UCHAMBUZI: Ni wakati wa kubadilisha mfumo wa uchaguzi

Muktasari:

Wabunge na madiwani kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitoka kwenye vyama vyao vya upinzani na kwenda CCM, huku wakitoa sababu mbalimbali ikiwamo kuridhishwa na utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Wakati dira ya Taifa ikiwa ni kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, wimbi la wanasiasa kuhama vyao bado linaendelea na kusababisha rasilimali za Taifa kutumika katika kuandaa chaguzi ndogo.

Wabunge na madiwani kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitoka kwenye vyama vyao vya upinzani na kwenda CCM, huku wakitoa sababu mbalimbali ikiwamo kuridhishwa na utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Ni haki ya kila mtu kuhamia chama anachokitaka, hilo haliwezi kuzuiwa. Hata hivyo, tunatakiwa kufikiria juu ya gharama ambazo Taifa hili changa linazilipa bila manufaa yoyote kwa maendeleo yake.

Jambo hilo linanisukuma kutazama njia mbadala ambayo itatuepusha na gharama hizo, lakini pia ikitoa haki kwa wanasiasa kuhamia vyama wanavyovitaka. Njia hiyo ni kubadilisha mfumo wa uchaguzi uwe tofauti na huu tunaotumia sasa.

Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika inatumia mfumo wa FPTP (First Past The Post) ambao unampa nafasi mtu aliyepata kura nyingi kuliko wengine wote. Mshindi anaweza kupatikana hata kwa kumshinda mwenzake kwa kura moja.

Jambo hili limekuwa likiibua mjadala miongoni mwa wanazuoni wakibainisha kwamba kama mshindi wa pili naye kapata kura nyingi, kwa nini naye asishirikishwe kwenye Serikali hiyo kwa sababu naye ana watu wengi.

Kama mshindi amepata asilimia 52 ya kura, wanapendekeza yule aliyepata asilimia 48 naye awepo serikalini kwa sababu ana watu wengi ambao nao ni raia. Hiyo, wanasema itaongeza umoja wa kitaifa na kupunguza uhasama baina ya vyama vya siasa.

Mfumo wa uchaguzi ndiyo unatoa mwongozo wa namna ya kupata viongozi kwa kuzingatia matakwa ya watu. Kila mfumo ni mzuri lakini una changamoto zake inapofika wakati wa utekelezaji.

Hata hivyo, kwa hali inayoendelea hapa nchini ya viongozi kuhama vyama, nadhani kuna kila sababu ya kutumia mfumo wa uwakilishi (proportional representation) ili kuepusha gharama kubwa ambazo zinakwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mfumo huu unampa nafasi mpigakura kuchagua chama ambacho anadhani kina sera nzuri au kinafaa kuongoza nchi. Chama kitakachopata kura nyingi, ndicho kitakuwa na idadi kubwa ya wabunge na kitaunda Serikali.

Mathalan, kama chama ‘A’ kimepata asilimia 40 ya kura zilizopigwa maana yake ni kwamba chama hicho kitapata asilimia 40 ya viti bungeni na chama ‘B’ chenye asilimia 60 ya kura zote kitapata asilimia 60 ya viti bungeni na kuunda Serikali. Inapotokea mbunge wa chama hicho amefariki dunia, amejiuzulu au kahama chama basi chama ambacho kimempoteza mbunge huyo kitajaza nafasi hiyo kutoka kwenye orodha ya watu kiliowateua.

Mfumo huo siyo mgeni hapa nchini kwa sababu ndiyo unaotumika kupata wabunge wa viti maalumu. Inapotokea mbunge wa viti maalumu akahama chama, akafukuzwa au kupoteza maisha basi chama chake kinajaza nafasi hiyo kupitia orodha iliyopo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Tuliona wabunge wanane wa viti maalumu wa CUF walipovuliwa uanachama, NEC ilitangaza mara moja watu wengine wa CUF kutoka kwenye orodha iliyowasilishwa na chama hicho wakati wa uchaguzi kwa kufuata mtiririko.

Uzuri wa mfumo huo ni kwamba hakuna kwenda kwenye uchaguzi tena. Inapotokea kiti kiko wazi kinajazwa na watu wengine kutoka kwenye orodha ya makada wa chama husika kwa sababu kile ni kiti chao.

Pia, gharama za kufanya chaguzi ndogo mara kwa mara zitakomeshwa. Watu wataweza kuhama vyama vyao bila kizuizi chochote wakati shughuli nyingine za maendeleo zikiendelea kufanyika.

Mfumo huo unatumika katika nchi za Ubelgiji, Ugiriki, Finland, Uswisi, Italia, Israel, Luxembourg, Sweden, Denmark, Urusi, Norway na Hungary. Kwa Afrika, mfumo huo unatumika kwenye mabunge ya Afrika Kusini, Burkina Faso na Burundi.

Ipo mifumo mingi ya uchaguzi, lakini kwa Tanzania, nadhani mfumo wa PR utakuwa ni mwarobaini wa gharama zisizo za msingi. Natambua kwamba demokrasia ni gharama lakini gharama hizo sharti ziepukwe katika nchi maskini mpaka pale zitakapojihakikishia ustawi wa maisha ya watu wake.

Ni vyema Serikali, wadau wa siasa na wananchi kwa ujumla wakalitafakari suala hili ambalo kimsingi linakwenda na mahitaji ya mabadiliko ya Katiba. Taifa ni moja na dhamira yetu ni moja kulijenga Taifa hili.

0763891422