#WC2018: Rekodi bora yaibeba Senegal

Muktasari:

Baada ya kuanza vyema fainali hizo kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Poland, makocha na wachambuzi wa soka nchini wameipa nafasi kubwa Senegal kurudia au kupata mafanikio kama ilivyokuwa fainali za mwaka 2002.

Senegal iliifunga Poland mabao 2-1 katika mechi ya kwanza kwa wawakilishi hao wa Afrika.

Dar es Salaam. Mzimu wa mafanikio wa miaka 16 iliyopita huenda ukaibeba Senegal kulinganisha na timu za Morocco, Misri, Tunisia na Nigeria katika Fainali za Kombe la Dunia.

Baada ya kuanza vyema fainali hizo kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Poland, makocha na wachambuzi wa soka nchini wameipa nafasi kubwa Senegal kurudia au kupata mafanikio kama ilivyokuwa fainali za mwaka 2002.

Katika fainali zilizofanyika Korea Kusini na Japan, Senegal licha ya kushiriki mara ya kwanza, ilifanya maajabu kwa kuingia robo fainali kabla ya kufungwa na Uturuki bao 1-0 katika dakika 30 za nyongeza.

Kocha na mchambuzi wa soka, Kennedy Mwaisabula aliliambia gazeti hili jana, upo uwezekano Senegal kufanya vizuri kwenye fainali hizo kutokana na namna kikosi chake kinavyocheza kulinganisha na timu nyingine kutoka Afrika. “Ukitazama benchi la ufundi Senegal, lina wachezaji watano waliokuwemo kwenye kikosi kilichofanya vizuri mwaka 2002 kwenye Kombe la Dunia wakiongozwa na kocha mkuu, Aliou Cisse aliyekuwa nahodha.

“Hawa nadhani wanachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Senegal katika kuwajenga kisaikolojia wachezaji na kuwapa hamasa ya kupambana na kujitolea. Wameisuka vizuri timu kuanzia safu ya ushambuliaji ambayo ina kasi kubwa na imekuwa na wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu katika kutengeneza nafasi, kufunga na kufanya uamuzi pindi wanapokuwa na mpira wakiongozwa na Sadio Mane.

Lakini pia safu yao ya ulinzi inacheza kwa kujitolea na nidhamu kubwa inayochangia isifanye makosa ya mara kwa mara. Uwepo wa Cisse na wenzake una mchango mkubwa katika hili kwa sababu wao pamoja na wachezaji wanaelewa vyema falsafa na utamaduni wa nchi, lakini hata hivyo ni rahisi kuwasiliana. Hata rekodi zinaonyesha kuwa nchi nyingi zinazotwaa Kombe la Dunia zinakuwa zinaongozwa na makocha wazawa, naamini Senegal itafika mbali,” alisema Mwaisabula.

Kocha wa Alliance Academy FC iliyopanda Ligi Kuu Tanzania Bara, Kessy Mziray alisema licha ya ugumu wa mashindano hayo, Senegal ina nafasi kubwa ya kuitoa kimasomaso Afrika.

“Kwanza Senegal wana morali ya hali ya juu, lakini wachezaji wanajituma na kupambana bila kuchoka kwa dakika zote za mchezo.

Nafahamu mechi zote za mashindano ni ngumu, lakini Senegal wana nafasi kubwa ya kufika mbali. Hata hivyo naweza kusema Kombe la Dunia mwaka huu lina mabadiliko makubwa na lina msisimko kwa sababu nchi nyingi zilizokuwa na uwezo wa chini zinafanya vizuri, watazame Japan,” alisisitiza Mziray.

Pamoja na ushindi wa mechi ya kwanza dhidi ya Poland, Senegal ina kibarua kigumu cha kuhakikisha inafanya vyema kwenye mechi mbili zinazofuata dhidi ya Japan na Colombia ili kufuzu hatua ya 16 Bora.

Uwepo wa kundi kubwa la wachezaji wanaocheza soka la kulipwa Ulaya kama ilivyokuwa mwaka 2002, unaonekana kuwa faida kubwa kwa Senegal kutokana na kiwango cha uzoefu na uwezo wa hali ya juu kusoma na kukabiliana na mbinu za timu pinzani kama walivyoonyesha dhidi ya Poland.

Kama ilivyokuwa kwenye Kombe la Dunia mwaka 2002 ambalo Senegal iliingia bila kupewa nafasi kubwa, kiwango walichoonyesha dhidi ya Poland kimeonekana kuwapa matumaini Waafrika tofauti na awali na timu zilizopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mashindano hayo kabla ya kuanza ni Nigeria na Misri.

Wakiwa kwenye Kundi A lililokuwa linaundwa na timu za Denmark, Ufaransa waliokuwa mabingwa watetezi na Uruguay, Senegal walishtua dunia baada ya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo na kufuzu hatua ya 16 Bora kabla ya kusogea hadi robo fainali walipokwamia dhidi ya Uturuki.

Ikiwa na kikosi kilichoongozwa na Cisse na wenzake ambao sasa ni wasaidizi wake katika kuinoa timu hiyo, Omary Daf, Lamine Diatta na Tony Silva, Senegal ilianza kwa kuifunga Ufaransa bao 1-0 kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Denmark na ilifunga hesabu kwa kutoka sare ya mabao 3-3 na Uruguay.

Misri imepokea vipigo kwenye mechi mbili na Uruguay waliofungwa bao 1-0 kabla ya kulala dhidi ya Russia kwa mabao 3-1. Nigeria ilianza vibaya kwa kufungwa mabao 2-0 na Croatia.

Wawakilishi wengine Afrika, Morocco walifungwa bao 1-0 mechi ya ufunguzi dhidi ya Iran na jana Ureno idadi hiyo huku Tunisia wakipoteza mbele ya England kwa mabao 2-1.