Wasanii wa filamu wamshangaza waziri Zanzibar

Muktasari:

  • Waziri Kombo amewashangaa wasanii hao kutochangamkia soko la filamu lililozinduliwa leo

Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabith Kombo  amesikitishwa na wasanii wazawa kutofika kwa wingi katika soko la filamu lililozinduliwa leo mjini Zanzibar maarufu Discop.

Discop ni tamasha kubwa linalohusu biashara ya michezo ya televisheni na ununuzi wa hakinakili za filamu.

Kombo amesema katika uzinduzi huo wamejaa wasanii kutoka Nigeria, Ethiopia, Kenya na Afrika Magharibi wakati tukio lenyewe linafanyika Tanzania.

Amesema Watanzania wachache hata wa Kenya na Waganda wametuzidi na atashangaa sana akisikia wasanii wa kitanzania wakilalamika kuwa hawajapata taarifa, atajiuliza nchi nyingine wamepataje.

Waziri Kombo amesema wasanii wa Kitanzania wamelala katika kuchangamkia fursa, halafu ndio wakwanza kulalamika kuwa Serikali haiwapi fursa wala majukwaa ya kimataifa  kwa ajili ya kutangaza kazi zao.

Amesema Discop ni mara ya kwanza kushiriki tamasha la ZIFF na ndio utaratibu uliowasaidia Hollywood na Bollywood kunyanyuka katika soko la filamu hivyo kama wakitaka Bongowood na Zollywood basi wachangamke.