Taifa Stars yashikwa

Wednesday November 20 2013

By Sweetbert Lukonge, Mwananchi

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeendeleza unyonge wake mbele ya Zimbabwe baada ya kulazimishwa sare 0-0 jana katika mchezo wa kirafiki wa Kimataifa uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tangu 1982, Tanzania na Zimbabwe zimekutana mara tisa, huku Stars ikishinda mechi moja 2-0, mwaka 1990, wakifungwa mara tano na kutoka sare mara tatu.

Kwa mujibu wa takwimu za viwango vya  ubora wa soka duniani  vilivyotolewa na Fifa mwezi uliopita, Taifa Stars inakamata nafasi ya 129, wakati Zimbabwe ipo katika nafasi ya 102.

Katika mchezo wa jana Zimbabwe walipata bao dakika 90, lakini mwamuzi Ronnie Kalema kutoka Uganda alikataa kwa madai mfungaji alikuwa ameotea.

Katika mchezo huo ulioshuhudiwa na mashabiki wachache, Stars watajilaumu wenyewe baada ya washambuliaji wake kukosa nafasi kadhaa za kufunga dhidi ya Zimbambwe iliyokaa kambini kwa siku moja kabla ya mchezo huo.

Kocha Kim alimwanzisha kwa mara ya kwanza kiungo mpya wa Yanga, Hassan Dilunga katika mchezo huo na baadaye alimwingiza chipukizi mwingine Farid Mussa.

Taifa Stars iliuanza mchezo huo kwa kasi na dakika ya kwanza, Mwinyi Kazimoto na Thomasi Ulimwengu walishindwa kuunganisha krosi nzuri ya Ngassa.

Stars ilikuwa ikicheza mfumo wa 4-4-2 kama ilivyokuwa kwa wapinzani wao Zimbabwe, huku viungo chipukizi Frank Domayo, Dilunga na Kazimoto walicheza kwa ushirikiano mkubwa na kuwapoteza wapinzani wao.

Washambuliaji wa Stars, Ulimwengu, Samatta na Ngassa walipoteza nafasi nyingi za kufunga.

Advertisement