NEC iangalie idadi ya wapigakura kupungua

Muktasari:

Katika Jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia alishinda kwa kura 30,247 huku mpinzani wake mkuu, Salum Mwalimu wa Chadema akipata kura 12,353.

Uchaguzi wa marudio wa majimbo mawili ya Kinondoni na Siha uliofanyika Jumamosi, umeshuhudia wagombea ubunge wa CCM wakishinda.

Katika Jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia alishinda kwa kura 30,247 huku mpinzani wake mkuu, Salum Mwalimu wa Chadema akipata kura 12,353.

Katika Jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel wa CCM alishinda kwa kura 25,611 dhidi ya Elvis Mosi wa Chadema aliyepata kura 5,905 na Tumsifueli Mwanri wa CUF aliyepata kura 274.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kuwa katika Jimbo la Kinondoni, Mtulia ameshinda kwa pungufu ya zaidi ya kura 40,000 tofauti za mwaka 2015 alipopata kura 70,337 aliposhinda kupitia CUF.

Idadi ya kura hizo za Mtulia ni nusu ya zile alizopata miaka mitatu iliyopita kwani alipata kura 70, 337 dhidi ya mpinzani wake, Idd Azzan wa CCM aliyekuwa amepata kura 65,964.

Katika jimbo hilo, waliojiandikisha walikuwa 264,055 lakini waliojitokeza kupiga kura ni 45,454 sawa na asilimia 17.2 tu.

Ukiangalia katika Jimbo la Kinondoni tu, ina maana kuwa kuna zaidi ya watu 200,000 ambao hawakujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo.

Hii haileti picha nzuri kwani kama zaidi ya asilimia 80 ya watu waliojiandikisha kupiga kura hawakujitokeza ina maana kuna tatizo mahali fulani.

Hiyo inaweza kuwa imetokana na sababu mbalimbali kama wachambuzi wa siasa wanavyoweza kujadili.

Kuna ambao wengi wanasema ni kuwa watu wamechoka kupiga kura mara kwa mara, wengine wanasema mwamko wa watu umepungua katika siasa na sababu nyingine ni za kuwapo kwa uchaguzi wenyewe.

Kwa sababu zozote ambazo zitatolewa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ina kazi kubwa ya kutoa elimu zaidi ya kuwaelezea wananchi umuhimu wa kupiga kura.

Mafanikio ya NEC si kusimamia tu uchaguzi, ila ni kuhakikisha watu wengi zaidi wanajitokeza na kutumia vizuri haki yao ya kidemokrasia.

Uwakilishi unapokua mkubwa katika uchaguzi inapendeza zaidi kidemokrasia kuliko mbunge anapochaguliwa na idadi ndogo ya wapigakura.

Ukiangalia mfano huu wa Kinondoni, miongoni mwa majimbo yenye watu wenye elimu, mwamko wa kisiasa na kwamba jimbo lipo mjini, inasikitikisha kuona idadi ndogo ya watu waliojitokeza.

Ingawa kuna hoja inajengwa kuwa chaguzi ndogo na za marudio huwa na idadi ndogo, tunataka hiyo isiwe sababu ya kiujumla jumla badala yake utafiti ufanyike ili kujua sababu za msingi.

Uchunguzi huo utaleta majibu sahihi ambayo yatatumiwa na NEC kwa ajili ya kujua mikakati ya kuhamasisha watu wajitokeze zaidi katika chaguzi zijazo.

Lakini ni muhimu kwa NEC pia kuangalia malalamiko kutoka vyama vyote vya siasa kama huwa yanafanyiwa kazi au yanajibiwa kisiasa au kitaalamu. Kwa sababu kama kuna kundi la watu wanaamini kuwa chama chao hakitendiwi haki itakuwa ngumu kwao kujitokeza kupiga kura.

Ingawa katika siasa na uchaguzi, hisia na mihemko huwa inatawala zaidi, ni vizuri NEC kama msimamizi mkuu wa uchaguzi ikawa inashughulikia malalamiko ya vyama vya siasa kwa haraka ili kupunguza malalamiko.

Huku tukiamini kuwa NEC itakuwa imeona changamoto zilizojitokeza Kinondoni katika uchaguzi huu, inapaswa kujipanga ili siku zijazo kusitokee malalamiko mengi na kuwe na wapigakura wengi zaidi.