Ni haki kufanya biashara, zingatia sheria

Muktasari:

  • Hivyo, kufanya kazi au biashara halali ni haki ya kikatiba ya kila raia nchini. Pamoja na Katiba kutoa uhuru wa kufanya biashara kwa mujibu wa sheria, zipo sheria nyingine zinazotumika kushughulikia mambo mbalimbali yanayohusiana na biashara.

Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinatoa ruhusa kwa kila Mtanzania kufanya biashara au kushiriki shughuli yoyote halali za kumuingizia kipato. Zinatoa uhuru wa mtu kufanya kazi na kupata ujira au kufanya biashara itakayomuingiza faida.

Hivyo, kufanya kazi au biashara halali ni haki ya kikatiba ya kila raia nchini. Pamoja na Katiba kutoa uhuru wa kufanya biashara kwa mujibu wa sheria, zipo sheria nyingine zinazotumika kushughulikia mambo mbalimbali yanayohusiana na biashara.

Baadhi ya Sheria hizo ni kama ile ya kampuni, majina ya biashara, benki na taasisi za fedha, ununuzi wa bidhaa na ya masoko ya hisa na mitaji. Pamoja na haki ya kikatiba iliyopo, sheria nyingine zilizopo zinapaswa kuzingatiwa pia.

Sheria hizi zote zinakusaidia kujua namna unavyoweza kusajili, kuendesha pamoja na kupata au kukuza mtaji ikiwa ni pamoja na kuwekeza fedha zako katika maeneo salama kwa mustakabali mzuri wa biashara yako.

Ni muhimu ukatambua aina ya biashara ambayo unataka kuisajili ili ikupe fursa ya kujipanga na kujua mahitaji muhimu unayopaswa kuyazingatia. Usajili unasimamiwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela). Ofisi hii ina mamlaka ya kusajili biashara yoyote.

Zipo aina mbalimbali za usajili ambazo ni pamoja na ule wa kampuni ambayo inaweza kuwa binafsi au ya umma ama yenye mtaji wa hisa au isiyo na mtaji wa hisa. Hivyo ni muhimu ukafahamu ni aina gani ya kampuni ungependa kuisajili.

Vilevile, unaweza ukasajili biashara katika mfumo wa ubia au partnership. Hii ni biashara inayojumuisha watu, kikundi au taasisi zaidi ya moja kwa ajili ya kufanya biashara waliyoikusudia.

Aina nyingine ni usajili wa biashara binafsi. Hii ni biashara ya mtu au familia moja tu kama mhusika mkuu katika biashara hiyo. Yeye atawajibika kwa kila kitu kinachohusiana na biashara hiyo zikiwamo taratibu za benki na taasisi nyingine za fedha.

Kwa mujibu wa Brela, biashara ya ubia na binafsi zinasajiliwa kupitia mtandao wake kwa mhusika kufuata maelekezo yote yanayohitajika ikiwamo kufanya malipo. Unaweza kuomba ushauri kwa wanasheria ili wakusaidie kukamilisha usajili.

Unahitaji kusajili biashara yako sasa. Ukilinganisha faida utakazopata kwa kufanya hivyo utagundua kusajili biashara ni rahisi na nafuu sana. Faida za kusajili biashara yako na kuifanya itambulike kisheria na iwe rasmi ni nyingi zaidi kuliko changamoto utakazokutana nazo.

Kusajili biashara kunakupa utambulisho rasmi wa kibiashara na uhalali thabiti wa kisheria. Kunaipa anuwani kibiashara yako. Kutakufanya uaminike na jamii ikiwa ni pamoja na taasisi za fedha na kukufanya ukopesheke. Kutajenga imani kwa wateja na kutakuza jina na mustakabali wako kibiashara.

Ukitaka kufanikiwa kibiashara lazima uwe tayari kulipa gharama. Usiogope gharama zitakazokupeleka hatua ya juu zaidi. Kiwango cha mafanikio yako kinategemea uhakika wa biashara yako.

Biashara yako ikiwa haitambuliki, mafanikio yako hayatotambulika pia. Kumbuka, mafanikio huja pale maandalizi yanapokutana na fursa. Fanya maandalizi leo, usisubiri kesho kusajili biashara yako. Hakuna lisilowezekana, chukua hatua.

Hata baada ya kusajili biashara yako, zipo hatua kadhaa unazopaswa kuzizingatia. Biashara bora na yenye mafanikio haiishii hatua ya usajili na kupata cheti tu, ni lazaima uende mbele zaidi kuifanya iwe na uwezo wa kuanza kazi rasmi kisheria.

Japo si lazima michakato yote ifanyike kwa wakati mmoja lakini ni muhimu kujiwekea malengo ya namna gani unaweza kuifanya biashara ianze rasmi. Baada ya kusajiliwa itahitaji namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika ofisi iliyopo karibu na mahali biashara yako ilipo au mahali utakapoweka ofisi ya biashara yako.

Namba ya utambulisho lazima isome jina la biashara na iambatane na cheti cha kuthibitisha malipo ya kodi (Tax Clearance Certificate). Baada ya kumalizana na TRA ni muhimu kwenda halmashauri na kukata leseni ya biashara zitakazokusaidia kupata nyaraka muhimu endapo utahitaji kufungua akaunti ya biashara benki.

Ni muhimu kufungua akaunti benki kwa jina la biashara ili kujenga mfumo mzuri wa fedha na kuleta imani kwa wateja ambao mara nyingi hupenda kufanya malipo kwenye akaunti ya biashara na si ya mtu binafsi. Kama wengine wameweza na wewe unaweza pia. Amau sasa.

Kuwa rasmi sokoni kwa kila unachokifanya ni uamuzi wako wa busara utakaofungua fursa nyingi nyingine.

Mwandishi ni wakali. Kwa ushauri na maoni, anapatikana kwa 0755 545 600.