Mwamko kodi ya majengo umeilemea TRA

Wananchi wakiwa kwenye foleni ya kulipa kodi ya majengo kwenye ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyopo Barabara ya Lumumba eneo la Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana. Picha Omar Fungo

Muktasari:

Kadri siku zinavyokwenda ndivyo tunaendelea kushuhudia idadi kubwa ya watu na hivyo ile tafsiri ya Rais John Magufuli kwamba watu wanajitokeza kulipa kodi kwa hiari, inazidi kudhihirika.

Tangu muda wa kuhakiki na kulipa kodi ya majengo ulipoongezwa kutoka Juni 30 hadi Julai 15, misururu ya watu imeendelea kutawala ofisi za Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA).

Kadri siku zinavyokwenda ndivyo tunaendelea kushuhudia idadi kubwa ya watu na hivyo ile tafsiri ya Rais John Magufuli kwamba watu wanajitokeza kulipa kodi kwa hiari, inazidi kudhihirika.

Hali hii inaashiria kwamba watu wanaohitaji huduma hiyo, bado ni wengi na hawakujitokeza siku za mwisho kama ambavyo imekuwa inatokea kila mara pale mamlaka hiyo inapotumia utaratibu kama huu kufanikisha jambo fulani.

Ni kutokana hali hiyo inayojitokeza katika vituo vyote vya kukusanyia kodi hiyo, wakazi wa Dar es Salaam jana walinukuliwa na gazeti hili wakiiomba TRA iongeze muda wakibainisha kuwa siku zilizosalia ni chache na watu bado ni wengi.

Maombi ya wakazi hao ni ya msingi na wazi kwa kuwa misururu ya watu inaonekana kila mahali na hivyo sababu zilizoisukuma TRA kuongeza muda kwa mara ya kwanza hadi leo, zinaendelea kuwapo.

Katika kituo cha Mkoa wa Kinondoni, misururu ilianzia katika maegesho ya magari ya jengo la LAPF Kijitonyama na baadhi ya watu walikuwapo tangu alfajiri hadi jioni bila kufikiwa na maeneo mengine walilazimika kukatisha hata barabara.

Pamoja na kuwa mkurugenzi wa elimu kwa mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amewataka wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi kabla ya siku ya mwisho haijafika, tunaamini kuwa hali ilivyojionyesha hadi jana hakutakuwa na sababu ya muda huo kutoongezwa.

Mbali na foleni hizo, wapo watu walioshindwa kuvumilia foleni ndefu na kuamua kurejea majumani kusubiri wakati mwingine ambao utakuwa na unafuu au pale muda utakapoongezwa.

Tukitambua kuwapo umuhimu wa kukamilisha malipo hayo kabla ya Juni 30 kwa watu waliosajiliwa kulipa kodi hiyo miaka ya nyuma au mwaka jana baada ya kodi hiyo kuhamishiwa TRA. Pia, mamlaka hiyo inatakiwa kutambua kuwa kuna walipaji wapya ambao ndio kwanza wanasajiliwa kwa mara ya kwanza, hivyo hakuna ulazima wa kuwabananisha kwenye siku chache wakati mwaka mzima wa fedha 2017/18 ndio kwanza unaanza.

Wakati usajili huo na malipo unaendelea yamekuwapo malalamiko mengine ambayo bila shaka TRA inayasikia na pengine inayafanyia kazi kuhusu suala la tofauti ya makadirio ya kiwango cha kulipa yanayokinzana na tamko la Serikali au tangazo la mamlaka hiyo.

Wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema kwenye Bajeti yake kwamba “nyumba zote ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango maalumu (flat rate) cha Sh10,000 kwa nyumba ya kawaida na Sh50,000 kwa nyumba za ghorofa; tangazo la TRA lilitoa viwango tofauti kati ya Sh15,000 na Sh20,000.

Mbali na matamko hayo, wapo watu ambao wamekwenda TRA na kukuta tathmini tofauti wakati wanaamini nyumba zao ni za kawaida. Lakini pia tatizo la mtandao kuwa chini limefanya misururu kukua siku hadi siku.

Tunadhani kuwa TRA itatathmini matatizo hayo pamoja na utendaji wake na kuona umuhimu wa kuongeza muda kabla ya siku ya mwisho ya malipo bila faini.