Tuesday, April 18, 2017

Msako wa vyeti feki usiwe na upendeleo

By Mwananchi

Rais John Magufuli wakati akizindua majengo mapya kwa ajili ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Jumamosi iliyopita alisema kuna watumishi wapatao elfu tisa serikalini wenye vyeti feki.

Ingawa orodha hiyo haijawasilishwa rasmi mezani kwake, imefahamika baada ya kazi ya miezi kadhaa ya kuhakiki wafanyakazi serikalini, utendaji wao ikilinganishwa na elimu yao, majina yao katika vyeti vya sekondari na vyuo.

Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani iliamua kuhakiki vyeti vya watumishi wake ili kujiridhisha na taaluma yao maana katika miaka ya hivi karibuni wapo waliofeli katika ngazi fulani ya elimu lakini baadaye wanakuja kuonekana na vyeti vya elimu ambayo hawakuifanyia kazi.

Pia, miaka ya hivi karibuni baadhi ya watu wamethubutu hata kughushi vyeti vya shahada ya kwanza, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu ndio hao wanaitwa Dokta fulani wakati hana elimu ya kiwango hicho.

Hivyo, tunapongeza juhudi za Rais Magufuli kupambana na ‘ufisadi wa elimu’ na tunaamini atadhibiti sawa na alivyoshughulikia sakata la watumishi hewa waliobainika kufikia 56,000.

Mpango wa kuhakiki vyeti kwa wafanyakazi wa umma ni mzuri kwa kuwa unalenga kuondoa wale wasio na elimu hiyo katika kuhudumia wananchi.

Wapo wanaojenga majengo bila ya kufuata kanuni za ujenzi kutokana na kutokuwa na elimu sahihi na hivyo kusababisha baadhi kuanguka au maeneo ya makazi kutokuwa na mpangilio.

Tumeshuhudia pia maeneo kama hospitalini, watu wasio na sifa wamediriki hata kujiwekea ofisi na kutoa huduma kwa muda mrefu, bila ya hata kujulikana. Kama wasio na sifa walidiriki kuingia ofisini na kufanya majukumu ya kitabibu, hali ikoje kwa wale walioghushi vyeti? Jibu ni kwamba hali ni mbaya.

Kwa hiyo, mpango huo utasaidia kurekebisha utumishi katika sekta ya umma.

Tunaamini pia uhakiki utasaidia kupata ukweli na kuhitimisha mjadala wa muda mrefu kuhusu baadhi ya wateule wa Rais hasa mkuu wa mkoa mmoja.

Inadaiwa mteule huyo alifeli elimu ya sekondari lakini anaonekana na jina jingine ambalo licha ya kelele za kumtaka aeleze kiwango chake ili kuwanyamazisha wapinzani wake, hadi sasa yuko kimya.

Wapo waliokwenda hadi kijijini kwake, baadhi ya wasanii wametunga nyimbo kumdhihaki, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wamezungumzia elimu ya mteule huyo kwenye vikao vya Bunge, wakitaka Rais atengue uteuzi wake, huku Meya wa Ubungo, Boniface Jacob akiliwasilisha suala hilo mbele ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kwa hiyo tunatarajia ripoti hiyo itahusisha suala hilo na hivyo kumpa Rais fursa ya kufanya uamuzi kwa haki na kufunga mjadala huo.

Tunaamini kuwa mteule huyo ni mmoja tu, lakini wapo watu wengi wa aina hiyo ambao ripoti hiyo inatakiwa iwaanike bila ya kupendelea au kuwaficha, ili wananchi wajenge imani kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imepania kusafisha utumishi wa umma na kuboresha utendaji bila ya kuonea wala kupendelea watu fulani, au wa kada fulani au kundi la watu fulani.

Kama Serikali imewekeza rasilimali watu na fedha kupita kila ofisi kuhakiki vyeti, tunaamini kazi hiyo itafanyika kwa weledi bila ya kuacha shaka kwa mtu hata mmoja.

-->