#WC2018: Kocha England aanza mbwembwe

Muktasari:

  • England ilianza mechi hizo kwa kuichapa Tunisia kwa mabao 2-1 kabla ya kuipopoa Panama kwa mabao 6-1, na kujihakikishia kutinga hatua ya 16 bora, lakini Southgate amesema hajaridhishwa na kiwango cha vijana wake.

Moscow, Russia. Katika kile kinachoonekana kama kuanza mbwembwe kutokana na ushindi katika mechi za makundi za Fainali za Kombe la Dunia, Kocha wa England, Gareth Southgate, amesema jambo linaloweza kuwafikirisha wengi.

England ilianza mechi hizo kwa kuichapa Tunisia kwa mabao 2-1 kabla ya kuipopoa Panama kwa mabao 6-1, na kujihakikishia kutinga hatua ya 16 bora, lakini Southgate amesema hajaridhishwa na kiwango cha vijana wake.

“Sote tumefurahishwa na matokeo lakini napenda kuweka wazi kuwa binafsi bado sijaridhishwa na kiwango chetu, sijaridhishwa na namna tulivyocheza na kupoteza nafasi tulipocheza na Tunisia na pia tulianza vibaya mchezo dhidi ya Panama ingawa baadaye tulishinda,” alisema Southgate.

Akifafanua zaidi Kocha huyo alisema kuwa anadhani ushindi wao wa kishindo kwa Panama ulitokana na udhaifu wa wapinzani wao lakini sio ubora wa kikosi chao.

England itacheza mchezo wa mwisho keshokutwa dhidi ya Ubelgiji mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa ili kumpata kinara wa kundi hilo.

Katika mechi ya juzi nahodha wa England, Harry Kane alifunga mabao matatu ‘hat trick’ ya kwanza tangu aanze kuitumikia timu hiyo, wakati John Stones alipiga mawili na yoso Jesse Lingard alifunga bao moja.