Mkakati huu wa gesi utaokoa mazingira

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba anasema Serikali hivi sasa ipo katika majaribio ya gesi ya kupima mithili ya matumizi ya umeme wa Luku yaani mteja kuwa na uwezo kununua kadri ya uwezo wake.

Kwamba utafika wakati mwananchi atakuwa na uwezo wa kwenda dukani na kununua gesi akiwa na Sh800 ni habari njema na yenye matumaini makubwa kwa wengi wetu na zaidi wale wa kipato cha chini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba anasema Serikali hivi sasa ipo katika majaribio ya gesi ya kupima mithili ya matumizi ya umeme wa Luku yaani mteja kuwa na uwezo kununua kadri ya uwezo wake.

Katika matumizi hayo, Waziri Makamba alisema mwananchi atanunua mtungi wa gesi ambao utakuwa na kifaa maalumu ambacho kitamuwezesha kutumia gesi kadri atakavyokuwa akilipia na kiwango cha fedha alicholipia kikiisha gesi inazima.

Tunazo sababu za kusema kwamba hiyo ni habari njema, kwanza ni gharama. Kwa watumiaji wa nishati hiyo wanaelewa jinsi wanavyolazimika kuwa na kati ya Sh48,000 au zaidi ya Sh50,000 ili kupata mtungi mmoja wa gesi wa kilo 15.

Ukubwa huo wa gharama sambamba na ule bei ya umeme, umewafanya wananchi wengi kutegemea zaidi kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia, nishati ambazo licha ya kuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira, kama Waziri Makamba alivyobainisha, ufanisi wake ni mdogo.

Mafanikio ya hatua hiyo yanaweza kuokoa majanga mengi ya asili yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi. Takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 90 ya Watanzania wanategemea mkaa kama chanzo chao cha kwanza cha nishati na hilo linadhihirishwa na misururu ya malori, baiskeli na pikipiki zilizojazana katika barabara zetu zikisomba nishati hiyo kuelekea kwenye miji kila kukicha.

Tukumbuke kwamba mti mmoja hadi kukomaa, unaweza kuchukua zaidi ya muongo mmoja lakini matumizi yake unapokatwa na kutumika kama nishati hauchukui hata wiki mbili. Kasi hiyo ndiyo inayofanya maeneo mengi kugeuka makame, yasiyokuwa na rutuba na kusababisha kukosekana kwa mvua, malisho ya mifugo na ustawi wa mazao.

Mara kadhaa tumewahi kushauri kwamba njia sahihi ya kupambana na uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa ni kutafuta njia mbadala za nishati hiyo badala ya kutunga sheria nyingi na kali.

Mei mwaka jana, gazeti hili lilimkariri Charles Meshack, Mkurugenzi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG) akisema sababu ya wananchi kukimbilia kwenye mkaa ni kutokana na ughali wa nishati nyingine au ulazima wa kuipata kwa mkupuo na Mtanzania wa kipato cha chini anayepata fedha kwa kubangaiza hawezi kumudu.

“Kwa mfano umeme au gesi inabidi anunue kwa mkupuo, iwe ankara au mtungi. Sasa tunajua Watanzania wengi uwezo huo hawana ndio maana wanakimbilia kwenye mkaa ambako anaweza kununua kibaba kimoja au viwili na kutumia kwa siku,” alisema na kusisitiza kwamba kuzuia mkaa hakutadhibiti ukataji miti kwa sababu Watanzania hawachomi mkaa kwa bahati mbaya au kwa kuwa ni wahalifu.

Tunashukuru kwamba sasa Serikali inaelekea kuipatia suluhisho la kudumu changamoto ya uharibifu wa mazingira kwa kuwa bei ya gesi sasa itakuwa nafuu zaidi ya mkaa. Itakaposambaa na kuenea, inaweza sasa kuja na sheria ambayo itamfanya mtu kufikiria mara mbilimbili adhabu anayoweza kukabiliana nayo akipatikana na hatia ya kukata miti kwa ajili ya nishati au kutumia gesi ambayo sio tu kwamba bei yake ni rahisi, bali pia haina usumbufu.