti na kile anachokionyesha mitandaoni siku zote.

Watu wamekuwa mateka. Watumwa. Waumini na wafungwa wa mitandao. Wamemua kujipa shida kwenye maisha kwa sababu wanataka kuishi kimtandao. Dada’angu Ray C usiende huko, tulia.

Kama Ray C amerudi kwenye ubora wake baada ya mapambano ya matumizi ya dawa za kulevya atambue kwamba maisha ya mitandao au akili za mitandaoni kama utaziendekeza na kutaka kushindana nazo ni sawa na kuanza upya matumizi ya dawa za kulevya.

Mitandao ina mateja wengi kuliko mateja wa unga mitaani. Tofauti ya mateja wa mitandaoni na wa unga, wale wa mitandaoni hawana dhambi. Hawana kasoro. Siyo maskini. Hawana matatizo wala hawali chakula kibaya. Wamekamilika kama malaika.

Mateja wa akili za mtandao ni malaika kamili. Hawana kasoro. Ukitaka kupasua kichwa waendekeze. Ukitaka amani na kufanya shughuli zako kwenye ubora na utulivu puuza wapuuzi wa mitandao. Instagram ni dawa za kulevya pia. Shituka Ray C.