Mwana hawezi kuadhibiwa kwa kosa la baba yake mzazi

Muktasari:

  • Mtu mwenye hasira alimkosa panya kwa risasi akavunja redio ya thamani na kioo cha dirisha. Alikuwa kwenye hekaheka za kumuua panya aliyekula vyeti na shahada zote muhimu. Kama vile haitoshi, panya huyohuyo akaja kumguguna kisigino chake kabla hajaamka!

Mmoja wa maadui wakubwa wa mwanadamu ni panya. Panya huguguna kila akionacho mbele yake bila sababu za msingi. Haangalii kama ni chakula au la. Binadamu humuona panya kuwa anafanya uhuni kwa sababu mnyama huyu mdogo anajua kula chakula bora.

Mtu mwenye hasira alimkosa panya kwa risasi akavunja redio ya thamani na kioo cha dirisha. Alikuwa kwenye hekaheka za kumuua panya aliyekula vyeti na shahada zote muhimu. Kama vile haitoshi, panya huyohuyo akaja kumguguna kisigino chake kabla hajaamka!

Kumbe panya alikuwa na la kujitetea. Meno yake hurefuka kwa inchi tano kila mwaka, na akiyaachia hutoboa fizi zake na kumtoa damu. Ili kuyazuia, huyasaga kwenye vitu vigumu. Kwa bahati mbaya zaidi fizi zake humuwasha wakati wa ukuaji wa meno hivyo hujikuna kwa ‘kuguguna’ suti na vyeti vya wenzie.

Mtaani kwetu kulikuwa na dogo tuliyemwita Jerry kwa kumfananisha na katuni ya panya. Kwanza alikuwa mchokozi, kisha alijua kuyatumia meno yake. Akiona mwenzie ana mpira basi haraka atauguguna. Sanamu za watoto, madaftari na kila kitu aliguguna. Na ukimgusa tu, anakutia meno.

Kumbe hata akiwa nyumbani. Tulimsikia mama yake akipiga uyowe: “Jamani hili toto sijui nikabadilishane na nani…” Maana ‘aliguguna’ hadi sabuni za chooni. Na alikuwa na tumbo zuri sana maana hakuharisha wala kuumwa.

Hata hivyo, mama alimpenda. Atapiga kelele kutwa nzima akiapa kumuuza kwa jero, kumbadilisha kwa kinda la bata au hata kumtupa jaani. Lakini ukitaka kuona mcharuko wa Komba, mwaga ‘kiroba’ chake (sorry, mwaga pombe yake). Ukimtia konzi yule dogo ndipo utajua kuwa uchungu wa mwana aujuaye mzazi.

Kinyume chake dada mlezi aliyemlea mtoto wakati mama yake akiwa kazini. Mama alikuja kugundua kuwa mwanaye alibadilika rangi kila mwezi. Kila tarehe thelathini alivimba na kuingia wekundu kidogo. Akaamua kufanya uchunguzi.Alibaini ukweli uliomtoa machozi yenye ukakasi wa limao.

Mara nyingi yeye alichelewa kulipwa mshahara, hivyo alilazimika kumlipa msaidizi wake katika tarehe za mwanzo za mwezi uliofuata. Kumbe masikini dada alijazwa upepo na kuamini kuwa alifanyiwa kusudi. Akaamua kujifariji kwa kumgeuza mtoto kuwa ngoma ya chapuo.

Alimdunda kutoka asubuhi hadi mchana, kisha akamwogesha na kusubiri mshiko wake jioni. Asipoletewa, kesho wembe ni ule ule. Hatimaye arobaini yake iliwadia asubuhi moja mama alipofanya ziara ya kushtukiza nyumbani. Alimkuta dada akiwa juu ya mwanaye huku kichapo kikiendelea.

Inaumiza sana. Kweli zipo adhabu anazoweza kubebeshwa mtu kwa kosa la kumficha mhalifu, lakini hata kama damu ingekuwa nzito kuliko mlenda, hakuna baba ambaye angefungwa kulipia madhambi ya mwanaye. Hata kama penzi ni upofu, lakini haiwezekani kumfunga mke kwa kosa la mume.

Kwa bahati nzuri Watanzania tumefunzwa kuishi kama ndugu. Sote tunaishi chini ya baba mmoja. Baba huyu asipozingatia mahitaji ya mmoja wetu, basi tunayo nafasi ya kuongea naye. Iwapo atatudharau au kutufukuza tutapeleka kilio kwa mama.

Haiingii akilini iwapo kaka mkubwa atakosa haki yake kwa baba ati aje kututia makonzi wadogo zake. Hii si njia madhubuti ya kumshurutisha baba kurekebisha mwenendo. Tena kama ni baba wa kufikia ndio atazidi kukaza kamba ili mkosane kabisa apate kuwatimua.

Sisi sote ni ndugu; tatizo la mmoja ni la kwetu sote. Huwa naona jambo la ajabu sana pale taasisi muhimu inapogoma kuwatumikia wananchi ati kwa sababu ya kuiwajibisha Serikali.

Kwa mfano yawezekana kuna ukiukwaji wa haki za msingi kama upungufu wa mishahara kwa wafanyakazi, longolongo kwenye mashine za risiti kwa wafanyabiashara au miswada ya sheria kwa wasafirishaji, lakini kugoma kutoa huduma kwa wananchi ni kuwaonea wananchi.

Serikali ndiyo mhimili mkuu na rungu la dola. Baada ya Serikali kuna Bunge na Mahakama. Iwapo Serikali itafanya maamuzi inayoona ni ya manufaa, ikasema “Twende huku!” lakini mwananchi wa kawaida akaona huko hakuwezekani, basi ni wajibu wake kuishirikisha mihimili hii mingine.

Wakati mwingine si kwamba Serikali inaamua kibabe, ila ukienda safari ya miguu na mwanajeshi si makosa kumuomba apunguze mwendo. Hivyo hata Serikali inaweza ikashauriwa na wananchi lakini kwa njia zinazokubalika na kutambuliwa kisheria.