#WC2018: Mabango yaiponza Denmark

Muktasari:

  • Adhabu hiyo iliyoambatana na onyo kali ilitolewa jana, kutokana na mashabiki wa nchi hiyo kupeperusha mabango yaliyokua na ujumbe wa matusi wakati timu yao ya Taifa ikicheza mechi za Kombe la Dunia.

Zurich, Uswisi. Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA), limekipiga faini Chama cha soka Denmark (DFA), kiasi cha dola za Marekani 20,040, pamoja na kutishia kuiengua kwenye Kombe la Dunia.

Adhabu hiyo iliyoambatana na onyo kali ilitolewa jana, kutokana na mashabiki wa nchi hiyo kupeperusha mabango yaliyokua na ujumbe wa matusi wakati timu yao ya Taifa ikicheza mechi za Kombe la Dunia.

Mabango hayo na mengine yenye ujumbe wa kibaguzi yalipeperushwa katika mechi kati ya Denmark na Australia iliyoisha kwa sare ya bao 1-1 mchezo uliopigwa Alhamisi iliyopita mjini Samara.

Denmark, kwa sasa inashikilia nafasi ya pili kwenye kundi C na leo itakamilisha mechi ya mwisho dhidi ya kinara wa kundi hilo Ufaransa mchezo utakaopigwa Luzhniki stadium, jijini Moscow.

Kocha wa Denmark, Age Hareide, alikiambia kituo cha televisheni cha Denmark, TV2 kuwa ni vema mashabiki wa nchi hiyo kuachana na tabia hizo mbaya kwani zinaweza kuwagharimu.