Msafiri: Nateseka sina fedha, nahitaji kufanyiwa upasuaji

Muktasari:

  • Nyama ni miongoni mwa vitoweo vinavyopendwa na wengi, hivyo kwenye mlo wa familia, sherehe hata kwenye biashara hupatiwa nafasi kubwa.

Wakati unakula chakula ukipendacho cha aina yoyote ile, kumbuka kuna watu hushindwa kula kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ya masharti waliyopatiwa na madaktari kutokana na maradhi mbalimbali waliyonayo.

Nyama ni miongoni mwa vitoweo vinavyopendwa na wengi, hivyo kwenye mlo wa familia, sherehe hata kwenye biashara hupatiwa nafasi kubwa.

Justina Raphael maarufu ‘ Msafiri’ anasema hulazimika kutoka nje ama kwenda chumbani huku akitiririkwa machozi anaposhuhudia watu wa familia yake wakila nyama na vyakula vingine alivyokatazwa kuvitumia na daktari.

“Naumwa, ninateseka kwa maumivu, lakini pia suala la kukatazwa kula nyama linanifanya nikose raha hasa ninaposhuhudia wenzangu wakiila wakati mimi nimeambiwa nile zaidi mboga za majani zisizowekwa chumvi,” anasema Msafiri.

Mwonekano wa Msafiri ambaye ni mkulima, mkazi wa Kilando, Nkasi, unaonyesha wazi kuwa ana maumivu makali hata tembea yake ni ya kujivuta na tumbo lake limevimba.

Unapomtazama usoni, amenyong’onyea na kila wakati anakunja ndita kwa kuugulia maumivu. Lakini licha ya hali hiyo, Msafiri analazimika kutembea maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kuomba msaada wa fedha za matibabu.

Anasema anajutia mtindo wake wa maisha aliyokuwa akiishi kuwa ni chanzo cha maradhi yake.

Asimulia historia ya maisha yake

Msafiri anasema kabla ya kuanza kuugua, alikuwa akinywa sana pombe. “Nimeapa hadi naingia kaburini, sirudii tena kunywa pombe.”

Msafiri ambaye ni baba wa watoto watano, anasema hana uwezo wa kugharamia matibabu ya maradhi yanayomsumbua.

Nini kinamsumbua Msafiri?

Mgonjwa huyo anasema yupo jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na mpwa wake anayemtaja jina Ignus Kwisaki, ili atibiwe.

Anasema mpwawe huyo ameshampeleka kwenye hospitali kadhaa kwa matibabu lakini bado hajapona.

“Kote nilikoenda kutibiwa, nimeambiwa ninamatatizo kwenye ini, natakiwa kufanyia upasuaji,” anasema Msafiri.

Msafari anasema baadhi ya hospitali alizokwisha tibiwa ni pamoja na ya Zakhem Mbagala, Temeke, na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikolazwa kwa nyakati tofauti.

“Nimeambiwa nina tatizo kwenye ini, hapa nchini hakuna tiba isipokuwa nje ya nchi, lakini sina fedha za kwenda huko, nimebaki nateseka kwa maumivu,” anasema Msafiri.

Anaomba msaada wa fedha za kugharamia matibabu hayo kwa mtu, taasisi na watu binafsi kumsaidia aweze kwenda nje kutibiwa.

Licha ya kukosa matibabu halisi ya ugonjwa huo, Msafiri anasema anajitahidi kuzingatia masharti aliyopewa na madaktari, hasa ya kuepuka kula nyama na vyakula vilivyotiwa chumvi.

“Tumbo langu linajaa maji na kunisababishia maumivu hadi kwenye kipofu cha mkojo, sina furaha ya maisha kwa sababu siwezi kula vyakula vizuri lakini pia mke wangu naishia kumtazama tu, kwa kuwa siwezi hata kushiriki tendo la ndoa,” anasema Msafiri.

“Naamini naishi kwa sababu Mungu amependa niendelee kuishi, nilipokuwa nimelazwa nilishuhudia watu wenye miili yenye afya kuliko mimi wakifa, ndiyo maana nahangaika kutafuta msaada wa matibabu huenda Mungu anamakusudi na mimi,” anasema Msafiri.

Madaktari wanasemaje?

Tabibu wa dawa za asili, Dk Samson Kibona wa Antipa Herbal Clinic anasema ugonjwa aina ya hepatitis B, C, na D ni chanzo cha ugonjwa wa cirrhosis, unaosababishwa na hepatitis B.

Anasema mtu anayeugua maradhi hayo huwa na dalili kadhaa ikiwamo ya kuwa na rangi ya njano kwenye macho.

Dk Kibona ambaye amesomea tiba ya binadamu na kuamua kujikita kutengeneza dawa za asili na lishe, anasema mtu anayekabiliwa na cirrhosis hupatwa na maumivu makali ya tumbo.

Anasema hali hiyo ya maumivu na mambo mengine hutokana kuongezeka ukubwa wa ini baadaye tumbo hujaa maji yanayotakiwa yatolewe mara kwa mara,

“Ingawa hakuna tiba ya upasuaji hapa nchini, anaweza kuendelea kuishi kama atazingatia masharti anayopewa na madaktari, pamoja na kubadili mfumo wa maisha na akitumia dawa za kupunguza sumu mwilini zinazoweza kumsaidia kupata nafuu,” anasema Dk Kibona.

Daktari bingwa Khamis Bakari ambaye ni mtaalamu wa Tiba na Uchunguzi kwa kutumia mionzi ya Nyuklia (Nuclear medicine), katika moja ya andiko lake kuhusu ugonjwa wa ini, anasema ni miongoni mwa maradhi 12 duniani yanayoongoza kwa kusababisha vifo.

Anasema maradhi ya cirrhosis husababishwa na unywaji wa pombe kupindukia.

na ugonjwa wa hepatitis B, C, na ugonjwa wa fatty liver disease.

Anasema kwa wagonjwa wengine wasiotumia pombe chanzo chake bado hakijajulikana.

Je ni vipimo gani hutumika?

Dk Bakari anasema vipimo vya uchunguzi vinavyofanywa ni pamoja na cha damu (Complete blood count).

Anasema mgonjwa huangaliwa kiwango chake cha damu (anaemia), kupungua kwa chembechembe bapa za damu au platelets (thrombocytopenia).

Pia mgonjwa hupimwa kama amepungukiwa chembechembe nyeupe za damu (leukopenia) na chembechembe aina ya neutrophils (neutropenia) na kama amepungukiwa madini aina ya sodium.

Dk Bakari ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, anasema kuna kipimo kingine anachotakiwa mgonjwa afanyiwe ambacho ni cha ufanyaji kazi wa ini na kuangalia kama albumin zimepungua na majibu yakija chanya, basi mgonjwa huyo atakuwa anaugua cirrhosis.

Hata hivyo, anasema kuna mambo ambayo wataalamu wa afya hushauri kama hatua mojawapo ya kuzuia uhabirifu zaidi wa ini.

Nayo ni pamoja na kuzuia utumiaji wa dawa aina ya paracetamol na pombe.

Anasema ili kutibu hepatitis B na C, mgonjwa hupatiwa dawa za kuongeza damu. Na kama atabainika anaupungufu mkubwa atatakiwa kuongezewa damu kwa njia ya dripu ili kuzuia madhara ya cirrhosis yasije kutokea na pia kumzuia asitumie chumvi kwenye chakula.

Anasema mgonjwa pia anapaswa kupunguza kula vyakula vyenye protini nyingi, kutumia dawa za antibiotiki ambazo daktari atashauri, kutumia dawa aina ya lactulose ili kupunguza madhara ya heptic encephalopathy kwa kupunguza kiwango cha amonia mwilini zinazoweza kumsaidia mgonjwa kupata choo laini.

Je maradhi ya hepatitis B yanaweza kusababisha saratani?

Dk Bakari anasema maradhi hayo yanaweza kusababisha saratani ya ini ambayo nayo husababisha vifo vingi hivi sasa duniani.

Pia husababisha kusagika kwa mifupa ya kwenye mikono na miguu inayomsababishia mgonjwa maumivu makali na wakati mwingine miguu hukakamaa na kuvimba.

Anasema wengi wanaougua maradhi hayo hukumbwa na hali ya kuchanganyikiwa, kupungua umakini, kusahau haraka, kuwa na hasira, kupungua uwezo wa kujiamulia mambo na hawezi kujali muonekano wake.

“Lakini pia mgonjwa anaweza kupata matatizo ya kulala, hii inatokana na kuongezeka kwa ammonia ndani ya damu inayosababisha madhara kwenye ubongo. Madhara ya cirrhosis yakishindwa kudhibitiwa au kama ini litashindwa kufanya kazi kabisa, mgonjwa atahitajika kupandikizwa ini lingine,” anasema daktari huyo.