Mikakati ya chakula kila kaya ienee kote

Muktasari:

  • Kuna aina nyingi za ukatili na unyanyasaji kijinsia. Upo wa kingono kwa wapenzi na wanandoa, kiuchumi na hata kiuongozi kwenye nyanja za siasa na utawala.

Ukatili na unyanyasaji wa kijinsia una sura nyingi na ni kati ya mambo yanayopigwa vita kitaifa na kimataifa kwa nia ya kuleta usawa na haki ya kijamii kwa makundi yote.

Kuna aina nyingi za ukatili na unyanyasaji kijinsia. Upo wa kingono kwa wapenzi na wanandoa, kiuchumi na hata kiuongozi kwenye nyanja za siasa na utawala.

Katika jamii nyingi nchini, wanaume husalia kuwa wenye sauti na maamuzi ya mwisho na ya kiimla katika umiliki na matumizi ya mali za familia, ikiwamo mazao yanayovunwa baada ya kazi kubwa inayofanywa na wanawake. Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza ni kati ya maeneo nchini yenye ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanaume kuamua hatima ya mazao yanayovunwa na familia.

Wanaume wengi wa wilaya hiyo huuza mavuno yote na kwenda mijini kuponda raha ikiwamo kuoa wake wengine bila kujali akiba ya chakula iliyosalia kwenye familia itakayowavusha hadi msimu mwingine wa mavuno.

Tabia hiyo inayochukuliwa na wenyeji kama asili au haki kwa wanaume ni miongoni mwa sababu ya familia nyingi wilayani humo kukumbwa na njaa kila mwaka licha ya eneo hilo kuwa na mavuno mengi kutokana na ardhi yenye rutuba na mvua ya kutosha. Ili kukabiliana na aina hiyo ya ukatili na unyanyasaji kijinsia, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi umeanza mikakati ya kudhibiti uuzwaji na matumizi holela ya mazao kwa kupita na kukagua akiba ya chakula kwa kila kaya.

Mkakati huo uliotangazwa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Eliud Mwaiteleke unalenga kuziepusha kaya hizo na ukosefu wa chakula. Mwaiteleke anaeleza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wanaume ambao kaya zao zitakutwa hazina akiba ya chakula.

Mbali na suala hilo, harakati za kupambana na ukatili wa kijinsia kwa njia mbalimbali zinaendelea kama anavyoeleza Mkurugenzi Mtendaji wa Kivulini, Yasin Ally.

Ally anasema wanaharakati 200 na viongozi 500 wa sungusungu wamenolewa kwa kujengewa uwezo wa kushiriki vita dhidi ya ukatili na unyanyasaji kijinsia katika wilaya hiyo.

Mkakati wa Misungwi siyo tu wa kupongezwa, bali unapaswa kuigwa na viongozi wa halmashauri zingine nchini ili pamoja na kuwapa wanawake na watoto sauti kwenye maamuzi ya matumizi ya mazao na mali nyingine ya familia, pia izihakikishie uhakika wa chakula.

Miongoni mwa mambo yanayolinda utu na sifa ya mtu, familia na jamii ni kujitegemea na kujitosheleza kwa mahitaji, hasa chakula. Pamoja na kuuza mazao kwa ajili ya fedha za starehe, matumizi mengine ya hovyo yanayopaswa kudhibitiwa kupitia sheria ndogo ni kutumia sehemu kubwa ya nafaka kutengeneza pombe za kienyeji zinazoambatana na sherehe na ngoma za jadi katika maeneo mbalimbali nchini.

Vita dhidi ya umaskini lazima ianzie kwenye uhakika wa chakula kwenye kaya zetu. Vita hivi vinapaswa kupiganiwa na kila mtu mwenye mapenzi mema. Marufuku ya matumizi holela ya mazao baada ya mavuno iwe moja ya mikakati ya kufanikisha vita dhidi ya umaskini.

Shughuli ya uzalishaji haiwezi kufanywa na watu wenye njaa. Lazima tuhakikishe watu wetu wanashiba, njia ya kufikia lengo hilo ni uhakika wa chakula kuanzia ngazi ya kaya.

Juhudi za Serikali za kuhimiza uzalishaji kufikia Taifa lenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025 kupitia maendeleo ya sekta ya viwanda haziwezi kufanikiwa bila kwanza kuwa na uhakika wa chakula.

Pamoja na kuhimiza uzalishaji wa mazao kutokana na Taifa letu kujaliwa ardhi yenye rutuba na mvua za kutosha, tuelekeze nguvu kwenye kuelimisha jamii kuhusu matumizi bora na sahihi ya mavuno. Wanaokaidi wadhibitiwe kama Misungwi ilivyoanza. 0757 708 277