Dakika 10 zinavyoitesa Afrika

Kiungo wa Peru Pedro Aquino (kushoto), akiwania mpira na nyota wa Ufaransa, Paul Pogba, katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Dunia, uliochezwa jana usiku. Ufaransa ilishinda bao 1-0. Picha na AFP.

Muktasari:

Timu za Afrika zimekuwa na tatizo la kufungwa mabao ya dakika za mwishoni katika Kombe la Dunia.

Dar es Salaam. Wakati Nigeria ikikabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Iceland itakayoamua hatima yao kwenye Fainali za Kombe la Dunia, timu hiyo ina kibarua kingine cha kuchunga dakika 10 za mwisho kwenye mechi hiyo.

Timu za Afrika zimekuwa na tatizo sugu la kupoteza umakini dakika 10 za mwisho kabla ya filimbi ya mwisho na kujikuta zikiruhusu mabao yaliyochangia kupoteza mechi kwenye mashindano hayo yanayoendelea nchini Russia.

Rekodi isiyovutia kwa timu za Afrika kuruhusu mabao ya dakika za ‘jioni’ kwenye fainali za mwaka huu ilianzia kwa Misri ambayo licha ya kuibana Uruguay kwenye mechi ya raundi ya kwanza, ilijikuta ikifungwa bao katika dakika ya 89 ya mchezo ambalo lilidumu hadi filimbi ya mwisho.

Bao hilo lililofungwa kwa kichwa na beki wa Uruguay, Jose Gimenez lilitokana na mpira wa faulo iliyosababishwa kwa uzembe na Mohamed Abdel-Shafy aliyemsukuma mfungaji ambaye hakuwa na madhara pembezoni mwa uwanja.

Pia dakika hizo za majeruhi ziliendelea kuwa na nuksi kwa timu za Afrika baada ya Morocco kuruhusu bao pekee la ushindi kwa Iran katika mchezo wa raundi ya kwanza.

Bao hilo alijifunga beki Aziz Bouhaddouz dakika za nyongeza alipokuwa kwenye harakati za kuokoa shambulizi la wapinzani wao.

Kana kwamba haitoshi, Tunisia nayo iliingia kwenye mtego wa kufungwa bao dakika za mwisho iliporuhusu bao la ushindi dhidi ya England, June 18 lililofungwa na Harry Kane na kufanya mechi hiyo kumalizika kwa England kupata ushindi wa mabao 2-1.

Katika hali ya kushangaza, Senegal nayo iliruhusu bao dakika ya 86 ya mechi yao dhidi ya Poland ingawa ilipata mabao mawili ya mapema yaliyofanya iibuke na ushindi wa mabao 2-1.

Udhaifu huo wa timu za Afrika kuruhusu nyavu zao kutikiswa dakika za mwishoni umekuwa ni tatizo sugu ambalo limekuwa likiziandama pindi zinaposhiriki Kombe la Dunia.

Mwaka 2002, Senegal ilijikuta ikifungwa bao la kizembe na Uturuki katika muda wa dakika 30 za nyongeza ambalo lilikatisha ndoto ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufuzu hatua ya nusu fainali.

Huku ikipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi, Senegal ilitawala mchezo kwa kiasi kikubwa katika dakika zote 90 za mchezo zilizomalizika kwa matokeo ya sare, lakini kupoteza umakini kwenye muda wa nyongeza, kuliifanya ifungwe bao dakika ya 94 ambalo lilihitimisha mechi hiyo kutokana na sheria ya ‘bao la dhahabu’.

Kucheza kwa umakini na tahadhali kubwa hasa dakika za lala salama ndio kunaonekana kama silaha muhimu kwa Nigeria dhidi ya Iceland leo, mchezo ambao inalazimika kupata ushindi utakaoweka hai matumaini yao ya kufuzu hatua ya 16 bora.

Baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Croatia kwa kufungwa mabao 2-0, Nigeria ‘Super Eagles’ inaweza kujikuta ikiungana na ndugu zake Morocco na Misri zilizoaga mapema ikiwa itapoteza mechi ya leo, pia hata sare yoyote haitakuwa nzuri kwao kwa kuwa itapaswa kusubiri miujiza ya mechi za mwishoni.

Kocha Joseph Kanakamfumu alisema kinachochangia timu za Afrika kuruhusu mabao ya dakika za mwishoni ni kupoteza umakini na nidhamu.

“Ni kukosa nidhamu tu kwa sababu hao wachezaji wa timu za Afrika, wengi wanacheza soka la kulipwa Ulaya na wanafundishwa hivi vitu, lakini wanashindwa kuvifanyia kazi wakiwa kwenye timu za Taifa kulinganisha na wenzao ambao muda wote wa mchezo wanahakikisha wanatimiza kile walichoelekezwa.

Lakini, kingine inaonyesha kuwa timu na wachezaji wetu hawana umakini kwa sababu katika mbinu za mchezo, mojawapo ni kuhakikisha timu hairuhusu bao katika robo nne za mechi zenye dakika 15 ambazo ni zile za mwanzoni kipindi cha kwanza na cha pili na zile dakika 15 za mwishoni katika vipindi hivyo vyote viwili. Ni jambo la kawaida kutokea lakini kwa timu zetu inaonekana limezidi kwa sababu tunapoteza umakini,” alisema Kanakamfumu.

Kocha wa Prisons, Mohammed Abdallah ‘Bares’ alisema kinachoziangusha timu za Afrika hadi kupelekea kufungwa mabao ya dakika za mwishoni ni kiwango cha utimamu wa mwili.

“Wachezaji wa timu za Afrika wengi hali yao ya ufiti iko chini lakini wanafanya makosa ya kizembe ambayo yanawagharimu wanapokutana na timu kutoka mabara mengine,” alisema Bares.