Mtoto anavyoweza kuathirika kiakili, kimwili kutokana na kaya maskini

Muktasari:

Jumamosi iliyopita ilikuwa ni Siku ya Idadi ya Watu Duniani. Ni wakati ambao dunia ilipata wasaa wa kujadili juu ya njia bora za binadamu kuongezeka na kuleta ustawi endelevu na ulio bora kwa watoto.

Suala la idadi ya watu lina uhusiano na njia za uzazi wa mpango, mfumo unaotumika ili kuiwezesha kaya au familia ya baba na mama kuwa na idadi ya watoto ambao itamudu kuwalea vizuri kwa chakula, mavazi, malazi, huduma za afya na elimu.

Kaya ambayo inashindwa kutekeleza hayo, watoto hushindwa kuwa kwenye ustawi ulio bora na hata maendeleo yao kielimu huwa duni. Matokeo yake ni kuendelea kuzalisha kizazi masikini.

Ustawi wa jamii unaanzia kwenye familia. Nchi yoyote inayokuwa na kaya nyingi masikini hata uchumi wake huzorota. Ndiyo maana wataalamu wa afya wanasisitiza nguvu ya kipato kizuri ianzie kwenye ngazi ya familia.

Uchunguzi unaonyesha kuwa familia nyingi nchini ni masikini hivyo hushindwa kuwatunza kikamilifu watoto ili wawe na afya njema.

Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani yamefanyika ikiwa ni wiki chache baada ya kuadhimishwa Siku ya Mtoto wa Afrika.

Chimbuko la maadhimisho mtoto wa Afrika lilitokana na mauaji ya kikatili ya watoto 15,000 waliokuwa wanapinga vitendo vya ubaguzi katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini, Juni mwaka 1976.

Shirika la Kimataifa la World Vision ni miongoni mwa taasisi inayoendesha harakati za kulinda na kutetea ustawi wa watoto.

Katika kufanikisha hilo, World Vision limekuwa likiendesha miradi kadhaa ya kusaidia familia kujikimu kiuchumi ili kujenga mazingira bora ya makuzi kwa watoto.

Shirika hilo limekuwa likiendesha miradi ya maendeleo ili kuwasaidia watoto 24,625 katika wilaya za Simanjiro, mkoani Manyara na Mwanga (Kilimanjaro) chini ya mradi wa Maendeleo wa Ruvu-Remiti (ADP).

Idadi ya watoto hao inalengwa na mradi huo wa ADP ulipoanza utekelezaji mwaka 1998 kwenye kata za Ruvu-Remiti na Loiboiti, katika Wilaya ya Simanjiro na za Mwanga za Kirya, Lembeni na Mgagao.

Mratibu wa ADP, Pendael Lukumay anasema wana miradi 16 yenye lengo la kuinua kaya 34,992 zinazojumuisha wanawake 17, 715 na wanaume 17,475.

Katika mpango huo miradi ya maendeleo kama kilimo na ufugaji huendeshwa kwa kuwezesha kaya.

Lukumay anataja miradi mingine kuwa ni ya kupunguza magonjwa kama malaria, kuhara na homa ya mapafu ambayo ni tatizo kwa maendeleo ya watoto kiafya, kielimu na makuzi.

“Tumefanikiwa kujenga zahanati saba na nyumba za madaktari sita kwenye eneo la miradi. Hii inarahisisha watoto walio chini ya miaka mitano kupata huduma za chanjo kwa urahisi na matibabu wanapougua,” anasema Lukumay.

Anasema mradi wake umewezesha pia elimu kwa jamii kwa kufundisha wahudumu wa afya wa wapatao 32 na waganga waandamizi kwa kuwajengea uwezo ili wahudumie watoto na jamii.

Lukumay anasema pia elimu ya afya imekuwa ikitolewa kwa akina mama wakati wa ujauzito, kujifungua na malezi bora ili kuwahakikishia malezi bora ya watoto wanapozaliwa na makuzi yao.

“Wakati wa utekelezaji wa miradi yetu tunatumia mbinu inayofahamika kwa jina la Sauti ya Uma ama “Citizen Voice and Action (CVA),” anasema.

Anafafanua kuwa kaya hupewa nafasi ya kuibua miradi kulingana na mahitaji ambayo ni halisi na hii inasaidia kuichukulia miradi kuwa sehemu muhimu ya maisha yao na rahisi kuitekeleza.

Lukumay anasema kutoka mwaka 1998 miradi iliyolengwa kwa Simanjiro na Mwanga, asilimia 95 ya malengo yamefikiwa na bado inaendelea na kugharimu Dola 3 milioni za Marekani karibu sawa na Sh6 bilioni.

Gasper Mola ambaye ni mwezeshaji kwenye mradi huo wa ADP Ruvu-Remiti anasema kwa upande wa elimu, mradi umejenga vyumba vinne vya madarasa na nyumba za walimu katika Kata ya Loibosoit.

Katika kudhihirisha ADP unampigania mtoto na kumkomboa kutokana na changamoto zilizokuwa zinawakabili na zinazowakabili, anasema wameziwezesha kaya kuunda Vicoba.

Mwenyekiti wa kikundi cha Vicoba cha Dira, Emmanuel Elifuraha anasema kupitia taasisi hiyo kaya zimefaidika kwa kukuza watoto kiafya na kielimu.

Mwenyekiti wa kikundi cha cha Vicoba cha Inuka, Auleria Lyamuya anasema yeye ana watoto 10 na kama siyo mradi huo wangekuwa katika hali mbaya kiafya na kielimu.

 

Malezi hatari kwa watoto

Mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Naberera Kata ya Naberera, Elizabeth Mollel akisoma risala kwa Katibu Tarafa wa Naberera, Mussa Mgogose anasema wamekuwa wakipata huduma za afya kikamilifu hali inayowawezesha kuwa na uhakika wa kuhudhuria vipindi darasani.

Anasema mtoto anapougua mara kwa mara, hawezi kuhudhuria darasani na hata maendeleo yanakuwa duni na hata kiakili anadumaa.

Naberera anasema ni vyema Serikali isimamie z utoaji haki, usawa, na maendeleo ya watoto nchini.

Anasema familia zilizokosa usaidizi wa uwezeshi kama unaotolewa na World Vision zimekuwa katika hatari ya kukosa amani kutokana na umasikini. Matokeo yake watoto wanalazimishwa kuacha masomo na kwenda kufanya kazi, zikiwamo hatarishi kiafya na makuzi.

Isitoshe, anasema umasikini kwenye familia ni chanzo cha watoto wa mitaani, uhalifu na hata baba na mama kuachana.

“Ndugu mgeni rasmi, watoto wakishakimbilia mitaani kwa kukosa haki, hujiingiza kwenye vitendo vya utumiaji wa dawa za kulevya, pombe, ukahaba na uporaji. Tusipoangalia watoto na haki zao, tutajenga jamii yenye maadili potofu na kuchochea ongezeko la maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU),” anasema Mollel.

 

Haki za watoto

Mollel anasema kimsingi mtoto anatakiwa apate haki za msingi kabla na baada ya kuzaliwa kama haki ya kulindwa na kuzua vitendo viovu wanavyotendewa, haki ya kuendelezwa kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii.

Anasema pia watoto wana haki ya kushiriki katika kutoa mawazo kwenye masuala yanayohusu maendeleo yao na jamii na haki ya kutokubaguliwa hasa katika masuala ya elimu.

Mambo hayo anasema ni lazima yazingatie usawa wa jinsia na upatikanaji haki sawa kwa watoto na pia uhimizaji wa mahitaji maalumu ya watoto wenye shida kama wenye ulemavu.

Mwanafunzi huyo anasema changamoto iliyopo wilayani Simanjiro ni wananchi kutoona umuhimu wa kuwajibika kuhamasisha na kuchukua hatua ya kuacha kuendeleleza mila na desturi potofu zinazohatarisha maisha na ustawi wa mtoto.

Mila na desturi mbaya wilayani Simanjiro na baadhi ya sehemu nyingine za Tanzania zimechangia watoto hasa wa kike kutopelekwa shule na kuolewa wakiwa na umri mdogo na kuendeleza mfumo dume kwenye jamii.

Tabia hiyo anaielezea kuwa imesababisha athari nyingi za kiafya kwa wasichana kama kubeba mimba wakati hawajafikia umri unaopendekezwa kitaalamu na kubeba majukummu mazito ya kifamilia kabla hawajakomaa kiakili na bila elimu.

Hali hii inaelezewa kuwa ni sawa na unyanyasaji na ndoa nyingi za utotoni huvunjika na kuwaacha wakiwa hawana mwelekeo mzuri kimaisha. Isitoshe wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa ya kiakili na kimwili.

“Tunashauri jamii kupiga vita mila potofu na mila nzuri ziimarishwe na kuendelezwa kushiriki katika malezi ya pamoja na utoaji wa huduma kwa wototo wanaoishi katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya Ukimwi,” anasema.

 

Kauli mbiu kwa watoto

Mollel anataja kauli mbiu ya mwaka huu kuwa “Ubakaji na ulawiti kwa watoto vinaepukika chukua hatua ya kumlinda mtoto.”

Kupitia kauli hii, anasema watoto nchini wanaiomba Serikali kuzuia na kupiga vita kuozwa wakiwa wadogo na pia kuchukua hatua kali kwa wanaondelea kuwaozesha na kuwapa mimba watoto wa kike.

Wale wote wenye dhamana ya kusimamia sheria za kuwalinda watoto watimize wajibu wao kwa kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake.

Katibu Tarafa wa Tarafa Naberera, Mussa Mgogose anasema Serikali katika eneo hilo kwa ujumla imekuwa ikihakikisha kuwa watoto wanapewa haki zao pasipokujali jinsi wala ulemavu.

Mgogose anasema Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha huduma za hospitali na katika kuwalinda watoto imekuwa ikitoa bila malipo huduma kwa mama mjamzito hadi kujifungua na kutoa matibabu bure hadi mtoto anapofikia miaka mitano. “Ni jukumu letu sote kama wazazi na walimu kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi katika kuondoa au kupunguza kero zinazosababisha unyanyasi,” anasema Mgogose.


Maoni au maswali tuma [email protected] au 0713247889