#WC2018: Mexico yaingia matatani, Fifa yaichunguza

Muktasari:

  • Mexico imeingia matatani baada ya mashabiki wa timu hiyo kumfanyia vitendo vinavyoashiria ushoga kipa wa Ujerumani Manuel Neuer.

Moscow, Russia. Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), limeanza uchunguzi na huenda hatua kali zikachukuliwa dhidi ya Mexico.

Mexico imeingia matatani baada ya mashabiki wa timu hiyo kumfanyia vitendo vinavyoashiria ushoga kipa wa Ujerumani Manuel Neuer.

Tukio hilo lilitokea katika mchezo wa Fainali za Kombe la Dunia ambao Mexico ilishinda bao 1-0 zinazoendelea nchini Russia.

Baadhi ya mashabiki walionyesha ishara ya vitendo vya ushoga kwa kipa huyo wakati akijiandaa kupiga mpira dakika ya 24 ya mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Luzhniki, Moscow.

Hata hivyo, Fifa haijatoa ufafanuzi wa adhabu inayotarajia kuchukua dhidi ya Mexico iliyoanza vyema fainali hizo baada ya kucheza kwa kiwango bora ilipovaana na Ujerumani.

“Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea hatuwezi kutoa taarifa haraka tunaendelea na mawasiliano,”ilisema taarifa ya Fifa.

Shirikisho la Soka Mexico limewahi kukumbwa na adhabu kutoka Fifa mara kwa mara kutokana na matukio ya mashabiki wake kujihusisha na ushoga viwanjani.

Maofisa wa shirisho hilo na wachezaji wa timu walijaribu kuwatuliza mashabiki kusitisha ishara zinazoashiria ushoga.

Kwa mujibu wa sheria mpya iliyoanza kutumika katika Fainali za Kombe la Dunia, Fifa ilitoa mwongozo kwa waamuzi kusimamisha mpira yanapojitokeza matukio yanayoashiria vitendo vya ushoga.

Sheria hiyo inasema kuwa endapo matukio ya aina hiyo yataendelea, mwamuzi ana mamlaka ya kuahirisha mchezo.