MAONI: NEC ifanyie kazi malalamiko yote ya uchaguzi

Muktasari:

  • Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athumani Kihamia huku akisisitiza kwamba wataongeza nguvu kwenye eneo la elimu, hususan kwa vyama vya siasa ili kupunguza malalamiko yanayojitokeza.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza kuanza kujipanga kupunguza malalamiko na kwamba nguvu itaelekezwa katika utoaji wa elimu. Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athumani Kihamia huku akisisitiza kwamba wataongeza nguvu kwenye eneo la elimu, hususan kwa vyama vya siasa ili kupunguza malalamiko yanayojitokeza.

Dk Kihamia alisema wamebaini baadhi ya malalamiko yanatokana na elimu ikiwamo suala la mawakala na ujazaji wa fomu za wagombea.

Tunaunga mkono uamuzi huo wa NEC kwa kuwa elimu katika masuala ya uchaguzi ni jambo la msingi na hasa katika mfumo wa demokrasia wa vyama vingi vya siasa.

Pamoja na kupongeza mpango huo wa NEC, ni vyema Tume hiyo ikajipanga kuyamaliza kabisa matatizo hayo kwani ni miaka 26 tangu Tanzania ilipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa na yamekuwa yakiripotiwa kila uchaguzi unapofanyika.

Rai yetu pia kwa NEC ikumbuke kufanyia kazi hoja zinazotolewa na vyama vya upinzani ikiwamo vikwazo katika utoaji fomu za mawakala, uapishaji wa mawakala na kubadilishwa vituo kwa taarifa za ghafla.

Pia, NEC inapaswa kujitathmini yenyewe kwa kujiuliza swali, kwa nini matatizo ya mawakala na ujazaji fomu yanawapata wagombea wa upinzani pekee?

Mfano, tukio la mawakala wa upinzani wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni, kulikuwa na haja gani ya mawakala hao kunyimwa fomu hadi zikatokea vurugu zilizosababisha kifo na watu wengine kujeruhiwa?

Vilevile, NEC iipatie jawabu changamoto ya wasimamizi wa uchaguzi wanaoelezwa kuwazuia mawakala wa vyama vya upinzani kuingia kwenye vituo vya kupigia kura. Vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamikia kuhusu wasimamizi kuwa makada wa chama tawala, NEC inapaswa kuyafanyia kazi madai hayo na kuyapatia ufumbuzi.

Pia, haina budi kuyafanyia kazi malalamiko ya upinzani kwamba matamko ya baadhi ya watumishi wa umma hasa wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu kujihusisha na kampeni.

Ni rai yetu pia kwamba elimu hiyo itawafikia wasimamizi wa uchaguzi ambao wamekuwa wakilalamikiwa kwa kuonyesha upendeleo kwa vyama wanavyoshabikia.

Sambamba na elimu hiyo, ni imani yetu kwamba NEC itaangalia namna bora ya kuepuka lawama kwamba hawatendi haki linapofika suala la uchaguzi.

Elimu hiyo pia ilenge kuimarisha ushirikiano wa Tume hiyo na wadau wengine wa uchaguzi kama vile Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ili kuleta utulivu wa kisiasa.

Tunaamini kwamba katika mpango huo wa utoaji wa elimu, NEC pia italiweka katika orodha suala la ujazaji wa nafasi za wabunge wa viti maalumu kwani imekuwa ikilalamikiwa kwamba katika baadhi ya matukio imewasiliana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakati ikijua chama kinachotakiwa kujaza nafasi kina mgogoro.

Tunaamini kuwa, iwapo NEC itayafanyia kazi malalamiko yote hayo, uwanja wa siasa utakuwa katika hali nzuri na uchaguzi utakuwa ukifanyika kwa amani na utulivu, badala ya kulazimika kutumia nguvu kubwa ya vyombo vya dola. Tunaamini vyama vyote vya siasa vitashiriki kikamilifu katika elimu hii ili kumaliza migogoro isiyokuwa na lazima.