#WC2018: Neymar azusha hofu

Muktasari:

Kuumia kwake katika mechi dhidi ya Uswisi kulimfanya jana ashindwe kuendelea na mazoezi kwenye uwanja wa the Yug Sport Stadium, mjini Sochi wakijiandaa kucheza na Costa Rica hapo kesho.

Sochi, Russia. Kujitonesha kwa mshambuliaji tegemeo na nahodha wa Brazil, Neymar kumezusha hofu kwa mashabiki wa taifa hilo.

Kuumia kwake katika mechi dhidi ya Uswisi kulimfanya jana ashindwe kuendelea na mazoezi kwenye uwanja wa the Yug Sport Stadium, mjini Sochi wakijiandaa kucheza na Costa Rica hapo kesho.

Brazil iliyo katika kundi E, inalazimika kushinda mechi zake zilizosalia ili ijihakikishie kucheza raundi ya pili kutokana na kuanza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Uswisi.

Nyota huyo wa klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa, alikua nje ya uwanja tangu Februari mwaka huu, akiuguza jeraha la mguu, jana alikiri kujisikia maumivu katika mguu huo.

Kuumia kwa Neymar na kushindwa mechi ya robo fainali katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2014,  kuliwatoa wachezaji wenzake mchezoni na hivyo kupigwa mabao 7-1 na Ujerumani.

Ni kutokana na kumbu kumbu hiyo mbaya ndio maana mashabiki wa Brazil wameingiwa na kihoro ingawa mshambuliaji huyo ameahidi kushuka dimbani kesho.

Wakati Neymar akiwa katika hatihati, mshambuliaji Philippe Coutinho aliyewafungia bao katika mechi iliyopita, ameahidi kupambana kupata matokeo hapo kesho.