#WC2018: Andersson: Ibrahimovic amehusika, nani kasema?

Muktasari:

Ibrahimovic ametangaza kustaafu kucheza soka la kimataifa mwaka huu

Moscow, Russia. Kocha wa mkuu wa Sweden, Janne Andersson amesisitiza kikosi chake hakihusiani chochote na nyota wa LA Galaxy, Zlatan Ibrahimovic aliyetangaza kutundika daluga, kuichezea timu ya taifa, baada ya kumalizika kwa fainali za Euro 2016.

Kauli ya Andersson wakati kikosi chake kikijiandaa kucheza mechi yao ya kwanza katika mashindano ya mwaka huu, dhidi ya Korea Kusini.

Kocha huyo, anayefahamika kwa misimamo yake amesema Ibrahimovic hayupo katika akili zao na wala hawahitaji msaada wake wa aina yoyote.

Andersson alisema Ibrahimovic pamoja na wachezaji wengine walipotangaza kuachana na timu ya taifa, waswidi waliheshimu uamuzi wake na hivyo ifahamike kuwa kwa sasa hana nafasi ya aina yoyote katika kikosi cha Sweden kilichopo nchini Russia.

"Niliheshimu uamuzi wake, kila mtu aliheshimu uamuzi wake, kwetu ni zaidi ya nembo ya taifa, lakini ieleweke kuwa hatumhitaji kwa sasa, tunajiamini, tumejiandaa na tuko kwa mambamano bila yeye," alisema Andersson.

Aidha kambi ya Sweden imekumbwa na matatizo kadhaa ambapo hivi karibuni kuliibuka taarifa kwamba, uwanja wao wa mazoezi ulioko huko Gelendzhik, ulitengwa kwa ajili ya kuvizia mazoezi ya timu pinzani. Katika tuhuma hizo, kiongozi wa msafara, Lars Jacobsson, alidaiwa kukodi nyumba kwa ajili ya kuivizia South Korea ikifanya mazoezi.

Sweden wataingia dimbani, katika uwanja wa Nizhny Novgorod, siku ya jumatatu kuumana na South Korea wakiwa na kikosi imara yenye matumaini makubwa ya kufanya vizuri.