#WC2018: Ndugu wawili wavunja rekodi World Cup 2018

Muktasari:

  • Thorgan aliingia zikiwa zimebaki dakika saba katika mchezo ambao Ubelgiji ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Panama.

Moscow, Russia. Eden na Thorgan Hazard wameweka rekodi mpya ya kuwa wachezaji ndugu kuitumikia timu ya Taifa katika mchezo mmoja kwenye Fainali za Kombe la Dunia.

Thorgan aliingia zikiwa zimebaki dakika saba katika mchezo ambao Ubelgiji ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Panama.

Kitendo cha ndugu hao kucheza pamoja katika mchezo mmoja, kimeweka historia mpya katika fainali hizo zinazoendelea nchini Russia.

Nyota huyo wa klabu ya Borussia Monchengladbach, aliungana na kaka yake Eden anayeng’ara katika kikosi cha Chelsea.

Hii ni mara ya kwanza ndugu hao kucheza timu ya Taifa ya Ubelgiji tangu Emile na Jerome Mpenza walipocheza fainali hizo miaka 20 iliyopita nchini Ufaransa.

Pia Bobby na Jack Charlton waliwahi kuitumikia England katika fainali za mwaka 1966 ambapo timu hiyo ilitwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza na mwisho katika historia ya nchi hiyo.

Wachezaji wengine ndugu kutoka mataifa mbalimbali waliowahi kucheza fainali hizo ni Jerome (Ujerumani) na Kevin-Prince Boateng (Ghana).

Yaya, Kolo Toure (Ivory Coast), John, Mel Charles (Wales), Bobby, Jack Charlton (England) Francois, Andre Kana-Biyik (Cameroon), Erwin, Ronald Koeman (Uholanzi), Frank, Ronald de Boer (Uholanzi), Brian, Michael Laudrup (Denmark), Tore Andre, Jostein Flo (Norway), Niko na Robert Kovac (Croatia).

Francois na Andre Kana-Biyik ni Waafrika wa kwanza kucheza mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia katika mashindano yaliyochezwa Italia mwaka 1990 ambapo Cameroon ilikuwa timu ya kwanza kupata mafanikio hayo kutoka nchi za Afrika.