Mifano ya kukujenga katika uandishi wa kuleta ufumbuzi

Muktasari:

  • Tukamilishe ufafanuzi huu kwa kuangalia mifano mitatu ifuatayo. Tuanze na andishi la Felician Shija, mwandishi wa gazeti la Mwananchi.

Katika makala mbili zilizopita ambamo nimefafanua uandishi wa habari unaolenga kuleta ufumbuzi wa changamoto na matatizo ya mtu binafsi na jamii, tumeona kuwa uandishi wa habari ni uandishi rafiki.

Tukamilishe ufafanuzi huu kwa kuangalia mifano mitatu ifuatayo. Tuanze na andishi la Felician Shija, mwandishi wa gazeti la Mwananchi.

Felician anaandika (Mwananchi, 13 Novemba 2018): “Aliyebakwa, kutobolewa macho, asimulia anavyobeba familia.” Ni simulizi juu ya vitendo vya ukatili. Anayeandikwa, kama amesoma, anadondosha chozi kwa mara nyingine; afueni iliyoanza kumsogelea inanyauka.

Mwandishi anatumia uchungu na dhiki za aliyebakwa na kutobolewa macho, kujenga hoja ya kutafuta afueni. Ofisa Ustawi wa Jamii na Mkuu wa wilaya Kahama, hawana majibu. Ni huzuni juu ya huzuni. Lakini Felician hana ufumbuzi. Amebeba bango la majonzi.

Mwandishi hakwenda kwa nia ya kuleta ufumbuzi. Alitaka kuanika tu. Ameanika. Basi. Lakini angejibiidisha kujua haki za binadamu zinataka nini, sheria inasemaje, mabingwa katika eneo hilo wanasema nini juu ya ufumbuzi; angeandika kwa shabaha ya suluhisho.

Kama angechimba na kujua kama hali ya aina hiyo ilishawahi kuwepo Kahama, Mkoa wa Mwanza, kwingine Tanzania au nje ya nchi na jinsi iliyotanzuliwa; angeleta hoja ya ufumbuzi. Hakufanya hivyo. Ni fursa iliyopotea.

Twende mfano wa pili. Tanzania ina mbuga nyingi za wanyama zinazopakana na makazi ya watu. Kwa mfano, Manyara, Mbuga ya Hifadhi Arusha, Tarangire, Pori la Hifadhi ya Selous, Mikumi na Ngorongoro.

Wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa wanyamapori wanaharibu mashamba na mazao yao; wanaharibu makazi; wanaua wananchi. Hakika huu ni “mgogoro” wa siku nyingi kati ya binadamu na wanyamapori.

Mwandishi wa habari wa Tanzania, ambaye anaandika habari juu ya mgogoro huu, badala ya kubeba bango la vilio, anaweza kuchukua mfano wa Sri Lanka ambao tayari umeanza kuigwa, kueleza jinsi ya kuleta ufumbuzi katika maeneo yanayopakana na mbuga.

Kila mwaka nchini Sri Lanka tembo walikuwa wakiua watu wapatao 50. Wakati huohuo wananchi, kwa kutumia bunduki, sumu na hata umeme, walikuwa wakiua kati ya tembo 100 na 150. Idadi hii inaonyesha jinsi “mgogoro” ulivyokuwa mkubwa katika maeneo ambako watu walikwenda na ambako pia tembo walivinjari.

Kwa miaka mingi hatua zilichukuliwa ili kuzuia vifo vya watu na tembo, kama vile kuweka ugo wa kutenga eneo la watu na tembo; au kujaribu kuelekeza wanyama sehemu nyingine ili wasiingilie shughuli na maisha ya watu. Hazikufanikiwa.

Ndipo mwaka 2016 Asasi ya Kuhifadhi Wanyamapori ya Sri Lanka (SLWCS) ilibuni njia ya kupunguza makali au kuondoa kabisa mgogoro kati ya binadamu na wanyama. Ilianzisha basi la abiria katika eneo la Wasgamuwa; kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine kwa kupitia mbuga hiyo ya wanyama.

Mwaka jana ilifanyika sherehe ya kuadhimisha mwaka mmoja wa kuwa na EleFriendly Bus – Basi la Urafiki Kati ya Tembo na Binadamu. Basi lilinunuliwa kwa dola za Marekani zipatazo 35,000.

Leo hii basi linaendelea kusafirisha wanafunzi na watu wazima katika vijiji vya jimbo la kati ambavyo ni pamoja na Himbiliyakada, Iriyagasulpotha na Weheragalagama, ambako sasa binadamu wanapunga mikono na tembo wanapunga mikonga bila kuparurana.

Taarifa juu ya ugunduzi huu zinaeleza kuwa mwaka jana migogoro kati ya tembo na binadamu “imepungua kwa asilimia 80” tangu kuanzishwa kwa basi la urafiki. Katika miezi saba tu ya kwanza matukio ya “migongano” yalipungua kutoka 83 hadi 21.

Hii hapa faida nyingine ya ubunifu huu: Hakuna tena umbali wa kwenda kwa mguu; woga umeisha, watoto hawaogopi tena kwenda shule na hawachelewi; binadamu na wanyamapori (hasa tembo), wako salama.

Chukua mfano wa tatu. Tanzania ina upungufu wa nishati ya umeme. Sehemu kubwa haina umeme; kwingine bado unatumika umeme wa jenereta na kwingine kuna umeme unaotokana na mitambo inayoendeshwa kwa maji.

Lakini Tanzania ina utajiri mkubwa wa jua na upepo. Kwa kuwa tatizo linafahamika, mwandishi wa habari anayeandika juu ya ukosefu wa nishati anaweza kuanza kwa kutafuta ufumbuzi.

Hii ni kwa kuchunguza mazingira alipo, kuchimbua tafiti mbalimbali, kukutana na kuhojiana na wajuzi kabla na wakati wa kuandika habari; na kuja na andishi linalolenga kuleta ufumbuzi kwa njia nyepesi kabla ya kufikiria miradi mikubwa ya kuzalisha nishati hiyo.