#WC2018: Kipa Pickford ajiandae makombora ya Croatia

Muktasari:

  • Campos alisema kipa huyo amefanikiwa kuibeba England kwa kiasi kikubwa tangu michuano hii ianze, akichomoa michomo mingi, lakini kuna haja ya kujiandaa kisaikolojia kwa sababu Luca Modric, Ivan Rakitic na Mario Mandzuikic sio watu wa mchezo mchezo.

Moscow, Russia. Gwiji wa zamani wa soka nchini Mexico, Jorge Campos, ameonesha kumzimikia zaidi kipa wa England, Jordan Pickford lakini ametahadharisha kuwa kipa huyo, ategemee upinzani mkubwa kutoka kwa kikosi cha Croatia, watakapokutana usiku wa leo, katika mechi ya nusu fainali ya pili.

Campos alisema kipa huyo amefanikiwa kuibeba England kwa kiasi kikubwa tangu michuano hii ianze, akichomoa michomo mingi, lakini kuna haja ya kujiandaa kisaikolojia kwa sababu Luca Modric, Ivan Rakitic na Mario Mandzuikic sio watu wa mchezo mchezo.

Pickford ambaye anakioiga katika kikosi cha Everton aliyojiunga nayo akitokea Sunderland, alisimama imara langoni katika mchezo wa robo fainali ya kwanza dhidi ya Sweden. Pia alifanikiwa kuwazuia Belgium kufanya madhara zaidi licha ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa mwisho wa makundi.

Kutokana na hilo, Campos ambaye aliichezea Mexico mechi 130, ikiwa ni pamoja na fainali za Kombe la Dunia, zilizofanyika huko Marekani mwaka 1994 na ile ya 1998 (Ufaransa), alisema kipa huyo mwenye umri wa miaka 24, amethibitisha thamani yake mpaka sasa.

"Unapozungumzia ubora, ni ngumu kuacha kumtaja Pickford, yuko vizuri sana japo kibarua kigumu kinamsubiri leo usiku. Kuna makipa wengine pia kama Thibaut Courtois na Hugo Lloris lakini huyu wa England yuko vizuri sana," alisema Campos