Ninatamani kuiona Chaneta ile ya Chiku Shomari

Muktasari:

  • Uchaguzi huo umepangwa kufanyika mkoani Dodoma Septemba 30, ni mwishoni mwa wiki tu hapo.

Ninamtakia uchaguzi mwema kila mshiriki wa anayewania nafasi katika Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta).

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika mkoani Dodoma Septemba 30, ni mwishoni mwa wiki tu hapo.

Uchaguzi huo utawaweka madarakani viongozi wapya kwa miaka mingine minne, kwa ajili ya kuinua mchezo huo.

Ninapotathmini uchaguzi huo, naangalia nyuma kwa waliokuwa madarakani na kupata jibu kuwa hawakuwa na kipya.

Kimsingi netiboli inaonekana kuingia shimoni, inachezwa eneo moja tu, klabu bingwa ya mikoa na baada ya hapo mchezo umemalizika.

Itakumbukwa, mwaka 2013, netiboli ilikuwa juu hata kupanda ngazi mbili, kutoka 19 hadi 17 kutoka katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (IFNA), naweza kusema angalau ilikuwa hatua nzuri kusimamia maendeleo ya mchezo huo.

Ilifika hatua netiboli ya Tanzania ilipata alama 1,205 na kuzishinda nchi zinazosifika kwa mchezo huo ikiwamo Ireland, Malaysia, Singapore, Uswisi, Namibia, Zambia, Marekani na Sri Lanka.

Kwa sababu hiyo, wanaotaka kuongoza Chaneta, watambue kuwa kuna changamoto mbele katika kuendeleza mchezo huo hata Tanzania kufika mbali katika ngazi za ubora duniani.

Hakuna miujiza zaidi ya kufanya jitihada katika mchezo huo na kuibua vipaji kwa wasichana na wavulana wenye vipaji.

Kuna vijana wengi ambao wana uwezo, hivyo ni wajibu wa viongozi watakaoingia madarakani kutoa changamoto kwa taasisi mbalimbali kama Polisi, Magereza, JWTZ, JKT kuanzisha timu za vijana kwani ndiyo wenye nafasi ya kuwarithi wachezaji waliopo sasa.

Mfano rahisi, kulikuwa na timu ya Jeshi Stars ambayo ilikuwa ikifanya vizuri, lakini wakasahau kutengeneza timu ya vijana.

Baadhi ya wachezaji waliokuwapo kina; Grace Daudi (marehemu), Magreth Fundi, Specioza Budodi, Christina Kimamla, Mwajabu Said, Rose William kutaja wachache ambao sasa wamestaafu na matokeo yake timu hiyo imepoteza mataji kwa kusahau kuandaa wengine.

Zilikuwapo pia timu za Bandari, Mapinduzi Dodoma, Tanesco, Bima, Madawa, Muhimbili, NBC, Bohari Kuu, Kurugenzi na nyingine nyingi lakini sasa hazipo.

Wakati wa Chaneta ya Katibu Mkuu, Chiku Kirundu (Chiku Shomari), netiboli ilikuwa juu mno na kuwa na msisimko. Nakumbuka ilifika hatua, netiboli ilikuwa ya pili baada ya soka kwa wapenzi, lakini sasa tujiulize ni ya ngapi?

Chaneta inatakiwa kuhamasisha kuundwa kwa timu za vijana katika ngazi za mitaa na ikiwamo kujenga viwanja inapostahili.

Chaneta iwe karibu na wadau wake kuhakikisha kila programu ya chama inatekelezwa kwa maendeleo ya netiboli Tanzania.

Netiboli na hata michezo mingine, inatakiwa kupiga hatua za mbali.

Itapendeza leo kila mmoja kuona Chaneta ya Anna Kibira inarudisha enzi zile za Mama Chiku Shomari akiwa katibu mkuu mwajiriwa wa Serikali.

Msisimko, kupendwa na kuhamasisha watu, ni wazi netiboli inaweza kuvuta hata wadhamini na wataigombania kuliko ilivyo sasa.

Netiboli kwa sasa haivutii, ni kama imepoteza mwelekeo. Sasa kama ni hivyo, nani atawekeza pasipo na msisimko?

Ukweli ni kwamba enzi za Mama Chiku Chaneta ilikuwa ‘active’ kweli na tulishuhudia mchezo huo ukipiga hatua kubwa.

Baada ya kustaafu, taratibu mchezo ulianza kushuka. Ulianza kupoteza mwelekeo wake na haukuwa tena na mvuto.

Kulifanyika mashindano, lakini hakukuwa na msisimko kwa wakati ule. Ilifika hatua mpira wa kikapu ukaipiku netiboli na kushika nafasi ya tatu kwa umaarufu.

Kimsingi, netiboli ni kama imekufa, haipo kama ilivyokuwa wakati ule wa miaka ya 1980 na katikati ya miaka ya 2000. Zaidi ni kutokana na aina za viongozi waliopo madarakani ambao ama hawana nia hasa kuinua mchezo huo au uwezo wao wa kuongoza ni mdogo.

Katikati ya miaka ya 2000 walau kasi yake ilirudi kidogo chini ya Anna Bayi ambaye muda wake ulipoisha, hakutaka kuwania tena kutokana na madai ya kutopewa ushirikiano.

Kweli kuna kazi kubwa ya kuinua mchezo huo katika ngazi mbalimbali kwani siku hizi hata kwenye shule za msingi na sekondari hausikiki tena.

Miaka ya nyuma, mashindano ya shule kwa shule, baada ya soka ilifuata netiboli, siku hizi hata walimu wa mchezo huenda hata hawapo.

Ndiyo maana ninasema, watakaoingia madarakani Jumamosi ijayo, wajue kuna changamoto za kuinua netiboli kuanzia Mtwara hadi Kagera.

+255 655 264 003