Njombe inavyokabiliwa na utapiamlo mkali licha ya chakula kedekede

Muktasari:

  • Takwimu zinaonyesha Njombe ni kati ya mikoa vinara wa uzalishaji wa mazao ya chakula ingawa umo kwenye orodha ya iliyoathirika kwa watoto wenye udumavu kwa asilimia 49.4. Taarifa iliyosomwa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo (RCC) Septemba 2017, unakadiriwa kuvuna zaidi ya tani milioni 1.35 za mazao ya chakula na kuwa na ziada ya tani milioni 1.06 kwani mahitaji yake ni tani 171,771 tu.

“ Sijui kwa nini mtoto wangu anaumwa kiasi hiki wakati kila siku anakula mara tatu. Asubuhi, mchana na usiku. Hali yake ilikuwa mbaya na tulikata tamaa. Tusingepata ushauri wa madaktari na kuambiwa ni utapiamlo, mjukuu wetu angepoteza maisha.” Ndivyo anavyosema Josephine Mfumbilwa, mkazi wa Kitongoji cha Igominyi, mkoani Njombe akisimulia hali aliyonayo mjukuu wake.

Bibi huyu anaishi na mumewe Petro Mangula, pamoja na mjukuu wao wa miaka mitatu aliyedhoofu kutokana na ukosefu wa lishe bora. Licha ya kuwa na umri wa kutembea, mtoto huyo hakuwa na uwezo wa kufanya hivyo hadi alipoanzishwa lishe maalum chini ya uangalizi wa mhudumu wa afya ya msingi wa Kijiji cha Nyombo, Leonard Mfikwa. Nyumba ya Mfumbilwa imezungukwa na mashamba yenye viazi, mahindi, maharage na mboga za majani lakini bado mtoto huyo amedhoofika kwa udumavu. Familia ina ng’ombe na kuku wa kienyeji. Kadi yake ya kliniki ya mtoto huyo inaonyesha uzito wake ni kilo nane ingawa alipaswa kuwa na kilo zaidi ya kilo 15.

Baada ya kuhangaika naye sana, wazee hawa waliamini mjukuu wao amerogwa, kabla hawajagundua ni utapiamlo. Mfikwa anasema asingeingilia kati, huenda mtoto huyo angepoteza maisha. Utapiamlo si tatizo linaloitesa familia hiyo pekee. Ni ugonjwa unaowaumiza watoto wengi Njombe licha ya mkoa huo kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara.

Takwimu zinaonyesha Njombe ni kati ya mikoa vinara wa uzalishaji wa mazao ya chakula ingawa umo kwenye orodha ya iliyoathirika kwa watoto wenye udumavu kwa asilimia 49.4. Taarifa iliyosomwa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo (RCC) Septemba 2017, unakadiriwa kuvuna zaidi ya tani milioni 1.35 za mazao ya chakula na kuwa na ziada ya tani milioni 1.06 kwani mahitaji yake ni tani 171,771 tu.

Ofisa lishe wa mkoa huo, Ester Kibona, anasema kiwango cha udumavu kimepungua kutoka asilimia 52 iliyobainika mwaka 2010 mpaka silimia 34 kulingana na takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Takwimu za Baraza la Afya Duniani zinaonyesha katika kika watoto watano wenye umri chini ya miaka mitano nchini, wawili wamedumaa. Ingawa kati ya mwaka 1992 hadi 2014 kiwango cha udumavu nchini kilipungua kwa asilimia 30, idadi ya watoto waliodumaa imeongezeka kutoka milioni 2.4 hadi milioni 2.7 katika kipindi hicho. Shirika la Afya la Dunia (WHO) linaonyesha kila siku, zaidi ya watoto 270 wenye chini ya miaka mitano hupoteza maisha nchini kutokana sababu mbalimbali ikiwamo lishe duni. Sababu Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kipaumbele cha wazazi na walezi wengi wa Njombe ni kazi. Huwa na muda mfupi wa kuhudumia watoto na hawana uelewa wa kutosha wa chakula bora. Kukosekana kwa uelewa wa lishe kamili ni sababu kubwa ya mkoa huo kuongoza kwa udumavu.

Wazazi na walezi wengi wametingwa na shughuli za shamba na kuwasahau watoto.

Familia nyingi zina tatizo hilo ingawa zina akiba ya chakula cha kutosha kukidhi mahitaji ya makuzi ya watoto zilizonao.

Ofisa lishe huyo anasema kutozingatia lishe bora katika siku 1,000 za mwanzo wa maisha ya mtoto tangu mimba inapotungwa mpaka mtoto anapofikisha miaka miwili inachangia kwa kiasi kikubwa mkoa huo kuwa na udumavu.

Anania Danda, mkazi wa Kata ya Kichiwa anasema mara nyingi, kipindi cha kilimo, hulazimika kuwaachia kiporo watoto wake kwa ajili ya chakula cha asubuhi na cha mchana ili amudu shughuli zake bila kupoteza muda.

“Huwa nawaachia kiporo cha ugali na maharage jikoni ninapojihimu shambani,” anasema Danda.

Muuguzi wa Zahanati ya Mlewela, Josephine Nyongole anasema kijiji hicho kina watoto wenye utapiamlo pia kutokana na sababu hizo. Wazazi hawajali lishe ya watoto.

Mganga wa Zahanati ya Nyombo, Leinisa Amulike, anasema utapiamlo ni hatari ikiwa wazazi wengi wataendelea kupuuzia lishe kwa watoto wao. “Wazazi wengi hawajali watoto, hawapangi ratiba kwa ajili ya chakula na wametingwa na kilimo. Hii ni hatari kwa makuzi ya watoto,” anasema.

Mtaalamu kutoka Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita), Lucy Maziku anasema udumavu ni sababu kubwa ya kuugua mara kwa mara kwa mtoto katika siku 1,000 tangu azaliwe.

Nyingine ni taratibu usiofaa wa kuwalisha watoto wachanga na wadogo ikiwamo kutowanyonyesha maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa.

“Unapompa mtoto chakula kisicho na ubora, yaani virutubisho vinavyotakiwa, unamuweka kwenye hatari ya kupata udumavu,” anasema.

Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa mtoto anatakiwa kunyonya maziwa ya mama pekee kwa miezi sita kabla hajaanza kupewa chakula kingine chenye mchanganyiko wa makundi mbalimbali.

Lucy anasema lishe duni ya wanawake kabla, wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua inaweza kusababisha mtoto kupata udumavu.

Hali ya vijijini

Bibi Mfumbilwa hakutarajia katika umri wa zaidi ya miaka 70 atakuja kulea mtoto mwenye utapiamlo. “Kijana wangu anaishi Dar es Salaam. Alimpa mimba binti wa watu wakaja wote hapa. Tulilea mimba hadi alipojifungua. Matokeo yake walipoondoka, mama yake akamtelekeza mwanae na kukimbia,” anasema.

Baada ya kuachiwa mjukuu huyo, anasema hali ya mtoto ilianza kubadilika na hospitali wakaambiwa ana utapiamlo. “Kumbe hatukuwa tunamlisha vizuri,” anasema.

Emilia Lucheza, mkazi wa Kijiji cha Ikuna ambaye mtoto wake alizaliwa akiwa na kilo 3.5 lakini akapungua uzito hadi kilo 1.5 anasema hajui kwa nini mwanae alipata utapiamlo.

“Labda kwa sababu nilikuwa nashinda shambani ndiyo maana mtoto aliumwa, lakini nilikuwa namlisha,” anasema.

Anasema baada ya kupewa rufaa kutoka zahanati ya kijiji hadi Hospitali ya Mkoa wa Njombe na kupata matibabu, afya ya mwanae iliimarika. “Walinifundisha. Siku hizi namsimamia na ninahakikisha kwenye kila mlo nampa matunda,” anasema.

Mhudumu wa afya katika Zahanati ya Ikuna, Safina Sanga, anasema hali ya mtoto huyo ilikuwa mbaya lakini baada ya usimamizi wao amepona.

Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Mlewela, January Nkinda anasema japo baadhi ya watoto wenye utapiamlo kijijini kwake, bado anajifunza namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Athari

Wataalam wa lishe na afya wanasema zaidi ya asilimia 40 ya vifo vya watoto wenye utapiamlo hutokea katika mwezi wa kwanza wa maisha yao. Baraza la Afya Duniani linasema mtoto akidumaa hupata athari zisizoweza kurekebishika kwani hudumu katika maisha yake yote.

Miongoni mwa athari zinazotajwa kwenye kitabu cha baraza hilo cha mwaka 2015 ni udumavu wa akili jambo linaloweza kumfanya mtoto ashindwe kumudu masomo darasani.

“Ikiwa tatizo hili litaendelea kuwakumba watoto, linatishia kuwapo kwa wataalamu wa kutosha siku zijazo,” anasema mtaalamu mratibu wa Panita, Jane Msagati.

Watu wazima ambao walikuwa na udumavu utotoni hupungukiwa uwezo wa kufanya kazi hali inayosababisha kupungua kwa tija na mapato ya kiuchumi.

Ushauri

Miongoni mwa malengo ya Baraza la afya Duniani ni kupunguza idadi ya watoto waliodumaa kwa asilimia 40.

Ofisa lishe wa Njombe, Kibona anasema chini ya ufadhili wa Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) wanaendelea kupambana na udumavu ili kuokoa maisha ya watoto. Anasema Serikali imeamua kulivalia njuga suala hilo ili kuondokana na aibu ya kuwa juu kwa takwimu za utapiamlo.

Mhudumu wa afya Kijiji cha Ikuna, Japheth Ngimbudzi anasema kazi kubwa anayoifanya kijijini hapo ni kuzizungukia familia zenye watoto ili kutoa elimu ya namna ya kuwalisha.

Upo mkakati wa kutoa elimu ya chakula cha watoto, usafi wa mazingira na mwili, malezi na kuzingatia kanuni za afya kupambana na tatizo hilo.

“Wenye utapiamlo tunawasimamia wapate matibabu na tunapambana kuimarisha utoaji wa matone ya vitamini A, dawa za minyoo, upimaji wa hali ya lishe na kutoa rufaa kwa watoto wenye utapiamlo,” anasema.

Kingine kinachofanyika ni kuwafundisha wananchi umuhimu wa kutumia chumvi yenye madini joto pamoja na kuwaelimisha kuhusu uzalishaji, uhifadhi na matumizi ya vyakula vyenye viinilishe vya kutosha kwenye mashamba darasa yaliyopo.