Nape alitakiwa atetee Sheria ya Vyama vya Siasa

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye

Muktasari:

  • Nape alisema hayo alipohojiwa na kituo cha televisheni cha KTN kuhusu madai ya viongozi wa Chadema kwamba Rais John Magufuli anaminya demokrasia, hasa kuzuia mikutano ya hadhara.

Mwishoni mwa wiki iliyopita mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye akiwa Nairobi, Kenya alisema kuzuiwa mikutano ya kisiasa si kuminya demokrasia kwa kuwa kuna Bunge ambalo linaweza kutumika kutoa maoni.

Nape alisema hayo alipohojiwa na kituo cha televisheni cha KTN kuhusu madai ya viongozi wa Chadema kwamba Rais John Magufuli anaminya demokrasia, hasa kuzuia mikutano ya hadhara.

Katika majibu yake, Nape aliyewahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema uchaguzi ukishamalizika siasa zinahamia bungeni ambako wabunge wanaweza kutoa maoni yao.

Pia, alisema zamani wanasiasa waliruhusiwa kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali nchini. Kisha akasema wakati wa Uchaguzi Mkuu shughuli nyingi huwa zinasimama kwa sababu ya mikutano ya wanasiasa.

Majibu haya yanasikitisha kwa sababu Watanzania wanaelewa vizuri demokrasia ya zama za mfumo wa chama kimoja na baada ya vyama vingi kurejeshwa mwaka 1992.

Watanzania wanajua kila nchi inaendesha shughuli zake kwa kuzingatia Katiba na sheria. Na ndiyo maana hapa kwetu mkuu wa nchi anapokula kiapo huwa anaapa kuilinda Katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayounda sheria za nchi.

Ibara ya 18 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa fursa ya kujumuika ikisema bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

Sehemu ya (2) inasema kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.

Mbali ya Ibara hiyo ya 18 ya Katiba, sehemu ya lV ya sura ya 258 ya Sheria ya Vyama vya Siasa sehemu inatoa haki kwa chama chochote cha siasa kuandaa mkutano au maandamano.

Ibara ya 11 ya sheria (1) inasema chama chochote chenye usajili wa muda au wa kudumu; (a) kinaruhusiwa kuandaa mikutano yake eneo lolote katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kujitangaza au kutafuta wanachama baada ya kuwapa taarifa polisi wa eneo husika; (b) kinastahili kupewa kinga na msaada wa ulinzi ili kiweze kufanya mkutano wake kwa amani.

Lakini Nape anasema: “Hapa kwetu baada ya Uchaguzi Mkuu tunaruhusiwa kufanya mikutano kwenye majimbo, haturuhusiwi kufanya mikutano nje ya majimbo yetu.”

Kwa kauli hiyo Nape hakuwa sahihi ama alikwepa kuzungumzia ukweli wa hali ilivyo. Ni dhahiri kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa bado haijafutwa ila kilichopo ni amri ya kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano.

Kwa maana hiyo, kujaribu kutoa maelezo yanayoonyesha kuwa hakuna sheria inayoruhusu mikutano ya hadhara na maandamano ni kujaribu kupotosha jamii ya kimataifa na wananchi kwa ujumla.

Kama mbunge ambaye kazi yake ni kutunga sheria, Nape alitakiwa atetee sheria ambayo chombo chake kiliiunda kwa kuwa hilo ni moja kati ya makjukumu makuu ya Bunge. Nape pia anaelewa taratibu za kufuata iwapo sheria hiyo imepitwa na wakati na hivyo kunahitajika marekebisho.