#WC2018:Hatimaye Kombe la Dunia hili hapa

Muktasari:

Kule Russia sasa, wenyeji watacheza pambano la kwanza la dhidi ya Saudi Arabia huku michuano hii ikiwa ya 21 tangu kuanzishwa kwake na itajumuisha jumla ya timu kutoka mataifa 32. Kati ya mataifa hiyo, 20 yalikuwapo Brazil kwenye fainali zilizopita.

NDIO, hatimaye zile fainali za Kombe la Dunia hizi hapa tena. Ni baada ya miaka minne kupita huku mara ya mwisho likiwa limechezwa Brazil na Ujerumani ikabeba ndoo kwa kuibwaga Argentina.

Kule Russia sasa, wenyeji watacheza pambano la kwanza la dhidi ya Saudi Arabia huku michuano hii ikiwa ya 21 tangu kuanzishwa kwake na itajumuisha jumla ya timu kutoka mataifa 32. Kati ya mataifa hiyo, 20 yalikuwapo Brazil kwenye fainali zilizopita.

Iceland na Panama zitakuwa zikishiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza katika historia. Jumla ya mechi 64 zitachezwa katika viwanja 12 vilivyo katika miji 11. Mechi ya fainali itachezwa katika Uwanja wa Luzhniki Julai 15.

Uwanja huo ndio ambao ulitumika kwa fainali za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya katiya Manchester United na Chelsea mwaka 2008.

Hadi kufikia fainali zilizopita, nchi 77 zilikuwa zimeshiriki katika michuano hii tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930. Kati ya nchi hizo, ni 12 tu ndio zimefanikiwa kucheza fainali huku nchi nane tu zikiwa zimetwaa taji hilo.

Brazil inaongoza kwa kutwaa taji hilo mara tano wakati Ujerumani na Italia zinafuatia kwa kutwaa taji hilo mara nne kila moja. Bahati nzuri kwa Brazil ni kwamba Italia haikufuzu katika michuano hii lakini kama Ujerumani ikifanikiwa kutetea taji lake, basi itaifikia Brazil kwa kuchukua taji hilo mara tano. Hata hivyo, katika historia ni Italia tu ndio timu pekee ambayo imewahi kutetea taji hilo baada ya kulitwaa mwaka 1934 na kisha wakalitetea tena mwaka 1938.

Mabingwa wengine katika michuano hiyo ni Uruguay na Argentina ambazo ziliwahi kutwaa mara mbili wakati England, Ufaransa na Hispania, kila moja imechukua mara moja. Ujerumani ilichukua mara ya mwisho mwaka 2014 lilikuwa la kwanza kwao kuchukua wakiwa taifa moja.

Iliyokuwa Ujerumani Magharibi ilitwaa mara tatu nyuma. Mwaka 2014, Ujerumani ilikuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa huo katika ardhi ya Marekani ya Kusini, wakati mwaka 2010 Hispania ilitwaa ubingwa huo Afrika huku mwaka 2002 Brazil ikiwa nchi ya kwanza kutwaa ubingwa Asia. Brazil pia ilikuwa nchi ya kwanza ya Marekani ya Kusini kutwaa ubingwa huo Ulaya wakati kizazi cha akina Pele kilipofanya hivyo mwaka 1958 kule Sweden.

Hii itakuwa michuano ya kwanza kufanyika Ulaya tangu ilipofanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2006 kule Ujerumani na itakuwa michuano ya kwanza kufanyika katika ukanda wa Ulaya Mashariki huku ikiwa ni mara ya tisa kwa michuano hii kufanyika Ulaya.

 Kwa mara ya kwanza katika michuano hii, Fifa imepitisha matumizi ya msaada wa teknolojia katika matukio ya utata baada ya mchezo wa soka kuendelea kukumbwa na matukio mengi tata yanayozigharimu timu mbalimbali.

Katika fainali za mwaka 2006, ukijumlisha watu waliotazama mechi za michuano hiyo iliyofanyika Ujerumani, inakadiriwa watu 26.9 bilioni walitazama fainali hizo huku 715 milioni wakiitazama mechi ya fainali kati ya Ujerumani na Ufaransa.

Waamuzi 36 wa kati wanatazamiwa kuchezesha fainali hizi huku wakiwa na wasaidizi 63.Waamuzi 13 watakuwa wanasimamia fainali hizi kupitia video.