Nguvu ya wengi inahitajika utelekezaji watoto

Muktasari:

  • Wanawake hao wamekuwa wakifika hapo kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa Paul Makonda, ambaye alitangaza kuwa ana dhamira ya kuwasaidia wanawake hao ambao ni wakazi wa mkoa wake.

Kwa siku nne sasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, hasa wanawake wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa ajili ya kuwasilisha madai ya kutelekezwa na wenza wao.

Wanawake hao wamekuwa wakifika hapo kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa Paul Makonda, ambaye alitangaza kuwa ana dhamira ya kuwasaidia wanawake hao ambao ni wakazi wa mkoa wake.

Awali wito huo uliitikiwa kwa nguvu na wanawake waliojitokeza kwa mamia katika viwanja vya ofisi ya mkoa, lakini kadiri siku zinavyokwenda baadhi ya wanaume nao wamejitokeza wakidai kutelekezwa.

Ukiondoa wanaume kujitokeza na kudai kutelekezwa, kuna matukio mengine yasiyo ya kawaida yamekuwa yakitokea ikiwamo ya wanawake wenye umri mkubwa kujitokeza wakidai kutelekezwa na baba zao!

Kinachoendelea katika ofisi hizo kimewastua watu wengi hasa kwa kuwa desturi za Watanzania wengi ni kuwa masuala ya kindoa na uhusiano ama hushughulikiwa faragha au hutafutiwa ufumbuzi kupitia vyombo vya kisheria kama Mahakama, ofisi za ustawi wa jamii na viongozi wa dini.

Kama wadau muhimu kwa jamii, jana tukalazimika kuweka bayana maswali 10 yanayoakisi mitazamo ya walio wengi kuhusu uendeshaji wa mchakato wa kusikiliza kero za wakazi hao.

Kwa muhtasari, baadhi ya maswali yetu yalihusu uhalali wa kisheria wa kinachoendelea, ulinzi wa haki za binadamu, uwezekano wa kuwapo kwa mgongano wa kitaasisi, usawa wa kusikiliza malalamiko, kuwapo kwa ajenda nyuma ya kampeni hiyo na namna gani mila na desturi za Kitanzania zimezingatiwa kuhusu suala la malezi.

Ni vyema mamlaka husika zikajibu na kufanyia kazi maswali haya na mengineyo yanayoumiza vichwa vya watu ili mwishowe mchakato mzima uonekane kuwa na maana.

Tusipofanya hivyo, sio utakuwa ni mchakato unaopoteza muda kwa wananchi, maofisa wanaoshiriki, lakini pia utazidi kuupa nguvu mtazamo wa baadhi ya watu kuwa pengine mchakato huo una ajenda maalumu.

Mwananchi hatutetei vitendo vibaya vya utekelezaji wa watoto, wanawake au waume. Ni vitendo vinavyopaswa kupigwa vita na kila mtu. Tatizo tunaloliona ni namna mamlaka husika inavyoendesha mchakato huo, huku ikionekana kujiweka kando na mitazamo ya wengi kama inavyoonekana kupitia maswali haya.

Hatupaswi kulichukulia suala hili kama jambo la mtu mmoja au chombo kimoja cha Serikali. Ni suala mtambuka na kwa kuwa lina sura ya kijamii zaidi, vyombo mbalimblai vya kiserikali, asasi za kiraia, madhehebu ya dini, vilipaswa kushiriki ili kutafuta dawa ya tatizo.

Kama ulivyo msemo wa wahenga; kwenye wengi hakuharibiki jambo, mchakato unaoendelea sasa katika ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam ulipaswa kuratibiwa kupitia ushiriki wa vyombo vingi zaidi ili kuondosha dhana mbalimbali zilizojengeka katika fikra za watu.

Kwetu sisi ushiriki wa taasisi nyingi zaidi, sio tu ungeufanya mchakato uwe na tija, lakini pia unaweza kusaidia kuepusha athari zinazoweza kujitokeza ikiwamo kuongezeka kwa mitafaruku kati ya wanandoa, kukomoana, utapeli, kuumizana kisaikolojia na athari nyinginezo.