Friday, November 4, 2016

Mwaka mmoja wa misingi sita

 

By Hassan Abbas, Maelezo

Kufanya tathmini ya mwaka mmoja kwa kiongozi wa aina ya Rais John Magufuli, ni kazi ngumu na rahisi. Ni ngumu kwa sababu yapo mengi aliyofanya, unagusa lipi? Ni rahisi kwa sababu eneo lolote utakalolichagua, utakuwa na mengi ya kuandika.

Ni kwa minajili hiyo, leo ningeweza kuangalia nidhamu aliyoileta Rais katika utumishi wa umma; au ningeweza kuchagua kueleza dira yake katika mapambano dhidi ya rushwa; au kumueleza Rais Magufuli na misingi ya uchumi wa nchi yetu.

Kwa takribani wiki nzima nimekuwa nikisoma, kusikia na kuona Watanzania na watalaamu mbalimbali wakimweleza Rais katika maeneo mengi.

Nikiwa naelekea kutimiza siku 100 tangu nipewe wadhifa nilionao katika kuitumikia Serikali, nimeona nitazame zaidi misingi ya mageuzi ambayo Rais anapitia katika kuivusha nchi ndani ya siku 366 akiwa madarakani.

Kwa maoni yangu, kuishi katika misingi ni kama kile mtaalamu wa masuala ya mageuzi wa nchini Malaysia, Profesa Idris Jalla anachokiita “transformative leadership (uongozi wa kimageuzi)”.

Katika dhana hiyo, Profesa Jalla anataja siri kuu sita au misingi ya uongozi wa kimageuzi. Tusafiri na Rais Magufuli katika siku zake hizi 366 kwa jicho la misingi hiyo sita aliyoianisha Profesa Jalla ili kuona ameishi vipi katika hayo.

 

Malengo magumu

Profesa Jalla anasema siri moja kubwa ya viongozi wa kimageuzi ni wale wanaojiwekea malengo makubwa na magumu kiasi kwamba kila mtu husema haiwezekani. Yeye huyaita malengo haya kuwa ni “olympic targets (malengo ya olimpiki)”.

Katika mwaka huu mmoja, namuona Rais Magufuli akiwa mtu aliyeishi katika msingi huo. Iwe ahadi za kwenye ilani ya uchaguzi, ahadi zake binafsi wakati wa kampeni, au akiwa madarakani, Rais amesikika akiweka malengo fulani magumu kwa kiwango cha wengi kusema atashindwa.

Nitatoa mfano wa ununuzi wa ndege. Siku Rais aliposema ifikapo Septemba, Serikali ingeleta ndege mpya mbili ikiwa ni safari ya kuelekea kulifufua Shirika la Ndege Tanzania, wengi walisikika wakinong’ona kuwa hilo lilikuwa lengo gumu na lisingetokea. Imetokea.

Siku alipolihutubia Bunge na kuahidi kuwashughulikia viongozi wazembe, wala rushwa, wasiotimiza majukumu yao vyema na wenye changamoto mbalimbali za kiutumishi kwa staili ya “kutumbua majipu”, wapo waliosema ni maneno tu. Ametenda.

 

Vipaumbele

Profesa Jalla na hata viongozi wenye uzoefu na masuala ya mageuzi kama aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, wanakubaliana kuwa siri nyingine au msingi mwingine muhimu wa kiongozi wa kimageuzi, ni kuweka vipaumbele.

Akieleza uzoefu wake katika eneo hili, Blair anasema katika kitabu “The Art and Science of Delivery (Mbinu na Sayansi ya Utekelezaji),” kwamba: “As a leader everyone you meet is looking to convince you that their issues should be at the top of your to-do list. But if everything’s a priority, then nothing gets done. You need to pick a small number of priorities and maintain a laser-like focus on delivering them.”

Yaani “kama kiongozi kila mmoja unayekutana naye anajaribu kukushawishi kuwa mambo yao ndiyo yanatakiwa kupewa kipaumbele, na hivyo hakuna kinachofanyika. Unahitaji kuchagua idadi ndogo ya vipaumbele na kuendelea kuweka macho yako yote katika kuyatekeleza”.

Wanaomfuatilia Rais Magufuli tangu akiwa Naibu Waziri, Waziri na sasa Rais watakubaliana nami kuwa ni mtu ambaye ana maono yenye vipaumbele vilivyo wazi katika visheni (maono) yake ya uongozi.

Wakati katika uchumi ameshatangaza na kasi kubwa inaendelea, kipaumbele cha uchumi wa viwanda katika mwaka mmoja ameweka wazi kuinua pato la nchi kwa kuelekea kujitegemea na kujenga utumishi au watumishi waliotukuka katika kuwahudumia wananchi.

 

Utekelezaji

Profesa Jalla anasema kama kuna msingi mwingine muhimu unaomtofautisha kiongozi wa kimageuzi na viongozi wengine, ni umakini wake katika utekelezaji wa vipaumbele vyake na ufuatiliaji.

Namuona Rais Magufuli kuwa kiongozi anayeishi na kutembea vyema na falsafa au msingi huu. Ni mwaka mmoja uliokuwa wa mambo mengi, lakini tumemuona Rais akitoa maagizo na kuyafuatilia, akiahidi na kutenda na wakati fulani akifika mwenyewe eneo la tukio kuongeza nguvu yake katika kuhakikisha utekelezaji.

Ndani ya siku chache tu tangu alipoapishwa, tulimuona akifika kwa kushtukiza ofisi za Wizara ya Fedha na kujionea hali na ari ya utendaji. Ziara yake ile na namna ilivyoleta mageuzi ya fikra kwa watumishi wa umma juu ya umuhimu wa kuwahi ofisini na kuwatumikia watu inaweza kuwa mada nyingine.

Haikutosha, licha ya kutoa maagizo bado mara kadhaa ama yeye au viongozi wake wengine, wamekuwa wakifika katika maeneo hayo. Katika mwaka mmoja huu Rais alikwenda Benki Kuu, bandarini, kwenye ujenzi wa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kwenye ujenzi wa nyumba za wakazi wa Magomeni Kota.

Katika ziara zake hizo ambazo mtu angeweza kuona ni jambo la kawaida tu, sote tumeanza kuona faida zake. Ziara na ufuatiliaji wa karibu wa Rais umejenga dhana ya uwajibikaji mkubwa sana kwa watendaji na watumishi wa umma na imewapa wananchi nguvu ya kuhoji pale huduma inapokuwa si ya kuridhisha.

Ukiniuliza katika hili, nitakwamba watendaji na watumishi wengi wa umma kwa sasa kila mtu anaishi akijiuliza swali moja muhimu katika utendaji wake; “ninafuatilia (kazi na maagizo) au hadi nifuatiliwe?” Na kila mmoja anajua likitokea hilo la pili, yuko matatizoni kiasi gani!

 

Timu ya ushindi

Kuwa na watendaji watakaokusaidia kazi ni kitu muhimu sana katika utekelezaji wa malengo na vipaumbele. Profesa Jalla anafafanua hili kwa kuzungumzia zaidi haja ya kiongozi wa kimageuzi kutengeneza kile anachokiita “winning coalition (timu ya ushindi)” yenye watu wanaoweza kuendana na falsafa yake.

Katika mwaka mmoja huu tumemuona Rais Magufuli akitimiza hili kwa kutumia muda wake mwingi kutengeneza timu ya ushindi. Na hakika tumeona na bahati nzuri katika teuzi zake amechukua muda wa kutosha wa kufikiria, kufuatilia na kutafakari.

Amefanya uamuzi mkubwa na utakaokumbukwa sana wa kuwaamini vijana katika nafasi kubwa za uongozi na utumishi wa umma. Leo, kuna vijana wengi katika ngazi ya uwaziri, naibu, makatibu wakuu, wakurugenzi, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa wilaya na halmashauri na hata miongoni mwa wasaidizi na washauri wake.

 

Mawasiliano ya kimkakati

Alipokuwa anazungumzia siri muhimu ya kiongozi wa kimageuzi katika kujenga timu ya ushindi, Profesa Idriss Jala pia anataja jambo moja muhimu na adhimu akisema viongozi wa kimageuzi uheshimu mawasiliano ya kimkakati kama nyenzo ya kuwatumikia watu.

Tunapozungumzia dhana hii, hatuishii tu kusisitiza viongozi wasikike, au wawaambie wananchi wanachokifanya, sera, mikakati, mafanikio na changamoto. La hasha. Mawasiliano ya kimkakati ni pamoja na wananchi nao kutoa mrejesho.

Nashukuru kuwa mimi ni mmoja wa vijana walioaminiwa na Serikali ya Rais Magufuli katika kusaidia uzoefu wangu mdogo kwa kuifanya Serikali kuwa na mawasiliano ya kimkakati.

Huu umekuwa mwaka wa Rais Magufuli kuhakikisha mawasiliano serikalini, kwa maana ya Serikali inafanya nini na inataka kuwafanyia nini wananchi, ni vitu vinavyoenziwa.

 

Kumtegemea Mungu

Katika nadharia yake hii kuhusu viongozi wa kimageuzi, Profesa Jalla anataja kitu ambacho kinaweza kuwagusa wengi au kuwashangaza wengi. Profesa anaamini kuwa katika siri za kufanikiwa kiuongozi msingi wa mwisho ni kumtegemea Mungu.

Hoja ya Profesa imejikita katika dhana kubwa mbili; mosi, sisi kama wanadamu kuna mambo mengi hatuna udhibiti nayo hivyo kumuomba na kumtegemea aliye na mamlaka hayo ni jambo muhimu. Pili, anaamini kuwa kiongozi anayemtumaini Mungu hataogopa kufanya mageuzi yenye manufaa kwa wengi na pia hatafanya mambo yasiyo na manufaa kwa watu wake.

Sisi sote ni mashahidi juu ya imani ya Rais Magufuli kwa Mwenyezi Mungu. Amekuwa akiwaomba Watanzania wamuombee. Pia, ameshirikiana na waumini wa madhehebu na dini zote.

 

Mwandishi wa makala haya ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali. Anapatikana kwa simu: 0713 584467.

-->