Mwalimu unavyoweza kuheshimiwa na wanafunzi bila kuwachapa

Muktasari:

Ungetegemea walimu waliojifunza namna ya kuwaadabisha wanafunzi wangekuwa na mtazamo tofauti. Lakini ukizungumza nao, unashangaa mawazo ni yale yale.

Imejengeka dhana katika jamii kuwa huwezi ‘kumnyoosha’ mtoto kitabia bila bakora.

Malezi na bakora vinachukuliwa kuwa sawa na pete na chanda. Huwezi kuvitenganisha viwili hivyo na ukaeleweka kirahisi.

Ungetegemea walimu waliojifunza namna ya kuwaadabisha wanafunzi wangekuwa na mtazamo tofauti. Lakini ukizungumza nao, unashangaa mawazo ni yale yale.

Walimu wetu hawaoni uwezekano wowote wa sauti zao kusikika na wanafunzi bila matumizi ya mabavu. Nafahamu wakati mwingine tatizo linaweza kuwa ukorofi wa wanafunzi wetu.

Kwa mfano, wapo wanafunzi wakorofi kiasi cha kuweza kujibizana na hata kumtukana mwalimu bila haya. Aidha, wapo wanafunzi wenye uthubutu wa kurushiana makonde na mwalimu.

Pamoja na ukweli kuwa wanafunzi wenye tabia hizi mara nyingi huwa na historia ya kuzoea mabavu kwenye familia zao, bado hatulazimiki kuwajibu kwa kutumia mabavu waliyoyazoea.

Majuzi nilikuwa na mafunzo na walimu wa sekondari kuwasaidia kutumia mbinu mbadala za kujenga nidhamu ya wanafunzi. Joto la mjadala lilikuwa kali.

Mwishoni mwa mafunzo hayo walimu wale walikubali kimsingi kuwa inawezekana kujenga nidhamu ya mwanafunzi bila bakora.Ningependa kutumia makala haya kukushirikisha baadhi ya masuala tuliyoyazungumza siku hiyo nikiamini, bila shaka yanaweza kukusaidia kukufundisha kitu kuhusu nidhamu.

Nguvu ya mwalimu

Tulianza mafunzo yale kwa kutafakari nafasi ya mwalimu katika maisha ya mwanafunzi. Niliwaeleza walimu wale kuwa kazi yao ni zaidi ya kuhakikisha wanafunzi wamefaulu mtihani. Mwalimu anayehesabu mafanikio ya kazi yake kwa kuangalia alama anazopata mwanafunzi darasani na kuishia hapo; huyu kwa hakika hajatambua kazi yake.

Kazi ya ualimu ni kuwalea wanafunzi kwa namna inayowawezesha kuitambua ‘dhahabu’ iliyojificha ndani yao na kisha kuwasaidia kukusanya uwezo wa kufikia ndoto zao. Hiyo ndiyo kazi kubwa ya mwalimu, yaani kulea maono ya wanafunzi wao.

Tulikubaliana kimsingi kuwa anayoyafanya mwalimu yanabaki kwenye kumbukumbu za mwanafunzi kwa muda mrefu. Maneno na tabia za mwalimu zina uwezo wa kumuathiri mwanafunzi kwa miaka mingi ijayo.

Tulikumbushana walimu waliotutukana tukiwa darasa la pili. Tukasimuliana kumbukumbu za walimu waliotudhalilisha kwa maneno makali enzi hizo tukiwa wanafunzi wadogo. Miaka mingi baadaye bado tunawakumbuka. Hiyo ndiyo nguvu aliyonayo mwalimu.

Kupitia uhusiano wake na mwanafunzi wake, mwalimu anaweza kabisa kubaki kwenye fahamu za mtoto kwa miaka mingi ijayo. Nilipowauliza walimu hawa namna gani wangependa kukumbukwa na wanafunzi wao, wengi walitamani kujenga kumbukumbu njema kwa wanafunzi wao.

Kufikia hapo nikawauliza, kwa nini hutokea mwanafunzi akamdharau mwalimu wake? Nini hufanya mwalimu akose ushawishi kwa mwanafunzi wake? Kwa nini tunafika mahali mwalimu anajikuta kwenye mazingira ya kukumbukwa kwa ukali wake kwa wanafunzi?

Ushawishi alionao mwalimu

Mwalimu ana nafasi ya kuwa na ushawishi mkubwa kwa mwanafunzi wake. Ushawishi maana yake ni ule uwezo wa mwalimu kusikika, kuigwa au kuheshimiwa na mwanafunzi bila kumtisha, kumkemea au kumwadhibu. Uwezo huu, ambao bila shaka kila mwalimu anauhitaji, unaweza kupotezwa na mambo kadhaa.

Mosi, mazingira mabovu ya shule yanayomfanya mwalimu aonekane si lolote kwa mwanafunzi. Mazingira ya shule yanapomfanya mwalimu aonekane si mtu wa kuheshimika, ni vigumu kutegemea mwalimu huyu ataweza kuwa na chochote cha maana kinachoweza kuigwa na kusikilizwa na mwanafunzi.

Heshima ya mwalimu haianzii darasani. Maisha yake nje ya kipindi yana nguvu ya kuamua ikiwa wanafunzi watakuwa na sababu ya kumsikiliza ama la.

Fikiria mwalimu anayetukanwa na mkuu wa shule mbele ya wanafunzi. Fikiria mwalimu anayetoa maelekezo na mkuu wa shule anayabatilisha mbele ya wanafunzi. Fikiria mwalimu anayeishi maisha duni kwa sababu uongozi wa shule haujaweza kumpatia haki yake.

Mambo kama haya yanaweza kuathiri ushawishi tunaotarajia mwalimu awe nao. Ni muhimu basi kwa uongozi wa shule na mamlaka za elimu kulinda hadhi ya mwalimu wakati wote.

Lakini pia, kuna suala la tabia ya mwanafunzi mwenyewe. Kama nilivyotangulia kugusia hapo awali, mazingira aliyokulia mwanafunzi yanaweza kumfanya akajenga dharau kwa mwalimu. Wapo wanafunzi, mathalani wanaoamini mwalimu si mtu wa kuheshimiwa.

Hawa wameaminishwa mtu pekee wa kupewa heshima ni yule mwenye wingi wa vitu. Heshima inategemea aina ya gari anayoendesha mtu, aina ya mavazi anayoonekana nayo mtu na mambo mengine kama hayo.

Katika mazingira ambayo pengine mwalimu haonekani kuwa na mafanikio yanayokidhi matarajio hayo ya mwanafunzi, inakuwa rahisi mwanafunzi kujiona ana haki ya kumdharau na kumtendea jeuri mwalimu wake. Na ilivyo ni kwamba tabia nyingi wanazozionyesha wanafunzi dhidi ya walimu, zinatokana na mitazamo waliyonayo kwa mwalimu wao.

Kujenga mamlaka ya mwalimu

Pamoja na sababu hizo, bado kuna ukweli kuwa tabia zako mwalimu zina mchango mkubwa wa kujenga heshima yako kwa wanafunzi. Unao wajibu wa kujenga mamlaka yako yatakayokufanya uheshimiwe na wanafunzi wako.

Tunapozungumzia mamlaka, tuna maana ya uwezo wako mwalimu kujenga ushawishi utakaokujengea mazingira ya kusikilizwa na mwanafunzi bila kulazimika kutumia mbinu za kimabavu. Kuna masuala kadhaa ya kuzingatia ikiwa unahitaji kujijengea mamlaka yako.

Kwanza, ni muhimu kujiheshimu kwa maana ya kuhakikisha kuwa tabia zako zinaakisi heshima unayoitarajia kwa wanafunzi wako.

Kabla hujatarajia kuheshimiwa, lazima ujiulize: je, unavaa kama mtu anayejiheshimu? Je, unazungumza kama mtu anayejiheshimu? Unaishi kama mtu anayestahili kuheshimiwa?

Heshima haina muujiza. Upandacho ndicho utakachovuna. Huwezi kuvaa kama waraibu wa madawa ya kulevya na bado ukategemea wanafunzi watakuheshimu. Kipimo unachojipimia ndicho utakachopimiwa na wanafunzi wako.

Unapokuwa mwalimu mlevi, mwalimu anayefahamika kwa tabia za ovyo kama uzinzi na matusi unajishushia heshima. Wanafunzi wanapokuita shemeji kwa sababu una uhusiano wa kimapenzi na mwenzao, usitegemee utaongea kitu wakakisikiliza. Lazima watakudharau kwa sababu hicho ndicho unachostahili kama mwalimu asiyejiheshimu. Itaendelea wiki ijayo

Blogu: http://sw.globalvoices.org Twitter: @bwaya