Mwanamichezo anatakiwa kuwa msafi wakati wote

Muktasari:

  • Mwanamichezo kujiweka msafi kimwili ni mojawapo ya mambo ya msingi katika kuzuia kupata maambukizi, magonjwa na harufu mbaya ya mwili.

Usafi wa mwili kwa mwanamichezo ni jambo ambalo ni la lazima kutokana na sababu za mbalimbali ikiwamo mwanamichezo binafsi, kiafya, kijamii na kisaikolojia.

Mwanamichezo kujiweka msafi kimwili ni mojawapo ya mambo ya msingi katika kuzuia kupata maambukizi, magonjwa na harufu mbaya ya mwili.

Wengi tunajitambua kuhusu umuhimu wa usafi wa mwili pengine kutokana na mafunzo tunayopata tangu utotoni, kupitia mashuleni ambako pia tumewahi kukutana na wanafunzi walionekana kuwa na matatizo ya usafi wa mwili.

Tunajitambua pia kuwa wasafi kama njia mojawapo yakuvutia jinsia nyingine na kuepuka kutengwa au kukimbiwa na marafiki utakaokutana kutokana na harufu mbaya ya mwili.

Vile vile kwa kufahamu kuwa kutokuwa msafi ni kuhatarisha afya yako ya mwili.

Hivyo basi kwa yule asiyetambua haya ipo haja ya kuelimishwa ili aweze kurudi katika kundi la wanajamii wenye kupenda usafi wa mwili.

Mwanamichezo ni kama kioo cha jamii, wanajamii wengi wanapokutana na wanamichezo maarufu hutamani kumshika mkono na kumsalimia kwa karibu.

Kuwa msafi kunakufanya kuwa na mwonekano mzuri hivyo kunakufanya ujiamini na kuwa na mwamko kimchezo hata unaposhiriki michezo unakuwa na msisimko wa mafanikio.

Ikumbukwe vyombo vya habari vinatoa habari ikiwamo katika Tv, Radio na magazeti kuwa na mwonekano msafi ina ongeza thamani na heshima katika jamii.

Usafi wa mwili unawapa picha jamii namna tabia zako zilizo, jamii inapendelea zaidi watu wanaojipenda. Kuwa msafi kunaongeza utu wako.

Ukiacha yote hayo, kuwa msafi ni hatua muhimu kwa mwanadamu kuwa na afya njema. Mwanamichezo mchafu hukumbana na magonjwa ya mbalimbali ikiwamo fangasi wa ngoz katika miguu, nywele, kucha.

Vile vile huweza kupata maambukizi ya ngozi yaliyotokana na bacteria ikiwamo upele na majipu.

Mwili wa mwanamichezo mchafu uko katika hatari yakupata fangasi za sehemu za siri, maradhi ya kinywa na harufu mbaya ya mdomo na kuwashwa mwili.

Ukiwa mwanamichezo unapaswa kuhakikisha kuwa unaoga kila unapomaliza kucheza kwa maji safi na sabuni ikiwezekana angalau oga mara tatu kwa siku.

Hakikisha nguo zako za michezo, jezi na vifaa unavyotumia zinafuliwa au kuoshwa na sabuni zilizo na kiambatana kinachoweza kuangamiza vimelea vya maradhi.

Kuwa na tabia yakunawa mikono yako kwa sabuni kwani mikono inashika maeneo mbali mbali hivyo kuwa chanzo cha kusambaza maambukizi.

Safisha kinywa chako kila unapomaliza kupata mlo, na kunywa maji ya kutosha kila siku.

Mwanamichezo mwenye jeraha la wazi hakikisha kidonda chako kinafanyiwa usafi na huku ukihakikisha kinabaki kuwa kisafi.