Ni rahisi kupata leseni ya biashara, itafute

Muktasari:

  • Kwa hivi sasa leseni zimegawanywa katika makundi mawili A na B. Katika kundi A kuna biashara zenye mtaji mkubwa ambapo hujumuisha leseni za uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, huduma za mawasiliano, bandari, vilabu vya usiku na uuzaji na usambazaji wa silaha na risasi.

Leseni ya biashara ni kibali ambacho hutolewa na mamlaka husika kwa mfanyabiashara au mtoa huduma. Mwanzoni leseni za biashara zilikuwa zinatolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara pekee lakini hivi sasa halmashauri zinaruhusiwa kufanya hivyo kwa daraja fulani.

Kwa hivi sasa leseni zimegawanywa katika makundi mawili A na B. Katika kundi A kuna biashara zenye mtaji mkubwa ambapo hujumuisha leseni za uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, huduma za mawasiliano, bandari, vilabu vya usiku na uuzaji na usambazaji wa silaha na risasi.

Biashara nyingine ni usafirishaji wa mafuta mazito, bima, huduma za utalii, benki na taasisi nyingine za fedha pamoja na maduka ya kubadilishia fedha. Leseni za biashara za kundi hili hutolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).

Katika kundi B kuna biashara za migahawa na hoteli za kawaida, vyama vya ushirika, wakala wa bima, usafirishaji wa abiria, viwanda vidogo, udalali, vipuri, utaalamu au ushauri, uuzaji wa bidhaa jumla na rejareja.

Biashara za kundi B leseni zake hutolewa na halmashauri ya eneo husika ambako biashara inafanyika. Leseni hizi zinatolewa na Wizara ya viwanda na Biashara, halmashauri za mikoa na miji pamoja na wilaya chini ya Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Leseni za Biashara namba 25 ya 1972.

Gharama za leseni hizi hubadilika mara kwa mara kulingana na inavyopendekezwa na mamlaka husika. Kufanya biashara bila leseni ni kosa kisheria hivyo ni vyema kuchukua hatua za kurasmisha biashara yako kisheria.

Ili kupata leseni ya biashara muombaji anatatakiwa kuhakikisha nyaraka zote muhimu ili kuepuka usumbufu wa kurudishwa kuondoa mapungufu yaliyopo. Muombaji ni lazima ajaze fomu ya maombi ya leseni zinazopatikana Brela au ofisi za halmashauri.

Wakati wa kuirejesha itatakiwa kuambatanishwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN), mkataba wa kodi ya pango kama sehemu ya biashara umepanga, cheti cha usajili wa kampuni au jina la biashara kutoka Brela, katiba ya kampuni, vitambulisho vya viongozi wa kampuni na cheti cha uthibitisho wa mlipa kodi.

Kwa muombaji wa leseni ya biashara ya huduma za kitaalamu atatakiwa pia kuambatanisha vyeti kutoka katika mamlaka husika mfano, TCRA (kwa leseni za mawasiliano), TFDA na TBS (kwa vyakula au dawa na ubora wake) au EWURA kwa uagizaji na usambazaji wa mafuta.

Pia katika masuala ya sheria, udaktari, uhandisi, urubani au unahodha ni lazima kuwa na hati ya kitaalamu (professional certificates) kuambatanishwa katika maombi ya leseni husika.

Kama nyaraka zilizoorodheshwa hapo juu zitaambatanishwa katika fomu ya maombi ya leseni, basi kuna uwezekano wa kupata leseni yako ndani ya muda mfupi ni mkubwa. Lakini ni lazima nyaraka zote ziwe kamili bila kasoro yoyote.

Kumbuka, leseni ya biashara hulipiwa kila mwaka mara moja tangu tarehe ilipotolewa mpaka ukomo wa matumizi yake.

Leseni utakayopatiwa itakuwa na taarifa zako muhimu mfano namba ya leseni, aina ya leseni, jina la mamlaka iliyotoa leseni hiyo, namba ya mlipa kodi (TIN), jina la kampuni au muombaji wa leseni na aina ya biashara.

Taarifa nyingine zitakazokuwamo ni mahali biashara itakapokuwepo, kiasi cha ada kilicholipwa na namba ya stakabadhi pamoja na tarehe ya malipo. Kutakuwa na maelezo kama leseni hiyo ni mpya au inaendelea, tarehe ya kutolewa na mwisho wa matumizi yake, sahihi ya mtoaji, jina na muhuri wa mamlaka husika.

Upatikanaji wa leseni utakunufaisha sana, kwani biashara yako itatambulika kisheria, itakusaidia wakati wa kufungua akaunti ya biashara, utaweza kukopa fedha kutoka katika taasisi mbambali za fedha, utaepukana na usumbufu wa kufungiwa biashara yako na kufikishwa kwenye vyombo vya dola kama muhujumu uchumi na utasaidia kukuza Pato la Taifa.

Ni muhimu kutambua kuwa kila leseni ni lazima itumike kwa biashara iliyoombewa na si vinginevyo. Kutozingatia hili nikosa ammbalo ukibainika unapaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Kwa kulitambua hilo, kila mfanyabiashara anaruhusiwa kuwa na zaidi ya leseni moja kulingana na wingi wa miradi aliyonayo. Kwa kutowekewa ukomo wa leseni unazoweza kumiliki, adhabu huwahusu wote wanaotumia lesenimoja kwa biashara zaidi ya moja iliyoombewa.

Leseni ni kinga ya biashara yako, epuka usumbufu nenda kachukue leseni yako katika mamlaka husika ili ujitendee haki wewe mwenyewe, biashara husika pamoja na wadau unaohusiana nao kufanikisha mafanikio unayoyakusudia.

Mwandishi ni wakili wa kujitegemea. Kwa ushauri na maoni anapatikana kwa namba 0755 545 545 600 au 0713 636 264