Mpango wa bajeti mpya uje na vyanzo vipya vya mapato

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango. Anapatikana kwa 0685214949/0744782880.

Muktasari:

  • Bajeti hii ina vyanzo vingi vya mapato mfano ni Kodi ya Mapato ambayo inajumuisha mapato yatokanayo na ajira faida kwa kampuni.
  • Vilevile, inajumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa bidhaa na huduma. Ushuru wa forodha unaingia kwenye kundi hili pia. Chanzo hiki kinatarajiwa kutoa zaidi ya Sh15 trilioni sawa na asilimia 51.14 ya makusanyo yote.

Kwa tafsiri rahisi, bajeti ni mapato na matumizi. Kwa sasa tunafuata masharti na vigezo vya bajeti ya mwaka 2016/2017 ambayo kaulimbiu yake ni kuongeza uzalishaji viwandani ili kupanua fursa za ajira.

Bajeti hii ina vyanzo vingi vya mapato mfano ni Kodi ya Mapato ambayo inajumuisha mapato yatokanayo na ajira faida kwa kampuni.

Vilevile, inajumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa bidhaa na huduma. Ushuru wa forodha unaingia kwenye kundi hili pia. Chanzo hiki kinatarajiwa kutoa zaidi ya Sh15 trilioni sawa na asilimia 51.14 ya makusanyo yote.

Kuna mapato yasiyo ya kodi yanayojumuisha faini, tozo, mauzo ya zabuni na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hapa kuna zaidi ya Sh3.4 trilioni sawa na asilimia 11.37 ya makusanyo yote.

Misaada na mikopo yenye masharti nafuu ni chanzo kingine kinachotarajia kuchangia Sh3.6 trilioni sawa na asilimia 12.19. Mikopo ya ndani na nje ilete Sh7.5 trilioni sawa na asilimia 25.31.

Makundi haya manne ndiyo yanayounda makusanyo ya Serikali kwa mwaka 2016/2017. Kwenye Bunge la Bajeti litakalokutana Aprili, tutafahamu chanzo kipi kati ya hivi kimefanya vizuri zaidi.

Kwa kutumia takwimu za mwaka 2014/2015, 2015/2016 na nusu ya mwaka 2016/2017 makusanyo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa mwezi yamepongezeka.

Makusanyo hayo yamepanda kutoka Sh904 bilioni kwa mwezi mwaka 2014/2015 hadi Sh1.02 trilioni mwaka 2015/2016 sawa na ongezeko la asilimia 11.37. ongezeko hili limeshuhudiwa zaidi baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani.

Aidha wastani wa makusanyo kwa mwezi yameonekana kupanda kutoka wastani wa trilioni 1.02 mwaka 2015/2016 hadi trilioni 1.183 kwa miezi minne ya mwanzo ya mwaka 2016/2017 sawa na ongezeko la asilimia 13.78.

Baada ya ufanisi huo ulioonekana mwanzo, Serikali ya awamu ya tano inatakiwa kutafuta vyanzo vipya vya mapato au kuboresha vilivyopo ili kuwa rafiki kwa wananchi.

Mara nyingi Rais John Magufuli amekuwa akijitambulisha kuwa kiongozi wa masikini na wanyonge. Kwamba, umasikini wa Watanzania umesababishwa na baadhi ya viongozi waliopewa mamlaka ya kuwatumikia kuyatumia kwa maslahi yao.

Changamoto inayoikabili Tanzania ni baadhi ya watumishi kufanya kazi kwa mazoea utaratibu ambao Serikali ya awamu hii imedhamiria kuuondoa ingawa juhudi zaidi zinahitajika.

Watumishi wengi wa umma hawapendi kushughulisha vichwa vyao, ndiyo maana kila mwaka vyanzo vya mapato ya Serikali vinakuwa ni vilevile. Wanachofanya ni ‘kukopi na kupesti’ kisha kuongeza asilimia za ongezeko na kubadili mwaka tu.

Mfano kama leseni ya biashara mwaka 2016/2017 ni Shilingi laki moja kwa mwaka huu basi mwakani Sh120,000 au faini ya makosa ya barabarani itaongezwa kutoka Sh30,000 iliyopo mpaka Sh50,000. Hii hufanywa bila kutoa sababu za kufanya hivyo. Hawataki kusumbua vichwa.

Haya ndiyo mazoea ninayoyazungumzia. Tanzania ni nchi kubwa na ina rasilimali nyingi ambazo zinaweza kuwekewa utaratibu wa kodi na kupunguza ‘mzigo’ kwa mwananchi wa kawaida.

Hali ya mwaka huu wa fedha inaonyesha uwezo wa mwananchi kununua umepungua, mfumoko wa bei ukiwa miongoni mwa sababu.

Takwimu zinaonesha kuwa Novemba mwaka jana mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 4.5 lakini Desemba ukpanda mpaka asilimia 4.8 na Januari, 2017 ulikuwa asilimia 5. Kwa miezi mitatu mfululizo mfumuko wa bei unapanda.

Moja ya sababu zinazochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni kupanda kwa bei za vyakula. Hii inatokana na ubovu wa miundombinu ya usafirishaji na wingi wa kodi unaopunguza kiwango cha mazao sokoni.

Kwa mujibu ripoti ya Benki ya Dunia umaskini duniani umepungua kutoka asilimia 34 mwaka 2007 hadi asilimia 28 mwaka 2012. Mpango na Bajeti wa mwaka 2017/2018 lazima uje na jibu la kupunguza zaidi umasikini huu. Si vinginevyo.

Serikali imeelekeza zaidi ya asilimia 40 ya bajeti yake kwenye miradi ya maendeleo. Kwa kiasi kikubwa imedhibiti matumizi yasiyo na tija kwa kwa kupunguza au kuzuia posho na safari zisizo na matokeo chanya kwa wananchi. Aidha mianya mingi ya ‘upigaji’ imezibwa.

Sababu hizi zinatajwa kupunguza mzunguko wa fedha kwenye mzunguko. Mwaka 2014/2015 bajeti ya miradi ya maendeleo ilikuwa asilimia 25 na matumizi ya kawaida asilimia 75.

Kupungua kwa uwezo wa kununua, mfumuko wa bei, kupungua kwa mzunguko wa fedha kwenye uchumi ni mambo ya msingi kuzingatiwa wakati wa uandaaji wa mpango na bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Sasa ni muda wa wataalamu kuumiza vichwa ili kuja na vyanzo vipya vya mapato.

Mwandishi ni Mtakwimu na Ofisa Mipango. Anapatikana kwa 0685214949/0744782880.