Wednesday, September 13, 2017

Migogoro ya vyama vya siasa imalizwe kwa busara

 

Gazeti hili jana lilikuwa na habari kuhusu mvutano kati ya wabunge wa CUF kujitokeza ndani ya Bunge baada ya Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya kuwasilisha majina ya viongozi wapya wa chama hicho ndani ya chombo hicho.

Kutokana na hatua hiyo, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisoma taarifa ya Spika wa Bunge, Job Ndugai ikionyesha safu mpya ya uongozi wa wabunge wa chama hicho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma anakuwa mwenyekiti wa wabunge wa chama hicho bungeni, katibu ni Rukia Kassimu (Viti Maalumu) na mnadhimu wao ni Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia.

Kutangazwa kwa safu hiyo ya uongozi kuliibua maswali kutoka kwa wabunge wengine, na Ally Salehe aliomba mwongozo wa Spika akihoji imekuwaje safu hiyo ikatangazwa ilhali wabunge wa chama hicho wakiwa zaidi ya 40 walifanya uchaguzi wa viongozi wao.

Kwa mujibu wa Salehe, katika uchaguzi wao, nafasi ya uenyekiti iliyoachwa wazi na Riziki Ng’wali, ilichukuliwa na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea, na kuwa imekuwaje kunakuwa na safu mbili za uongozi wa chama kimoja.

Si nia yetu kuingilia mamlaka ya Bunge wala Spika, lakini tunadhani kwa hali ya mgogoro wa CUF ilipofikia kunahitajika utulivu zaidi katika kufanya maamuzi ili pande zote zione kutendewa haki na kusiwe na malalamiko yoyote.

Tunasema hivyo kwa kuzingatia kuwa hatua hiyo imekuja siku chache baada ya ofisi ya Bunge kukubali barua ya upande wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba ya kuwavua uanachama wabunge wanane na papo hapo kuwaapisha wengine wanane kama mbadala wao.

Kama alivyojibu Naibu Spika kuwa Spika amepokea taarifa ya viongozi hao kutoka kwa Sakaya, lakini hajapokea taarifa ya uchaguzi wa upande wa akina Ally Salehe juu ya uchaguzi huo, tunadhani kwa mgogoro ulivyo uamuzi wowote ungevuta subira na kujiridhisha zaidi na hata kukaa na pande zote mbili kwanza kabla ya kufanya lolote.

Tunajua kuwa katika mgogoro uliopo sasa, taasisi mbalimbali zimekuwa zikifanya uamuzi kwa kutumia rejea ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye anaitambua kambi ya Profesa Ibrahimu Lipumba.

Kutokana na msimamo wa ofisi hiyo ya msajili ndio maana hata taasisi nyingine kama Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na sasa Bunge vimekuwa vikitumia kigezo hicho cha ofisi ya msajili.

Tunajua kuwa kuna kesi kadhaa mahakamani kuhusu mgogoro huo bado hazijamalizika kwa hiyo tulidhani wakati mwingine ingekuwa vyema pande hizo mbili zingelazimishwa kupatana ili kumaliza mgogoro huo. Hakuna ubishi kuwa hatua iliyofikia chama hicho kinazidi kuvurugikiwa na hata Sakaya anakiri kuwa katika uchaguzi huo hawakuwashirikisha wenzao wa upande wa Maalim Seif.

Tunatoa wito kwa taasisi za umma, kuhakikisha kuwa zinakaa na pande hizo mbili zinazovutana ili kumaliza mgogoro huo, na kwa kufanya hivyo demokrasia yetu itashamiri na kuwa mfano wa kuigwa kutoka nchi nyingine za Afrika.

-->