Monday, March 20, 2017

Msafara wavamiwa Kijiji cha Arash

 

By Mussa Juma, Mwananchi mjuma@mwananchi.co.tz

Arusha. Mwenyekiti wa kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amemuagiza Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Charles Mkumbo kuwakamata wote waliohusika uvamizi wa msafara wa wajumbe wa kamati hiyo.

 Msafara wa wajumbe wa hiyo ulivamiwa na makundi ya wafugaji wakiwa na silaha za jadi juzi jioni.

Wananchi hao wanapinga kuwekwa alama maeneo yanayohitajika kuhifadhiwa katika ikolojia ya Serengeti.

Kamati hiyo iliyoanza kazi ya kuweka alama kwenye pori tengefu la Loliondo, ilikumbana na mkasa huo katika Kijiji cha Arash kinachopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Kulikuwa na makundi kama matatu hivi, yaliyofunga barabara na kutushambulia, mmoja alifungua mlango wa gari langu,” amesema Gambo.

Kiongozi wa timu ya wataalamu waliokuwa kwenye msafara huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori, Martin Loiboki amesema makundi ya wananchi yalirusha mawe na kuvunja vioo vya gari lake ambalo lilikuwa mbele katika msafara huo.

 

-->