FURSA 2016: Ni fursa ya thamani ya mazao Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka

Muktasari:

  • Miongoni mwa waliojiandaa kwa hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka.

Neno milioni 50 za JPM siyo geni masikioni mwa Watanzania. Ni ahadi iliyotolewa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na Rais John Magufuli na iko mbioni kuanza kutekelezwa.

Fedha hizi zinakusudiwa kutolewa kwa kila kijiji nchini kwa ajili ya kusaidia shughuli za ujasiriamali miongoni mwa wananchi, lengo likiwa ni kukuza uchumi wa mwananchi mmojammoja na jamii kwa ujumla.

Viongozi kuanzia ngazi ya wilaya na mikoa hivi sasa wanafanya maandalizi kuhakikisha fedha hizo haziyeyuki kama ilivyokuwa kwa zile zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Nne maarufu kama mamilioni ya JK.

Miongoni mwa waliojiandaa kwa hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka. Anasema ameshaweka mikakati thabiti kuhakikisha kuwa fedha hizo siyo haziishii mikononi mwa wajanja wachache, bali zinakuwa chachu ya mabadiliko chanya ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wake.

“Moja ya mikakati yetu ni viwanda vidogovidogo vya kusindika mazao ya kilimo kulingana mahitaji, mazao yanayozalishwa katika eneo husika na rasilimali zilizopo  mkoani Simiyu,” anasema Mtaka

Anataja viwanda vitakavyojengwa kupitia mamilioni ya JPM kuwa ni vya kusindika mazao ya pamba vikiwamo vya kusokota nyuzi na kuzalisha mafuta ya pamba ili kuongeza thamani ya zao hilo badala ya kuuza pamba ghafi kama inavyofanyika sasa.

“Kwa sababu Simiyu pia tunalima viazi na mihogo, tutajenga viwanda vidogo vya kusindika mazao haya vikiwamo vya biskuti za viazi na mihogo,” anasema na kuongeza: “Katika mkakati huo, tutajenga pia viwanda vidogo vya kusindika mazao ya mifugo kama maziwa, nyama na ngozi.”

Anasema Simiyu pia kutakuwa na mashine za kisasa za kukoboa mpunga ili kuwawezesha wakulima kuuza mchele uliofungashwa vyema na kuongezewa thamani badala ya mpunga.

“Lazima tuwe na mikakati ya kuwasaidia wananchi wanapopokea fedha hizi. Tukiwaacha wajiendeshe wenyewe, hazitatumika katika mazingira yaliyo salama, zitaisha na kubaki wanalalamika,” anasema Mtaka.

Anasema miradi itakayoanzishwa kupitia fedha za JPM itabuniwa, kumilikiwa na kuendeshwa na wananchi wenyewe kupitia uongozi wa Serikali za vijiji, kata, wilaya na mkoa, lakini chini ya ushauri na uangalizi wa wataalamu wa masuala ya uchumi, biashara, maendeleo ya jamii, ushirika na usimamizi wa fedha.

Anaamini kuwa kwa njia hii, lengo la Serikali ya Rais Magufuli la Tanzania ya viwanda, litatimia kuanzia ngazi ya vijiji ambako ndiko msingi wa uzalishaji mali.

Simiyu kinara wa pamba

Licha ya ukweli kwamba Mkoa wa Simiyu ndiyo unaozalisha asilimia 40 ya pamba yote inayolimwa nchini, wakazi wake hawajanufaika vya kutosha kwa zao hilo,” anasema Mtaka. Anasema chini ya uongozi wake, zao la pamba lazima lichukue nafasi yake katika kuchangia uchumi wa mkulima mmojammoja na mkoa kwa ujumla.

“Tunakusudia kuwajengea mazingira mazuri wakulima wa pamba ili siyo tu walime kwa tija na kunufaika, bali pia zao hilo litoe mchango unaostahili katika maendeleo na uchumi wa Simiyu. Kwa kuanzia, tutakomesha mchezo wa danadana ambao kila mamlaka inayohusika na maendeleo ya zao la pamba huirushia mpira mamlaka nyingine kuhusu suala la kudorora kwa kilimo cha pamba.”

Katika mkakati huo, Mtaka anasema kila mdau kuanzia mkulima, wakala wa vipimo, Bodi ya Pamba, wataalamu pamoja ngazi zote za Serikali, atalazimika kutimiza wajibu wake katika kufufua zao hilo.

Anasema kuanzia msimu wa kilimo, maofisa ugani wote mkoani Simiyu shughuli zao zitakuwa vijijini kwa wakulima kuwashauri mbinu na njia bora za kulima kwa tija badala ya mtindo wa sasa ambao wengi wao hushinda maofisini huku wakiandaa taarifa bila kuonana na wakulima.

Historia ya mabilioni ya JK

Katika Awamu ya Nne chini ya Jakaya Kikwete, Serikali alitoa zaidi ya Sh50 bilioni kusaidia wajasiriamali wadogowadogo.

Kati ya fedha hizo, Sh43 bilioni zilizokuwa zikitolewa kupitia benki za CRDB, NMB na Posta ndizo zilizoangukia kwenye mikono salama na kurejeshwa huku Sh7 bilioni zikiyeyuka.

Pamoja na kutokuwapo maandalizi ya kutosha, fedha hizo zilizopitishwa kwenye vikundi na vyama vya Akiba vya Kuweka na Kukopa (Saccos), zilitolewa kiholela huku baadhi ya viongozi wakiwamo wanasiasa wakidaiwa kutengeneza majina feki na kujikopesha.