#WC2018:Argentina wakimtegemea Messi pekee, wamekwisha!

Muktasari:

Messi (30), ataongoza kampeni ya kikosi cha Argentina kwa mara nyingine tena, ambapo ratiba inaonesha watashuka dimbani kukabiliana na Iceland, Croatia na Nigeria kwenye Kundi D, huku dalili zikionesha kuwa Argentina itamtegemea sana Messi kupata mafanikio yao nchini Russia.

Moscow, Russia. Mlinda mlango wa Argentina, Nahuel Guzman amewataka wachezaji wenzake, kumpunguzia presha nahodha wao, Lionel Messi katika fainali za Kombe la Dunia, inayoanza kutimua vumbi leo.

Messi (30), ataongoza kampeni ya kikosi cha Argentina kwa mara nyingine tena, ambapo ratiba inaonesha watashuka dimbani kukabiliana na Iceland, Croatia na Nigeria kwenye Kundi D, huku dalili zikionesha kuwa Argentina itamtegemea sana Messi kupata mafanikio yao nchini Russia.

Kutokana na hilo, Guzman, ambaye alichukua nafasi ya Sergio Romero (majeruhi) kikosini, amewatahadharisha wachezaji wenzake kuhusu madhara ya kumtegemea Messi, kwani macho ya wapinzani wao yatakuwa kawa nyota huyo wa Barcelona.

"Kila mtu anaufahamu uwezo wa Messi. Kila mtu anajua umuhimu wake kikosini, tunafahamu anavyotamani kubeba kombe hili, lakini hiyo isiwe sababu ya kumuwekea mzigo. Tukifanya hivyo tumekwisha," alisema Guzman.

Ikiwa na matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia, kwa mara ya kwanza baada ya miaka 32, Argentina itaanza kampeni yao, siku ya Jumamosi, watakaposhuka dimbani, dhidi ya Iceland.