#WC2018:Watanzania vinara Afrika kuona Kombe la Dunia

Muktasari:

Ripoti iliyotolewa na taasisi ya utafiti ya GeoPoli, inaonyesha mashindano hayo mwaka huu yanafuatiliwa kwa karibu na asilimia 73 ya Watanzania, namba ambayo ni kubwa zaidi inayoifanya iongoze na kuzipiku timu zilizofuzu fainali hizo.

Dar es Salaam. Licha ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ kutoshiriki Fainali za Kombe la Dunia 2018, Tanzania imeweka rekodi ya kuwa nchi inayoongoza raia wake kufuatilia kwa karibu mashindano hayo kuliko nyingine yoyote Afrika.

Ripoti iliyotolewa na taasisi ya utafiti ya GeoPoli, inaonyesha mashindano hayo mwaka huu yanafuatiliwa kwa karibu na asilimia 73 ya Watanzania, namba ambayo ni kubwa zaidi inayoifanya iongoze na kuzipiku timu zilizofuzu fainali hizo.

Licha ya kufuzu fainali hizo ambazo pazia lake linafunguliwa rasmi leo, idadi kubwa ya raia wa Senegal, Morocco, Nigeria, Misri na Tunisia wamezidiwa na Tanzania ambayo hata kufuzu Fainali za Kombe la Afrika (Afcon) imekuwa mlima mrefu kwake.

Mara ya kwanza na mwisho Tanzania kucheza Fainali za Afrika ilikuwa mwaka 1980, zilizochezwa mjini Lagos, Nigeria.

Asilimia hiyo 73 ya Watanzania ambayo imekuwa ikifuatilia mashindano hayo ni sawa na idadi ya Watanzania 43 milioni kati ya 59 milioni ambayo ni namba inayokadiriwa kuwa na idadi ya jumla ya raia wote wa Tanzania kwa sasa.

Ripoti ya GeoPoll inaonyesha Nigeria inashika nafasi ya pili katika orodha ya nchi zenye idadi kubwa ya wafuatiliaji wa Kombe la Dunia mwaka huu ambapo asilimia 68 ya raia wake wamekuwa wakifuatilia mashindano hayo kwa karibu.

Wakati Ghana ikishika nafasi ya tatu kwa asilimia 60 ya raia wake kufuatilia Kombe la Dunia, Kenya inashika nafasi ya nne ambapo asilimia 55 ya raia wa nchi hiyo wamekuwa wakifuatilia mashindano hayo.

Katika hatua nyingine, ripoti hiyo imeainisha kuwa mamilioni ya Watanzania watatazama mechi za mashindano hayo wakiwa nyumbani na sio kwenye sehemu za starehe kama baa au kumbi ambazo huonyesha mechi za soka kama ilivyozoeleka. Tofauti na miaka ya nyuma ambapo idadi kubwa ya mashabiki wa soka walikuwa wakitazama mashindano makubwa kama hayo kwenye kumbi za starehe, mabanda ya mitaani na baa, safari hii maeneo hayo huenda yakawa na watu wachache huku wengi wao wakishuhudia mechi hizo nyumbani.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Utafiti ya GeoPoll iliyofanya utafiti wa muitikio wa Bara la Afrika kwa Kombe la Dunia, Watanzania asilimia 61 wataangalia wakiwa nyumbani, huku asilimia mbili wakitarajia kutazama kwenye maeneo ya wazi.

Asilimia sita tu ya Watanzania watakaofuatilia fainali hizo, watatazama mechi wakiwa baa au migahawa, wakati mashabiki ambao wataangalia wakiwa maofisini ni asilimia mbili.

Katika hali ya kushangaza, ripoti hiyo imeonyesha asilimia 16 ya Watanzania watakaotazama fainali hizo, wataangalia wakiwa na marafiki zao huku asilimia 8 ya mashabiki wa soka ikishindwa kuthibitisha wapi itatazama mechi za Kombe la Dunia mwaka huu.

Ripoti hiyo imekwenda mbali zaidi kwa kufafanua wanawake wa Tanzania watapendelea zaidi kutazama mechi nyumbani ambapo asilimia 72 wanatarajiwa kufanya hivyo na watakaokwenda kwa marafiki zao ni asilimia 11 .

Kwa upande wa mashabiki wa wanaume ambao wataangalia mechi za mashindano hayo asilimia 60 watakuwa mbele ya luninga za nyumbani na wanaotegemewa kwenda kwa marafiki zao ni asilimia 12.

Tathmini fupi iliyofanywa na gazeti hili, imebaini kitendo cha idadi kubwa ya vituo vya luninga hapa nchini kupata haki za kuonyesha mashindano hayo kumechangia uwezekano wa Watanzania wengi kutazama mechi hizo wakiwa nyumbani.

Tofauti na fainali zilizopita ambapo vituo vichache vya luninga Afrika vilipata haki za matangazo ya Kombe la Dunia.

Hali imekuwa tofauti kwa sasa ambapo vituo vingi vimepata haki hizo jambo ambalo linawapa fursa watu kutazama mechi za mashindano hayo wakiwa nyumbani.

Pia idadi kubwa ya vituo hivyo vimepunguza gharama ya malipo ya ving’amuzi na kuweka bei ambayo kundi kubwa la Watanzania wanamudu kulipa tofauti na zamani ambapo wachache hasa wamiliki wa baa na kumbi za kuonyesha mpira walimudu kulipa gharama.

Mbunge wa Jimbo la Malindi na wakala wa soka anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Ally Saleh alisema ripoti hiyo licha ya umuhimu wake, kuna maeneo ambayo ina dosari.

“Kimsingi takwimu zinapingwa kwa takwimu hivyo naheshimu waliofanya utafiti huo wameonyesha jinsi gani Watanzania wanavyofuatilia vyombo vya habari, pia inathibitisha kuwa vyombo vyetu vya habari vinatimiza wajibu wake wa kutuarifu umma wa Watanzania kinachoendelea kuhusu fainali hizo.

Lakini kwa upande mwingine ripoti inanipa mashaka hasa inapoonyesha asilimia 61 wataangalia mechi wakiwa nyumbani wakati kiuhalisia kundi kubwa la Watanzania hawana luninga majumbani kwao, lakini kingine ni kwamba wengi wao wanapenda kutazama mechi kwenye mkusanyiko wa watu,” alisema mbunge huyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Dodoma (Dorefa), Mulamu Nghambi alisema ripoti hiyo inapaswa kufanyiwa kazi kwa vitendo na nchi ili mchezo wa soka upige hatua.

“Kwa kutaja Tanzania inaongoza kwa raia wake kufuatilia habari za Kombe la Dunia, maana yake Watanzania wanapenda mpira wa miguu licha ya nchi yetu au nyingine zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara kutoshiriki mashindano hayo,” alisema Nghambi mmoja wa vigogo waandamizi wa klabu ya Simba.