MAONI: Muswada huu upitiwe kuimarisha demokrasia

Novemba 16, Serikali iliwasilisha bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa ambao tayari wadau mbalimbali wameanza kuupitia kwa kina na kutoa maoni yao.

Wanaoupinga wanasema hawajui waliouwasilisha wanalenga nini maana unadaiwa kupunguza uhuru wa wanachama kuamua mambo yao na nani awe kiongozi au yupi asigombee.

Hiyo ndiyo sababu wadau wakuu wa muswada huo ambao ni vyama vya siasa walikutana mwishoni mwa wiki iliyopita kujadili na kupaza sauti yao kuupinga kwa nguvu.

Wanadai muswada huo unakwenda kuongeza uchungu kwa miswada mingine ambayo licha ya wadau kutoa maoni yao, hayakuchukuliwa badala yake ilipitishwa kuwa sheria kana kwamba wao si sehemu ya jamii hii inayolalamika.

Miongoni mwa miswada iliyopitishwa licha ya wadau kukosoa na kulalamika ni wa vyombo vya habari; takwimu na makosa ya mtandaoni. Madhara yake kila mmoja anayaona. Kwamba mtu akipiga picha kuonyesha jengo fulani la umma lina nyufa kwa sababu ya kujengwa chini ya kiwango, badala ya kupongezwa kwa kutoa taarifa, mhusika anakamatwa na kufunguliwa kesi ya uchochezi.

Kadhalika, mtu akitumia takwimu za Serikali kuonyesha dosari pengine za mwelekeo wa uchumi ulivyoripotiwa tofauti na vyombo vya Serikali au matokeo ya utafiti binafsi uliofanywa wahusika anakamatwa na kushtakiwa. Katikati ya kilio kikubwa cha wadau kuhusu namna miswada hiyo ilivyopitishwa na kuwa sheria, safari hii umewasilishwa muswada ambao ukipitishwa, mfumo wa vyama vingi ulioanzishwa kwa mabadiliko ya Katiba mwaka 1992 kutokana na Waraka wa Serikali Na 1, utakuwa umebaki katika maandishi na siyo katika uhalisia wake.

Chini ya mfumo wa vyama vingi, sheria zinaruhusu watu kuanzisha vyama vya siasa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa. Hii ina maana watu wako huru kujiunga na chama chochote cha siasa chenye itikadi na sera wanazotaka na kutoa maoni yao, hata kama wengine hawayataki, ilimradi hawavunji sheria.

Sote tunafahamu kwamba chama cha siasa ni kikundi au kundi la watu wenye itikadi fulani ambao wana katiba, kanuni na miongozo yao. Katiba ndiyo huongoza kila kundi; hufafanua muundo wa chama, namna ya kupata viongozi pamoja na maofisa wengine wawapendao ili kutimiza malengo ya kisiasa. Kanuni huandaliwa kuelekeza utaratibu wa kuwapata viongozi husika.

Lakini katika namna isiyo sahihi na ya kushangaza, muswada huu wa mabadiliko ya sheria unapunguza uhuru na kidemokrasia, unapokonya utashi wa wanachama na kumpa mamlaka msajili wa vyama vya siasa anayepaswa kuwa mlezi.

Huyo ndiye muswada huo unataka awe na mamlaka ya kumvua uanachama mtu yeyote kwenye chama cha siasa na kupata taarifa za chama kutoka kwa mwanachama yeyote.

Hebu tujiulize, kwa nini msajili aingilie wakati katiba za vyama zimeweka taratibu? Kwa nini msajili anapewa mamlaka ya kupata taarifa na kutoa kibali cha mafunzo kwa viongozi wa chama?

Kwa nini msajili aache kuwasiliana na uongozi halali wa kuchaguliwa badala yake ategemee taarifa zozote za chama kutoka kwa mwanachama yeyote?

Hakuna shaka kuwa kuna mambo mazuri, lakini ni vyema mambo ambayo yanalalamikiwa yafanyiwe kazi.