#WC2018: Mourinho: Kijana wangu De Gea ameniaibisha

Muktasari:

  • Uzembe wa kipa huyo ulisababisha Ureno kupata bao la pili

Moscow, Russia. David de Gea hatasahau usiku wa jana wakati wa mechi ya Hispania dhidi ya Ureno kwa makosa yake kuizawadia Ureno bao la pili katika mchezo uliomalizika kwa sare 3-3.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kocha wa Manchester United, Jose Mourinho alijaribu kumtetea kipa wake lakini amekiri kuwa amefanya makosa ya kizembe.

"Ni kijana wangu, imeniumiza mimi, lakini anajua amefanya kosa kubwa," Mourinho aliimbia RT.

"Ni makosa ambayo hajawahi kufanya akiwa kwetu, United – amecheza msimu huu kwa kiwango cha juu."

"Lakini inatokea kwa mchezaji bora.

"Jambo zuri la kuwa bora mechi ijayo atajionyesha zaidi, bila wasiwasi wote ataisaidia timu na kuiongoza kusonga mbele."

De Gea anategemea kurejea langoni Jumatano ijayo wakati wa mchezo dhidi ya Iran.