Mwamko mpya Cecafa ulete matumaini mapya

Muktasari:

  • Michuano hiyo inaandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa). Mara ya mwisho mashindano hayo yalifanyika mwaka 2015 na Uganda ikatwaa ubingwa.

Kuanzia Desemba 3 hadi 17 mwaka huu Kenya itaandaa michuano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Michuano hiyo inaandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa). Mara ya mwisho mashindano hayo yalifanyika mwaka 2015 na Uganda ikatwaa ubingwa.

Baada ya hapo hayakufanyika kwa miaka miwili kutokana na sababu tofauti, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa wadhamini na nchi wanachama kutokuwa tayari kuandaa, huku Tanzania na Rwanda zikiwa zinaokoa michuano hiyo kila Cecafa ilipokuwa inakwama.

Hata hivyo, kwa kipindi chote hicho, nchi hizo zimekuwa kimya kiasi cha Kenya kukubali kuyaandaa mashindano hayo.

Hatutaki kuingia ndani zaidi kuangalia utendaji kazi wa Cecafa kama chombo cha kusimamia soka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Lakini ukanda huu ndio bado unafanya vibaya katika ngazi ya taifa na klabu kwa kuwa ni kwa nadra sana timu za taifa za nchi wanachama hufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika na hazijawahi kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Klabu nazo zimekuwa haziendi mbali kwenye mashindano ya klabu ya Afrika.

Ukanda wa Cecafa umekuwa ngazi kwa timu za kanda mwingine kufuzu kucheza hatua za juu za mashindano ya Afrika au dunia.

Hii ni ishara mbaya kwani mafanikio ya mataifa ya Afrika Magharibi au Kaskazini yanatakiwa kuwa hayo ya Afrika Mashariki, lakini haiko hivyo.

Ukiangalia upande mwingine, Cecafa imekuwa haina programu za maendeleo kwa nchi wanachama, kama mafunzo ya walimu, viongozi, waamuzi na madaktari ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya mpira.

Lakini kufufuliwa kwa mashindano ya Kombe la Chalenji, ambayo hushirikisha timu za taifa za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Sudan, Djibout na wageni kutoka kanda hii, ni ishara kwamba Cecafa imerudi katika njia sahihi.

Wakati michuano ya Cecafa ambayo ni mikongwe barani Afrika haikuwa ikitoa matumaini yoyote, michuano ya Shirikisho la Soka la Nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa) imesaidia kukua kwa kiwango cha nchi wanachama.

Cosafa sasa wana mashindano ya timu za taifa za wakubwa, ambayo hujumuisha zaidi wachezaji ambao wanaandaliwa na mataifa yao kwa ajili ya baadaye. Pia ina mashindano ya vijana walio na umri chini ya miaka 20 na hali kadhalika chini ya miaka 17.

Hii inasaidia mataifa wanachama kuwa na mikakati mizuri ya kuimarisha timu zao za taifa na si ajabu nchi kama Lesotho, Botswana na Swaziland zikatuacha katika kipindi kifupi kijacho.

Tunatarajia kuwa viongozi wa Cecafa wamejifunza kutoka Cosafa na sasa wamekuja na nguvu mpya ambayo itasisimua maendeleo ya soka.

Pia uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuamua kila kanda iwe inatoa wawakilishi wawili kwenye mashindano ya Afrika ya vijana walio na umri chini ya miaka 17, itaifanya Cecafa kujiimarisha zaidi ili itumie nafasi hiyo vizuri.

Cha muhimu ni viongozi wa Cecafa kuongeza bidii ya kuandaa programu zitakazovutia kampuni ili ziwekeze fedha kwenye mashindano yake na hivyo kuwa rahisi kuendeleza soka.

Tunategemea mwamko mpya wa Cecafa utakuja na mengi mapya na mazuri kwa soka.