Friday, November 4, 2016

Mwaka mmoja, abiria hatujui mwelekeo wa dereva

 

By Julius Mtatiro

Ni mwaka mmoja sasa unatimia tangu Rais John Pombe Magufuli aapishwe kuwa mkuu wa nchi. Rais JPM aliahidi mambo mengi kabla hajachaguliwa na hayo ndiyo kipimo cha mwaka huu mmoja.

 Kwa mtizamo wangu wa moja kwa moja, Rais amefanikiwa katika masuala machache kuliko ilivyotarajiwa na hata hayo ambayo amefanikiwa, bado hayajawa na athari kwa wananchi wa kawaida. Kwa kifupi nitajadili mambo matano muhimu ambayo hajafanikiwa sana; uchumi, huduma za jamii, uhusiano wa kimataifa, demokrasia na mambo ya jumla.

Kwa upande wa uchumi, sitaki kuwekewa maneno mdomoni, yatupasa turejee kauli za wabunge wa CCM ambazo zimetoka na kurekodiwa pale Dodoma wiki hii. Wabunge wa chama hicho wanaeleza kuwa nchi haina mwelekeo wowote kiuchumi, huenda ni siri ya Rais Magufuli peke yake.

Watanzania wanaona sarakasi nyingi kwenye uchumi, wakati JPM anaingia madarakani alikusanya makusanyo ya ziada na kuanza kufikia Sh1.5 trilioni kwa mwezi. Mwaka mmoja baadaye makusanyo hayo yameshuka na Serikali inajitutumua kuyaishi kwa njia ya ndoto.

Bandari inafanya vibaya, sekta ya utalii pia. Ujenzi wa viwanda na miundombinu ya kurahisisha uwapo wa viwanda bado haujaanza. Nimeusikiliza mpango wa mwaka mmoja wa Serikali uliosomwa na Waziri wa Fedha pale bungeni Dodoma, sijaona mahali popote pale hatua za kivitendo ambazo zitaonekana, nimesikia hadithi zile zile za miongo kadhaa iliyopita ‘makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma’.

Tutakuwa kwenye hatari kubwa ikiwa wananchi wa kawaida hawajui mwelekeo wa uchumi wao ili wamsaidie Rais kushiriki kwenye uchumi wa awamu yake.

Jambo la pili muhimu kuligusia ni huduma za kijamii, hapa kwa makusudi naomba nijumuishe elimu, afya, maji, miundombinu, kilimo n.k. Elimu bure tuliyotangaziwa kwa shule za msingi ilianza kutolewa Januari, Serikali haijafanya lolote kuwaokoa walimu, ambao wako kwenye hali mbaya katika kuendesha shule zinazotoa elimu bure lakini Serikali haijatangaza mipango yake katika kuondoa matatizo ya walimu ambayo sasa yamepitiliza. Sote tumezisikia takwimu za utoaji wa mikopo ya elimu ya juu mwezi uliopita, serikali ya JPM imeanguka kwa zaidi ya asilimia 50 katika utoaji wa mikopo. Sote tulitarajia kuwa JPM atatembea kwenye maneno yake wakati wa kampeni, kwamba “hakuna mtoto wa masikini ambaye atashindwa kusoma elimu ya juu ukizingatia kuwa fedha wanazopewa ni za mikopo”, kinachotokea sasa hivi sote ni mashahidi!

Katika sekta ya afya ni hivi majuzi tu madaktari, Wizara, Serikali na MSD vimekuwa vikivutana juu ya hali mbaya ya madawa nchini – hakuna mipango ya wazi iliyotangazwa na serikali kukabiliana na tatizo la ukosefu wa madawa, hasa vijijini.

Je, unataka tuzungumzie kilimo, takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, japokuwa kinachoshangaza ni kuwa kilimo chenyewe kinachangia asilimia 4 tu kwenye pato la taifa! Kilimo cha Tanzania kwa awamu zote zilizopita kimetegemea zaidi uwepo wa mvua, JPM alisema awamu yake itakiinua kilimo kwa nguvu, lakini cha kusikitisha, anategemea mvua pia, kama wenzake, kwamba tunatumia mbinu zilezile kwa kutegemea mvua ileile ambayo haipo miaka yote, ili tupate matokeo tofauti!

Haiwezekani, kama kuna eneo ambalo JPM na wenzake wanahitaji kufanya “homuweki” ni kwenye kilimo, kama hawatakuja na mikakati imara, asilimia 70 ya Watanzania watawekwa kwenye mashaka ya kudumu kwa miaka minne inayokuja na hadi JPM atakapomaliza kipindi chake.

Katika uhusiano wa kimataifa, hatujafanya vizuri pia. Naupenda sana uamuzi wa Rais wa kutosafiri nje hovyovyo. Mtangulizi wake, JK, alisafiri nje mno. Akiitiwa tuzo Afrika Kusini, na taasisi binafsi, anachoma mafuta na wasaidizi kwenda kupokea tuzo hiyo. Akipewa mwaliko wa kuhudhuria maadhimisho yoyote na nchi fulani, anakwenda, “it was too much to burden this poor nation” (ilipitiliza kuweka mizigo yote hiyo kwa taifa hili).

Lakini, lazima tukubaliane kimsingi kwamba Rais wa nchi anapaswa kusafiri kuhudhuria mikutano muhimu ambayo itaifanya nchi yake isiwekwe nje ya utangamano wa kidunia. Kwamba wakuu wa Umoja wa Afrika ulioasisiwa na kina Nyerere, Kwame Nkrumah na wengineo, wanakutana Addis Ababa, wewe rais huendi, kwamba wakuu wa nchi za Sadc wanakutana ili kuikabidhi nchi yako uenyekiti wa Sadc na “akchuali” mwenyekiti mwenyewe ni wewe na huendi! Sasa hapa si unaikomoa nchi yako na uchumi wako? Fursa ya kukutana ana kwa ana na wakuu wa nchi 15 ambazo unafanya nazo biashara muhimu si ndiyo wakati wa kufanya “lobbying” ili kujenga mustakabali wa utalii, kilimo cha umwagiliaji, ujenzi wa viwanda, utumiaji wa bandari yako na mambo mengineyo? Ni lini basi Rais anapata muda wa kushughulika na “prime issues” (masuala makuu) ya nchi yake kama si kwa kutumia majukwaa kama hayo? Nukta yangu hapa ni kuwa, tumeshaona nia yetu nzuri ya Rais kuzuia watumishi wa umma wasisafiri hovyo hovyo, lakini nachokiona ni kwamba, yeye JPM lazima ahudhurie masuala muhimu na makubwa na ambayo yanawakutanisha wakuu wengine wa nchi za dunia. Mbunge “Sugu” anasema “take a jet brother” (panda ndege kaka!)

Mwaka mmoja huu wa JPM amefeli kwenye eneo la ujenzi wa demokrasia nchini, na najua hiyo inafanywa kimakusudi. Rais alikuta wananchi wanapata fursa ya kufuatilia bunge lao, chombo chenye mamlaka na ukuu wa wananchi, akafutilia mbali utaratibu wa kuoneshwa bunge “live”, sababu ya kwanza ambayo haikuwa ya kweli kutoka serikalini ikiwa kubana matumizi. Vyombo binafsi vikataka kurusha kwa gharama zao vikakataliwa. Rais akaenda mbali zaidi, akaanza kudhibiti shughuli za vyama vya siasa, kwa nguvu kubwa, akazuia mikutano ya hadhara ya kisiasa na akajipa haki hiyo yeye peke yake. Hatua zote hizi kwa uchache ni kinyume kabisa na katiba ya Tanzania na sheria zake. Na ni kinyume kabisa na masuala ya haki za kiraia na dhana ya kukuza uwazi nchini. Hivi sasa Serikali ya JPM imehamishia nguvu katika kudhibiti vyombo vya habari na majukwaa ya kupashana habari, ambapo muswada wa Huduma za Habari unaopiganiwa na serikali yake, kwa kiasi kikubwa unashadidiwa ili kuvidhibiti vyombo vya habari. Unayo mambo machache sana yanayoweza kutajwa kama “nia njema” kwa sekta ya habari. Hali ni mbaya. Mwaka mmoja sasa demokrasi iko kitanzini na sijui ikishaminywa nini kitaletwa kama mbadala wake, maana nafasi ya demokrasia haiwezi kuzibwa na “kimabavu”.

Yapo mambo mengine kadhaa muhimu ambayo Serikali ya JPM haijayashughulikia katika kipindi cha mwaka wake mmoja. Ajira na viwango vya mishahara. Tatizo la ajira limezidi kupanuka, nguvu kazi kubwa sana inarudi mitaani na haina cha kufanya, hata ile inayohitaji kujiajiri, mitaji kwa ajili ya hatua hiyo haipo. Mwaka huu mmoja huku hakuna mkakati wa wazi wa kupambana na ukosefu wa ajira. Watu walioko kazini, serikalini na sekta binafsi, hali zao si nzuri pia. Wale wa sekta binafsi wanaondolewa kazini kwa kasi kwa sababu ya kuyumba kwa uchumi, wale walioko serikalini mishahara yao inatia aibu na ongezeko lililotangazwa na serikali mwaka huu (kwenye mishahara) ni kichekesho. Hiyo inatoa njia moja tu, serikali ya JPM ina kazi ya ziada kuwekeza katika uboreshaji wa rasilimali watu hapa nchini. Watu ndiyo maisha ya taifa na ukishindwa kuwajengea mazingira shirikishi na yanayotia hamasa unaua taifa lako wewe mwenyewe.

Wasomaji wangu wataniwia radhi sana, kwamba sijaongelea masuala mazuri yaliyofanywa na serikali ya sasa. Sijafanya hivyo kwa sababu mengi ya hayo yanayoitwa mazuri, hayajaonyesha dalili ya kuleta tija kwa maisha ya Watanzania, wakati huo ukifika nitayasema masuala hayo na kuonyesha tiza zake. Mathalani, ningeliweza kupongeza sana hatua ya kubana matumizi, lakini ni ikiwa tu hatua hiyo ingelikuwa imesababisha fedha zilizookolewa zikaongeze uzito kwenye mikopo ya wanafuzi wa elimu ya juu, au kwenye kujenga miundombinu ya umwagiliaji ili wakulima waanze kuwa na kilimo cha uhakika.

Lakini ikiwa tumebana matumizi, halafu fedha zilizookolewa hazijulikani ziko wapi, wakulima bado wanataabika, wanafunzi wanakosa mikopo, wafanyakazi wana hali mbaya – sipanui mdomo wangu katika hatua ya sasa hadi mazuri ya JPM yaanze kuwa na athari chanya kwa maisha ya wananchi. Namtaki rais wetu kila la heri katika mwaka mmoja ujao.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii na Kisiasa, Mtafiti na Mwanasheria Simu; +255787536759/ Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com/ Tovuti; juliusmtatiro.com.

-->