Miongo minne ya vita vya Ukimwi Tanzania

Muktasari:

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya Ukimwi Duniani jana, kwa Tanzania ni miaka 33 tangu ugonjwa huo ugundulike hapa nchini,mwaka 1983.

Mwalimu Njuguna Muigai, anaingia darasani kufundisha kama ilivyo ada yake. Anawauliza wanafunzi wake leo ni tarehe ngapi? Wanamjibu, ni Desemba Mosi. Anakumbuka kuwa hiyo ni siku ya Ukimwi duniani lakini fikra zake hazijikiti katika siku hiyo pekee bali anakumbuka kuwa ameishi na Virusi vya Ukimwi kwa miaka 25 sasa.

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya Ukimwi Duniani jana, kwa Tanzania ni miaka 33 tangu ugonjwa huo ugundulike hapa nchini,mwaka 1983.

Katika kipindi hicho, Tanzania imepigana vita vya hali na mali kuondoa au kupunguza maambukizi, kupunguza vifo au kumaliza kabisa ugonjwa huo.

Kikubwa kinachotajwa na wadau wa afya ni mafanikio ya dawa za kufubaza makali ya Ukimwi(ARV) ambazo zimesaidia kupunguza maambukizi mapya na kuwapa Watanzania maisha yenye afya.

Ofisa Uraghibishaji na Mawasiliano wa Tume ya Taifa ya Kupambana na Ukimwi (Tacaids), Simon John anasema katika kipindi cha miaka 33 tangu Ukimwi ugundulike nchini, kiwango cha maambukizi kimepungua.

Kwa mfano, utafiti wa mwaka 2007/2008 unaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi kitaifa kilikuwa wastani wa asilimia 7.1. Lakini takwimu za sasa za wizara zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi kimefikia asilimia 5.3 kwa Tanzania Bara “Ni wazi kuwa baada ya miaka 33 tangu ugonjwa huu ugundulike, Watanzania kwa asilimia 99.9 wana uelewa kuhusu Ukimwi baada ya kutoa elimu. Wengi wamepunguza unyanyapaa na wamejua kujikinga,” anasema

Anasema licha ya maambukizi kupungua changamoto iliyopo ni watu kubadili tabia .

“Maambukizi yamepungua lakini kuna makundi bado yana maambukizi makubwa kwa mfano wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, wanaouza miili, wanaojidunga dawa za kulevya na wanaofanya kazi za mbali kwa mfano madereva wa magari makubwa,” anasema

John anasema pamoja na maambukizi lakini dawa za kufubaza makali ya Ukimwi zimesaidia kupunguza vifo na madhara yanayosababishwa na ugonjwa huo.

Kadhalika John anasema mafanikio mengine ni kuwepo kwa sekta za Ukimwi(intervention) katika kila kitengo kwa mfano shuleni, ofisi za serikali na kwenye mazingira hatarishi.

Anasema hata upimaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa na sasa hivi wengi hawaogopi kupima kama ilivyokuwa zamani.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani ya Mwili Meshack Shimwela anasema kutokana na takwimu zilizopo maambukizi yamepungua lakini bado watanzania wanatakiwa kubadili tabia.

“Kuna mambo kadhaa watanzania wakiyafanya, tunaweza kumaliza kabisa hili tatizo, kwa mfano ndoa za mitala, ngono zembe na kuachana na tabia zote hatarishi,” anasema

Anayataja mafanikio mengine kuwa ni matumizi ya ARV ambayo kwa kiasi kikubwa yamepunguza mambukizi mapya.

Anasema matumizi ya ARV kwa wajawazito ili kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto yamesaidia kwa asilimia 100 kupunguza maambukizi mapya.

Kingine anachokitaja Dk Shimwela kifanyike ili kupunguza maambukizi mapya ni kujenga tabia ya kupima. Anasema mtu anapopima inamsaidia kujikinga ili asiambukize wengine lakini aanze kutumia dawa.

Akizungumzia siku ya Ukimwi Duniani, Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa, Alvario Rodriguez anasema kwa miaka 33 tangu Ukimwi ugundulike amefurahishwa na maendelo makubwa kwa watu wanaoishi na VVU.

Anasema alifarijika sana potembelea kituo kimoja cha vijana wanaoishi na VVU ambao wamepewa mafunzo ya kujikimu kimaisha.

“Nilifurahi sana kuwaona hawa vijana wakizungumza kwa ufahari jinsi wanavyoweza kufanya biashara ndogo ndogo kama kuuza sabuni, karanga na zaidi hasa jinsi wanavyopata uimara kwa kutumia ARV,”anasema

Rodriguez anasema ni lazima Tanzania iwekeze katika masuala ya Ukimwi kwa upanda katika maeneo yote ya maisha.

Anasema ni vyema ikawepo miradi mikubwa ya Ukimwi katika maeneo yote yenye mahitaji na elimu itolewe zaidi.

Anaongeza kuwa UN kupitia mradi wake wa maendeleo wa 2016-2021 (UNDAP 11) unaendelea kutoa huduma za kuzuia maambukizi ya Ukimwi, kupima na kutoa dawa ili kuhakikisha kuwa Ukimwi unakuwa si tishio la kiafya ifikapo 2030.

Mkurugenzi Ufuatiliaji na Tathimini wa Tacaids, Dk Jerome Kamwela anasema mafanikio ni idadi ya vifo kupungua.

Dk Kamwela anasema idadi hiyo inapungua kutokana na upatikanaji wa huduma nzuri za Ukimwi.

“Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2011 vifo vilikuwa juu sana tofauti na mwaka jana na tuna imani tafiti ya mwaka huu wa 2016 hesabu itakuwa chini tena,” anasema Kimwela.

Kamwela anaongeza kuwa takwimu hizo zinazingatia vigezo vya kimataifa kwa kuwa ripoti zote zinawasilishwa katika Umoja wa Mataifa inayotoa ripoti kila Desemba 1 duniani kuhusu Ukimwi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Tacaids, kiwango cha maambukizi kinapimwa kwa tafiti inayofanyika kila baada ya miaka minne.

Kwa mfano mwaka 2003, matokeo yalionyesha kuwa maambukizi yalikuwa ni kwa asilimia 7 na mwaka 2011/12 utafiti unaonyesha kuwa maambukizi yalishuka na kufikia asilimia 5.3.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, anayemaliza muda wake, Ban Ki Moon katika ujumbe wake wa Siku ya Ukimwi Duniani amesema mafanikio yameonekana katika vita vya Ukimwi kwani katika miaka mitano iliyopita idadi ya watu wanaopata dawa imeongezeka na kufikia 18 milioni dunia nzima.

“Kama tutawekeza inavyotakiwa dunia itapata mafanikio na kufikia malengo ya kuwapa matibabu ya Ukimwi watu milioni 30 ifikapo 2030,” anasema

Anasema mafanikio hayo ni pamoja na kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto inawafikia watu kwa asilimia 75.

Ki Moon anasema bado kuna changamoto kwa watoto wa kike ambao wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi hasa katika nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Anasema maambukizi mapya yameongezeka kwa watu wanaojidunga dawa za kulevua na wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.

“Maambukizi yanaongezeka Mashariki mwa bara la Ulaya, asia ya kati kutokana na unyanyasaji na sheria kali,” anasema

Ki Moon anasema changamoto nyingine inayopaswa kufanyiwa kazi ni watu wenye kipato cha chini ambao wanakosa huduma bora na unyanyapaa ambao unasababisha maambukizi mapya.

Lakini Ki Moon anasisitiza kuwa bado wanawake na watoto wanaathirika zaidi na Ukimwi.