#WC2018: Blatter awajaribu FIFA

Bosi wa zaman wa FIFA Sepp Blatter.

Muktasari:

Blatter anatumikia kifungo cha kutojihusisha na mambo ya soka ikiwemo kutoingia uwanjani kwa kipindi cha miaka sita alichohukumiwa Desemba 2015 kutokana na sakata la kashfa ya rushwa iliyolikumba Shirikisho hilo.

Moscow, Russia. Katika kile kinachoonekana kama kuwajaribu viongozi wa Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA), bosi wa zamani wa shirikisho hilo, Sepp Blatter, ametua nchini Russia kama alivyoahidi hivi karibuni.

Blatter anatumikia kifungo cha kutojihusisha na mambo ya soka ikiwemo kutoingia uwanjani kwa kipindi cha miaka sita alichohukumiwa Desemba 2015 kutokana na sakata la kashfa ya rushwa iliyolikumba Shirikisho hilo.

Awali kifungo chake kilikua cha miaka minane, lakini baadaye  Kamati ya maadili ya FIFA ikampunguzia na kubaki miaka sita, baada ya kutopatikana na hatia ya moja kwa moja ya kimadili, ingawa aliidhinisha malipo ya dola mil 1.35 Rais wa UEFA wakati huo na aliyekuwa makamu wake Michel Platini.

Uamuzi wa Blatter kutua jijini Moscow kipindi hiki zinapoendelea mechi za fainali za Kombe la Dunia kwa kisingizio kuwa ni mgeni rasmi wa Rais wa Russia, Vladmir Putin ni kama kuwajaribu FIFA.

Blatter anayeaminika kuchangia kwa kiasi kikubwa Russia kupewa uenyeji huu wa fainali za Kombe la Dunia 2018, anatarajiwa kuushudia mchezo wa leo kati ya Ureno na Morocco utakaopigwa saa 9:00 alasiri.