#WC2018: Mambo manne yaliyojiri Kombe la Dunia 2018

Muktasari:

  • Kufanya vibaya kwa timu za Afrika, kuboronga kwa vigogo vinavyopewa nafasi ya kufanya vizuri, utata wa uamuzi wa mechi licha ya matumizi ya teknolojia ya video kusaidia waamuzi (VAR) na kutotamba kwa kundi kubwa la mastaa waliotegemewa kung’ara kwenye fainali hizo, vimeacha alama ya kukumbukwa katika raundi ya kwanza.

Dar es Salaam. Wakati mechi za raundi ya pili za Kombe la Dunia zilianza kutimua vumbi jana, mambo manne yamechomoza katika fainali hizo kwenye mzunguko wa kwanza uliomalizika jana kwa michezo iliyokutanisha timu za Japan dhidi ya Colombia na ile ya Senegal iliyovaana na Poland.

Kufanya vibaya kwa timu za Afrika, kuboronga kwa vigogo vinavyopewa nafasi ya kufanya vizuri, utata wa uamuzi wa mechi licha ya matumizi ya teknolojia ya video kusaidia waamuzi (VAR) na kutotamba kwa kundi kubwa la mastaa waliotegemewa kung’ara kwenye fainali hizo, vimeacha alama ya kukumbukwa katika raundi ya kwanza.

Afrika inayowakilishwa na timu tano katika fainali hizo, imejikuta ikikumbwa na majonzi katika raundi ya kwanza baada ya wawakilishi wake kupokea vipigo vya mfululizo ambavyo vinazipa kazi ngumu katika vita ya kuwania kupenya hatua ya 16 bora.

Kabla ya mechi ya jana Senegal dhidi ya Poland, wawakilishi wanne wa Afrika, Misri, Morocco, Nigeria na Tunisia walijikuta wakiambulia vipigo ambavyo sio tu vimewafanya kuwa kwenye nafasi mbaya katika msimamo wa makundi yao, pia vimezifanya timu hizo kukabiliwa na mtihani wa kupanda mlima mrefu kuingia raundi ya 16 bora.

Misri ilijikuta ikipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Uruguay kwa kulala bao 1-0 na kutupwa hadi nafasi ya tatu ya Kundi A kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Russia. Timu hiyo itafunga dimba kwa kuvaana na Saudi Arabia.

Morocco nayo ilichapwa bao 1-0 na Iran, kipigo kilichowatupa hadi mkiani mwa Kundi B kama ilivyokuwa kwa Nigeria ambayo ilijikuta ikishika mkia katika Kundi D baada ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Croatia.

Juzi usiku wawakilishi wengine wa Afrika, Tunisia walipoteza kwa mabao 2-1 mbele ya England na kuwafanya washike nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi G.

Wakati timu za Afrika zikitota kwenye fainali hizo, raundi ya kwanza imeonekana pia kuwa ngumu kwa baadhi ya nchi ambazo zimekuwa zikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka huu, baada ya kushindwa kufurukuta katika mechi za mwanzo.

Hispania ilikabwa koo na Ureno kwa kulazimishwa sare ya mabao 3-3 kabla ya Argentina kutoka sare ya bao 1-1 na Iceland.

Timu nyingine ambazo zimeanza vibaya licha ya kupewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa ni Brazil iliyotoka sare ya bao 1-1 na Uswisi wakati mabingwa watetezi, Ujerumani walichezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mexico.

Mbali na kuanza vibaya kwa baadhi ya timu zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa, pia hata baadhi ya mastaa ambao walitegemewa kutamba kwenye fainali hizo wameanza kwa kusuasua ukiwaondoa Cristiano Ronaldo wa Ureno, Diego Costa (Hispania), Harry Kane (England) na Romelu Lukaku (Ubelgiji) ambao walifunga mabao muhimu yaliyozibeba timu zao.

Lionel Messi, Mesut Ozil, Luis Suarez, Edinson Cavani, Neymar, Radamel Falcao, Kylian Mbape, Sergio Ramos na David De Gea wote walibanwa na nyota wasiokuwa na majina makubwa.

Jambo jingine la kushangaza katika raundi ya kwanza ni matukio ya utata yaliyotokana na waamuzi ambayo licha ya kuwepo kwa teknolojia ya video, bado yalishindwa kutolewa uamuzi sahihi jambo lililochangia kuibua malalamiko kutoka kwa timu mbalimbali.

Ufaransa ilikuwa timu ya kwanza kuonja raha ya teknolojia hiyo baada ya ‘kuzawadiwa’ penalti iliyowapa bao la kuongoza dhidi ya Australia baada ya Antoine Griezman kuangushwa ndani ya eneo la hatari ingawa awali mwamuzi alipeta faulo hiyo.