#WC2018: Hali ya Dele Alli yazidi kutia shaka Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Alli aliumia paja katika mechi ya kwanza dhidi ya Tunisia na kuna uwezekano mkubwa akapumzishwa katika mechi ijayo dhidi ya wawakilishi hao wa Concacaf itakayofanyika Jumapili.

Kiungo huyo wa Tottenham Hotspurs aliumia nyama za paja katika mechi ya kwanza ya England dhidi ya Tunisia iliyoisha kwa ushindi wa mabao 2-1 kwa vigogo hao wa barani Ulaya.

 

Saint Petersburg. Kiungo wa England, Dele Alli ameshindwa kufanya mazoezi leo wakati shaka kuhusu uwezekano wake kuwa timamu kucheza mechi ijayo ya Kombe la Dunia dhidi ya Panama ikizidi kuongezeka.

Alli aliumia paja katika mechi ya kwanza dhidi ya Tunisia na kuna uwezekano mkubwa akapumzishwa katika mechi ijayo dhidi ya wawakilishi hao wa Concacaf itakayofanyika Jumapili.

Panama ilipoteza mchezo wa kwanza ilipofungwa mabao 3-0 na Ubelgiji, na hata kama akiwa fiti, Gareth Southgate anaweza kuamua kutompanga katika mechi hiyo itakayofanyika Nizhny Novgorod ili kupumzisha.

Ruben Loftus-Cheek na Marcus Rashford wote wanasubiria nafasi hiyo ya kucheza pembeni, baada ya wawili hao kumvutia kocha walipotokea benchi katika mchezo dhidi ya Tunisia.

Alli aliandika katika akaunti yake ya Twitter Jumatano akisema: "Inachanganya kupata jeraha dogo Jumatatu. Nitafanya kila ninaloweza kurudi katika hali ya kawaida mapema iwezekanavyo!"

Southgate mwenyewe ana tatizo la kimwili baada ya kuteguka bega alipokuwa akifanya mazoezi jana, ingawa leo ameonekana kutosumbuliwa na tatizo hilo.