Mwandishi anayejitambua haombi wala hapokei rushwa

Muktasari:

  • Kwa kipindi kirefu sasa, vyombo hivi vya habari vimekuwa vikichapisha tangazo maalumu kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

Kwa mara nyingine, Meza ya Mhariri wa Jamii inalazimika kuwasiliana na wananchi wote, hasa wasomaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti juu ya hoja ya rushwa.

Kwa kipindi kirefu sasa, vyombo hivi vya habari vimekuwa vikichapisha tangazo maalumu kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

Katika Mwananchi na Mwanaspoti tangazo limebeba kichwa: ‘Tunakataa rushwa.” Katika The Citizen kichwa kimekuwa: ‘We don’t condone corruption.’

Tangazo hili lilitokana na malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa baadhi ya magazeti na vyombo vingine vya habari nchini, vinaomba na, au kupokea rushwa ili kuchapisha taarifa zao.

Magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti huchapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ya jijini Dar es Salaam. Kampuni inaendesha pia mitandao kadhaa ya kijamii.

Katika juhudi za kujitofautisha na magazeti na vyombo vingine vya habari, ambavyo huenda waandishi wake wamekuwa wakipokea rushwa; vyombo vya MCL vimekuwa vikitoa tangazo kwa karibu mwaka mzima sasa kueleza msimamo wake kwa wasomaji.

Katika miezi minne ya kwanza ya kutangaza kupinga rushwa, hakuna yeyote aliyejitokeza kudai kutoa, kuombwa au kuona mwandishi anashawishi kupewa rushwa.

Wasomaji 52 waliolalamikia rushwa katika kipindi hicho, hawakutaja mwandishi au chombo cha habari chochote.

Walikuwa na madai na tuhuma katika uhusiano wao wa kifamilia, kirafiki na baadhi ya viongozi binafsi kwa ngazi wanakoishi.

Hata hivyo, hilo haliondoi madai na tuhuma za awali za baadhi ya wananchi kwamba “baadhi ya waandishi wamekuwa wakipokea bahasha za khaki zenye fedha ndani” ili washawishike kutoa au kutoa haraka, taarifa za wahitaji. Bado tuhuma zipo.

Hii ndiyo maana kumekuwa na juhudi za kuelimisha wananchi juu ya mfumo wa kutoa taarifa kwa mwandishi wa MCL na kufanya hivyo bila kudaiwa chochote. Hebu tujikumbushe taarifa kuhusu hili:

“Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), inazingatia uadilifu na umakini mkubwa. Haijayumba katika dhamira yake ya kuhakikisha waandishi wa habari wa magazeti na mitandao yake ya intaneti wanajitenga kabisa na rushwa.

“Ifahamike kwa wote, kwamba wahariri, maripota na wapigapicha wa MCL, wamezuiwa kabisa kushawishi, kupokea fedha au aina yoyote ya malipo au kishawishi chochote, kwa ajili ya kuchapisha taarifa, habari, maoni au makala.

“Maudhui hayo hayatozwi kiasi chochote cha fedha. Huchapishwa bure; na kigezo cha kuyachapisha ni sifa au ubora wake peke yake na maudhui pekee ya kugharamia ni tangazo.”

Kwa hiyo, MCL inawaomba wasomaji wa magazeti na mitandao yake ya habari, kutoa taarifa pindi watiliapo shaka mazingira yoyote ya rushwa; au hata kuona ambako wahariri, maripota, wapigapicha na wafanyakazi wake wengine wamekiuka misingi hii ya maadili.

“Tunaahidi kuchunguza madai na tuhuma zote kwa kina; na wale watakaobainika kukiuka watashughulikiwa ipasavyo,” linaeleza tangazo la MCL.

Kampuni inaweka wazi kwamba waandishi wake wote wa habari wana vitambulisho vya kampuni na kile kinachotolewa na Idara ya Habari (Maelezo) – Press Card.”

Hapa kuna msaada kwa wasomaji. Wanaambiwa moja kwa moja, “usitoe chochote.” Kama una taarifa unazoona ni kwa manufaa ya jamii; kuona tukio na hata kuwa na maoni binafsi, usilipe chochote ili zichapishwe.

Kinachoamua ubora wa taarifa siyo fedha ambazo unataka kutoa au ambazo unaweza kuwa unaombwa; bali mwenye stadi; aliye na ujuzi na maarifa juu ya kinachofaa na kinachostahili; na mwenye mamlaka ya kufanya au kuagiza lolote lifanyike ili taarifa iandikwe, ichapishwe au itangazwe.

Katika hatua zote hizo hakuna mahali ambako mwenye taarifa anapaswa kulipa chochote kwa utashi wake au kwa kuombwa. Ni katika mazingira haya mwandishi anastahili kukataa hongo kutoka kwa yeyote yule; na kukataa kuomba “chochote.”

Tunabaki na mkondo mmoja wa wasiokuwa waandishi wa habari kujitambulisha kuwa ni waandishi na kuomba rushwa ili “wasikuandike vibaya,” au kukuwasilishia taarifa kwa haraka.

Hawa ni waovu kama waovu wengine. Ni hao tunaokutaka uwaulize kitambulisho cha kampuni na kile cha Maelezo. Kama hawana, basi siyo waandishi wa habari na siyo wa MCL.

Hata wakiwa na vitambulishovyote; kama wanakutwa wakidai na au kupokea rushwa, wanastahili kuripotiwa. Mahali pa kuripoti ni kwa mhariri ambaye anwani yake imo gazetini; au kwa Mhariri wa Jamii kwa simu na baruapepe zifuatazo:

Simu: 0763670229/0713614872/0783190510 Barua pepe:[email protected]