Ni mwanzo, mwisho wa upinzani Kilimanjaro?

Muktasari:

  • Hakuna ubishi kuwa upinzani ni itikadi au imani na si rahisi kuua upinzani kama itikadi. Lakini je, pale ambapo waumini wengi wa itikadi hii wanapoamua kuachana nayo inatokea nini?

Katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa kitovu cha upinzani, lakini ndani ya miaka mitatu ya awamu ya tano hali imekuwa tofauti kabisa.

Hakuna ubishi kuwa upinzani ni itikadi au imani na si rahisi kuua upinzani kama itikadi. Lakini je, pale ambapo waumini wengi wa itikadi hii wanapoamua kuachana nayo inatokea nini?

Mwaka 1995 kukiwa na vuguvugu kubwa la mageuzi kupitia kwa mgombea urais wa NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema, upinzani ulinyakua majimbo sita kati ya tisa ya Mkoa wa Kilimanjaro. NCCR-Mageuzi ilichukua majimbo ya Moshi Mjini, Siha, Hai, Moshi Vijijini na Vunjo na Rombo likachukuliwa na Chadema huku CCM ikichukua majimbo ya Same Mashariki na Magharibi.

Historia hiyo inaonyesha mwaka 2000, CCM ilifanikiwa kukomboa majimbo ya Rombo na Vunjo, lakini 2005 CCM ikafanya kazi kubwa ya kisiasa na kukomboa majimbo yote isipokuwa Moshi Mjini.

Ushindi huo uliuamsha upinzani ambao mwaka 2010 ukarejesha majimbo ya Rombo na Hai na kutetea jimbo la Moshi Mjini, lakini 2015 ulivunja rekodi na kunyakua majimbo saba kati ya tisa.

Chadema pekee ilifanikiwa pia kupata kata 145, vitongoji 910, vijiji 4,72 na mitaa 38 katika chaguzi za 2014 na 2015.

Lakini tangu kuingia madarakani Serikali ya awamu ya tano, tunashuhudia wimbi la viongozi wa kisiasa wakiwamo wa kuchaguliwa na wananchi wakijiuzulu.

Sababu kubwa ya kujiuzulu kwao inafanana, kwamba wanaamua kuachana na vyama vya upinzani na kujiunga na CCM ili kumuunga mkono Rais katika kuleta maendeleo.

Kwa upande wa wabunge na madiwani waliojiuzulu, wengi wao walipewa nafasi ya kugombea tena nafasi hizo kwa tiketi ya CCM na kushinda, na ushindi wao haujapingwa hadi sasa.

Hakuna ubishi kipindi kifupi cha utawala wake, Rais Magufuli amefanya mambo makubwa ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na kuboresha shirika la ndege (ATCL) kwa kulinunulia ndege mpya.

Si hivyo tu, amerudisha nidhamu ya utumishi wa umma, amedhibiti mianya ya ukwepaji kodi na ufisadi, amesimama kutetea haki za wanyonge zilizokuwa zikikandamizwa, na haya ni machache tu.

Nimetangulia kuuliza ni mwanzo au mwisho wa upinzani Kilimanjaro, kutokana na kile kinachojitokeza sasa katika mkoa huo, hasa matokeo ya chaguzi ndogo zinazoendelea kufanyika.

Katika jimbo la Hai, Rombo, Moshi Mjini na Siha, madiwani waliojiuzulu kutoka upinzani na kujiunga na CCM, kote huko CCM imeshinda pamoja na jimbo la Siha kupitia kwa Dk Godwin Mollel.

Kwa mwenendo huu wa uchaguzi na matokeo, ni wazi hata chaguzi ndogo zinazotarajia kufanyika katika wilaya za Same na Moshi mjini, bado kuna uwezekano CCM kuzichukua.

Haikutarajiwa Chadema ingeshindwa katika kata za jimbo la Hai linaloongozwa na Freeman Mbowe.

Mbowe ndiye mwenyekiti wa Chadema, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na mwenyekiti mwenza wa Ukawa, hivyo matokeo hayo yanaibua maswali mengi kuliko majibu.

Ni kweli wananchi wa Kilimanjaro wameamua kuutosa upinzani walioishi nao hata kabla na baada ya uhuru na baadaye katika mfumo wa vingi vya siasa? Kama hawajautosa, nini kinatokea sasa?

Au chaguzi zinazoendelea sasa si huru na haki? Kama hivyo ndivyo, mbona hakuna kesi yoyote ya kuhoji chaguzi hizo? Kama wengi wanamuunga mkono Rais, itatokea nini katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Kiukweli hiki kinachotokea sasa ni kiashiria kibaya kwa vyama vya upinzani kuelekea chaguzi za viongozi wa Serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020.

Upinzani lazima sasa uzinduke kutoka usingizini vinginevyo watakumbuka shuka wakati kumekucha kwani malalamiko ya kuwapo figisufigisu hayatawasaidia kama hawatachukua hatua ya kukabiliana nayo.